moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Kila ninapoingia ndani ya ndege, kuketi kwenye kiti changu na kufunga mkanda wa usalama, mawazo yangu huanza kusafiri mbali zaidi ya safari ninayoianza.

Ni safari ambayo mara nyingi hunifanya nijiulize swali moja kubwa; ni nani anayehakikisha ndege ninayopanda inapaa salama, inapita angani bila hitilafu na kutua salama katika kituo chake?

Naam, huenda si mimi pekee ninayejiuliza hivi kwa sababu kuna maelfu ya watu ambao nao hutumia usafiri wa anga, kila mwaka.

"Nimewahi kusafiri kwa ndege mara kadhaa. Najua ni usafiri salama na wa uhakika, lakini mara nyingi huwa najiuliza ni nani hasa anayehakikisha kila kitu kinaenda sawa hadi tunafika salama tunakoenda,"

Kauli yake Abel Mathias, Mkazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam, katika mahojiano maalumu na M24 TANZANIA yaliyofanyika hivi karibuni.

Belinda Karia, Mkazi wa Mikocheni, anasema licha ya kufurahia usafiri wa anga, bado watu wengi hawafahamu kazi kubwa inayofanywa nyuma ya pazia kuhakikisha safari zinakuwa salama.

"Tunafurahia kusafiri kwa ndege kwa sababu ni usafiri wa haraka na unaotuwezesha kufika mapema kule tunakokwenda bila kuchoka. 

"Lakini wengi wetu tunawajua marubani pekee na wale wasaidizi wao wanaotupa huduma mbalimbali ndani ya ndege," anasema.

Kwa kauli ya Abel na Belinda nachukua hatua kuelekea Aviation House na moja kwa moja nafika Chuo cha Usafiri wa Anga [CATC].

Swali langu kuu: Je, nyuma ya kila safari ya ndege kuna nani anayehakikisha usalama wa abiria na je, uwekezaji kwa sasa Tanzania tumefikia wapi na tunaelekea wapi, tunapoianza DIRA 2025 - 2050?. 

Nilichokikuta kilinifunulia dunia ambayo abiria wengi hawaioni. Nyuma ya kila safari ya ndege kuna mtandao mkubwa wa wataalamu wanaofanya kazi saa ishirini na nne.

Kundi hili la wataalamu tusiwaona moja kwa moja hushirikiana kwa ukaribu na wale tunaowaona na kwa pamoja uhakikisha anga la Tanzania lipo salama na safari zinakuwa salama.

Kuna waongozaji wa ndege [Air Traffic Controllers], wahandisi wa mifumo ya kuongozea ndege, wataalamu wa taarifa za anga, wakaguzi wa usalama pamoja na wataalamu wengine wengi.

Kwa ushirikiano madhubuti wanafanya kazi kwa usahihi mkubwa ili kuhakikisha kila safari inafanyika kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya usalama.

Katika mahojiano maalumu, Mkuu wa Mafunzo wa Chuo cha Usafiri wa Anga [CATC], Didacus Mweya, anasema wataalamu hao hawapatikani kwa bahati mbaya.

Bali huandaliwa kupitia mfumo madhubuti wa mafunzo unaoendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya sekta ya usafiri wa anga duniani.

Ndani ya CATC wataalamu hao, hujengwa kupitia mafunzo maalum, teknolojia za kisasa na Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika eneo hili.

CATC ni chuo mahususi kilicho chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania [TCAA].

Kwa zaidi ya miaka 40, CATC imekuwa kitovu cha kuzalisha wataalamu wa sekta ya anga nchini na katika ukanda wa Afrika.

CATC imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kuhakikisha usalama wa usafiri wa anga unaendelea kuimarika sambamba na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Chuo hiki kilianzishwa mwaka 1985 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujenga uwezo wa nchi katika kuzalisha wataalamu wa huduma za anga [Air Navigation Services].

Kabla ya chuo hiki Tanzania ilikuwa ikitegemea kwa kiasi kikubwa mafunzo kutoka nje ya nchi, hali iliyokuwa ikiigharimu fedha nyingi na kuchelewesha upatikanaji wa wataalamu.

"Dhima ya kuanzishwa kwa chuo ilikuwa kuongeza idadi ya wataalamu wa huduma za usimamizi wa anga," anasema Mweya.

Anaongeza "Leo hii tumeendelea kukua sambamba na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya sekta ya anga duniani,".

MAENEO KIMKAKATI

CATC imejikita katika maeneo matatu muhimu ya taaluma za anga. Eneo la kwanza ni mafunzo ya waongozaji wa ndege [Air Traffic Controllers].

Kundi hili ni wataalamu ambao huwasiliana moja kwa moja na marubani ili kuhakikisha ndege zinaruka na kutua kwa usalama.

Eneo la pili ni huduma za taarifa za anga [Aeronautical Information Services], ambapo wataalamu hukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa muhimu zinazotumiwa na marubani.

Hatua hizo hufanyika kabla ya safari, ikiwemo hali ya hewa, ramani za anga na taarifa nyingine za usalama.

Eneo la tatu ni uhandisi wa mitambo ya kuongozea ndege, unaohusisha usimamizi wa rada na vifaa vya kisasa vinavyowezesha ndege kuongozwa kwa usahihi kutoka eneo moja hadi jingine.

