Na Veronica Mrema
"Ule ugonjwa wa Siko Seli naujua, ni upungufu wa damu, nimewahi kuona mtoto wa jirani yangu anaugua. Lakini kusema ukweli, sijui unasababishwa na nini?."
Hii ni kauli ya mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina moja, Mariam Jumanne Mkazi wa Msanga Kisarawe, Mkoani Pwani.
Pwani kama ilivyo maeneo mengine kadhaa nchini Tanzania, kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa Siko Seli.
Siko Seli ni miongoni mwa Magonjwa Yasiyoambukiza [NCDs] ambayo yanashika kasi hivi sasa duniani.
Shirika la Afya Duniani [WHO] limekuwa likisisitiza mataifa kuchukua hatua za ziada kuyakabili ili kuokoa raia wake.
Ni kwa muktadha huo, kambi maalum ya uchunguzi wa afya ya macho, meno, uzito wa mwili, Siko Seli na ushauri wa lishe imefanyika ndani ya Msanga, Kisarawe.
Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli Tanzania imeshirikiana na Serenox Afrika kutoa elimu kuhusu Siko Seli pamoja na uchunguzi wa awali.
Kambi hii maalum iliandaliwa na Tanzania Health Opportunities [THO] Juni 5, mwaka huu. Mwitiko wa wananchi ni mkubwa, zaidi ya watu 200 wamejitokeza kwa ajili ya uchunguzi wa afya na ushauri.
Watoto zaidi ya 10 walichunguzwa kinasaba cha Siko Seli na kati yao wanne walibainika ni wagonjwa.
Lakini licha ya umati kuwa mkubwa kwenye eneo hili, lakini si wengi kati yao walikuwa na utayari wa kuchunguza hali zao na hata baadhi yao hawakuwa na utayari kuchunguzwa watoto wao.
Suala ambalo linaonesha wazi kuna juhudi za ziada zinapaswa kufanyika katika kukabiliana na ugonjwa huu.
Kwa sababu takwimu za Wizara ya Afya zinaeleza kuna watu wapatao 15% - 20% ambao hawajijui hali zao za vinasaba, hali inayoongeza hatari ya kuzaliwa kwa watoto zaidi wenye ugonjwa wa Siko Seli.
"Tumebaini mambo makubwa matatu, katika kambi hii na tathmini inatupa picha kwamba bado tuna kazi kubwa ya kufanya kusaidia jamii,".
Meneja wa Kliniki wa Serenox Africa Dkt. Mizinga Moonze amesema hayo katika mahojiano maalum na M24 TANZANIA.
"Jambo la kwanza ni chanya, kwamba jamii hii tuliyoifikia, wengi wanafahamu kuhusu Siko Seli, mtu anakuambia ni ugonjwa wa upungufu wa damu, maana yake elimu imemfikia kwa sehemu anafahamu.
"lakini bado kuna pengo la ufahamu kwa maana ya namna gani ya kudhibiti ili mtu asiwe na ugonjwa huu, hapa nimeona tatizo lipo, watu wengi hawajui namna ya kudhibiti.
"Yaani ule uelewa kuhusu ugonjwa bado hauendani na uelewa wa namna ya kuudhibiti kikamilifu ili kuepusha ongezeko la idadi ya wanaougua," amebainisha.
Jambo jingine lililobainika ni baadhi ya wazazi na walezi ambao watoto wao wanaishi na ugonjwa wa Siko Seli [SCD] bado hawaelewi namna ya kufuatilia madhara yanayoweza kusababishwa na ugonjwa huo.
"Kwa mfano, hawajui wafanye nini kumuepusha mtoto na changamoto nyingine zinazoweza kutokea kwa sababu ya Siko Seli kwa mfano utapiamlo na ukuaji duni,' amebainisha Dkt. Mizinga.
Hezron Benson ni mkazi wa eneo hili amesema "jamii yetu huku bado kuna changamoto ya uelewa kuhusu Siko Seli.
"Binafsi naufahamu kwa sababu mtoto wa ndugu yangu mmoja anaishi na ugonjwa huu wa Siko Seli na hapa nimekuja wanichunguze pia, nijue hali yangu" amesema.
Kuna umuhimu mkubwa wa kuhamisha mkazo kutoka kwenye uelimishaji wa uelewa wa ugonjwa kwenda kwenye elimu ya usimamizi wa muda mrefu.
".., ikiwemo ufuatiliaji wa kitabibu na lishe kwa wagonjwa," amesisitiza Dkt. Mizinga.
Kuna pengo la jinsi pia, ni jambo jingine lililobainika katika eneo hili. Kwa mujibu wa Dkt. Mizinga ushiriki wa kundi la wanaume ni mdogo kuliko wanawake.
"Unaona wanaokuja zaidi kwenye meza yetu ni wanawake, wanaume ukiwaambia karibu upate elimu, wanaonesha hawapo tayari, wanapita pembeni kabisa, au wanaokuja ni wachache mno.
"Hii inaonesha bado kuna pengo kubwa la jinsi katika ushiriki wa mapambano dhidi ya ugonjwa huu,".
Ameongeza "Hali hii ni changamoto kwa kuwa Siko Seli huathiri familia nzima na inahitaji ushirikiano wa pamoja.
"Lakini wanawake ndiyo wameonesha kujali zaidi na kujihusisha, hasa katika uangalizi wa watoto na usimamizi wa dawa pamoja na lishe majumbani [kwa wale waliofika na watoto wao wanaougua].
“Wanawake wanajali sana, lakini bado wanahitaji elimu zaidi. Wao ndio wanaofuatilia dawa na lishe nyumbani,” amesema.
Dkt. Mizinga amesisitiza kuna umuhimu wa kuwawezesha zaidi wanawake katika usimamizi wa afya.
Changamoto ya tatu iliyobainishwa ni hofu na uelewa mdogo kuhusu tofauti kati ya uchunguzi wa awali [screening] na vipimo vya ki-tabibu.
"Badhi ya wanajamii waliofika hapa wanaogopa kupima kutokana na dhana potofu kwamba wanaweza kugundulika mambo yasiyotakiwa au hofu ya sindano!.
“.., wengine wanaamini kama hawakupimwa wakiwa watoto basi hawapaswi kupima sasa,” amesema Dkt. Mizinga.
Amesisitiza uchunguzi wa mapema ni muhimu hasa kwa vijana wanaotarajia kuingia kwenye ndoa na kuanzisha familia.
Changamoto hiyo imeonesha wazi pia kuna ulazima kwa jamii kuendelea kupatiwa elimu zaidi kuhusu tofauti kati ya uchunguzi wa awali 'screening' na vipimo vya uchunguzi wa kina.
"Hii itaepusha mkanganyiko wa kiuelewa walionao baadhi ya watu ndani ya jamii," amesema.
Licha ya changamoto hizo, kuna matumaini kwani jamii inaendelea kupokea elimu kwa uwazi zaidi kupitia kampeni mbalimbali.
"Programu zetu zijazo zitajengwa kwa kuzingatia uzoefu tulioupata hapa Msanga Kisarawe, ili kuboresha mawasiliano, kupunguza imani potofu na kuongeza uelewa wa jamii.
“Tunahitaji kuondoa imani potofu na kuhakikisha watu wanaelewa kuwa usimamizi ni muhimu. Siko Seli si hukumu ya maisha. Kuna matumaini,” amesisitiza Dkt. Mizinga.

Chapisha Maoni