Kadri sekta ya anga inavyoendelea kubadilika, ndivyo CATC ilivyoendelea kupanua wigo wa mafunzo yake.

"Kwa sasa chuo kinatoa zaidi ya kozi 90 zinazohusu maeneo mbalimbali ya usafiri wa anga," anasema Mweya.

Kozi hizo zinajumuisha mafunzo ya muda mrefu, ya muda wa kati na mafunzo mafupi yanayochukua siku chache.

Mafunzo hulenga kuongeza ujuzi kwa wataalamu waliopo kazini na kuwaandaa wengine wapya kuingia katika soko la ajira.

KINARA AFRIKA

Ubora wa mafunzo hayo umeifanya CATC kutambulika kimataifa, Mweya anabainisha zaidi "Chuo kina ithibati ya International Civil Aviation Organization [ICAO].

"Pia, ni miongoni mwa vituo vinavyotambulika kutoa mafunzo ya usalama wa anga [Aviation Security].

Anasema kutokana na hadhi hiyo, wanafunzi kutoka zaidi ya nchi 19 barani Afrika na maeneo mengine duniani wamekuwa wakija Tanzania kupata mafunzo.

"Leo hii Tanzania imekuwa kituo muhimu cha mafunzo ya usafiri wa anga katika Afrika. 

"Tunafundisha Watanzania, lakini pia tunapokea wanafunzi kutoka nchi mbalimbali kutokana na ubora wa mafunzo yetu," anasema Mweya.

Anabainisha, kabla ya kuanzishwa kwa CATC, wataalamu wengi wa uongozaji wa ndege walikuwa wakisomeshwa katika East African School of Aviation nchini Kenya kwa gharama kubwa.

Kuanzishwa CATC kumeokoa fedha nyingi za kigeni na wakati huo-huo kuiongezea uwezo Tanzania kuzalisha wataalamu wake yenyewe kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyoendana na teknolojia ya sasa.

Mbali na mafunzo ya kawaida ya anga, CATC pia imeingia katika teknolojia mpya ya ndege zisizo na rubani [drones], eneo ambalo linaendelea kukua duniani.

Mweya anasema matumizi ya drones yameongezeka katika sekta mbalimbali kama kilimo, utafiti, upigaji picha, usimamizi wa mazingira na uchoraji wa ramani. 

"Hata hivyo, matumizi hayo yanahitaji kufanyika kwa kufuata sheria za anga ili kulinda usalama wa ndege na abiria.

"Drone inaweza kuonekana ndogo, lakini ikitumika bila kuzingatia taratibu inaweza kusababisha ajali kubwa. 

"Ndiyo maana tumetengeneza kozi maalumu zinazowapa watumiaji uelewa wa matumizi salama ya anga," anasema.

Mbali na mafunzo ya msingi, CATC pia inatoa kozi za utaalamu maalumu katika aerial surveying, aerial mapping na matumizi mengine ya kitaalamu ya drones.

Hatua inayowafungulia vijana fursa mpya za ajira na kujiajiri. Mchango wa CATC hauishii Tanzania pekee. Mweya anasema chuo kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wataalamu kutoka nchi nyingine, Afrika.

"Kuna baadhi ya nchi zinategemea Tanzania katika kujenga uwezo wa rasilimali watu kwenye sekta ya anga.

"Kwa mfano, wataalamu wengi wa uongozaji wa ndege kutoka Burundi wamepata mafunzo yao nchini Tanzania, jambo linaloonesha nafasi ya nchi katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda," anasema.

VIJANA NA FURSA

Kwa vijana wa Kitanzania, Mweya anaona sekta ya anga bado ina fursa nyingi ambazo hazijatumika ipasavyo.

Anasema wengi hudhani ajira katika sekta hiyo zinahusu urubani pekee, wakati ukweli ni kwamba kuna taaluma nyingi zinazohitajika, zikiwemo uongozaji wa ndege, taarifa za anga, usalama wa anga.

Uhandisi wa mitambo, huduma za ardhini katika viwanja vya ndege pamoja na usimamizi wa drones.

"CATC hatuna kozi ya urubani, lakini tunatoa kozi nyingi zinazowawezesha vijana kupata ajira kwenye sekta ya anga na tumepunguza gharama za mafunzo ili Watanzania wengi waweze kuzimudu," anasema.

Kadri Tanzania inavyoendelea kupanua viwanja vya ndege, kuongeza idadi ya safari za anga na kuwekeza katika uchumi wa buluu na utalii, mahitaji ya wataalamu wa anga yataendelea kuongezeka.

Kwa mazingira hayo, CATC imeendelea kuwa nguzo muhimu ya kuhakikisha Tanzania haijengi tu miundombinu ya kisasa ya usafiri wa anga, bali pia inazalisha wataalamu wenye uwezo.

Lengo hasa ni wataalamu hao wawe na ujuzi thabiti wa kuisimamia sekta muhimu za usafirishaji kwa viwango vinavyotambulika duniani na kufikia malengo ya DIRA 2025 - 2050.

Nyuma ya kila ndege inayoruka salama katika anga la Tanzania, kuna hadithi ya uwekezaji katika elimu, teknolojia na watu.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement