moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Uamuzi wa kuchunguza afya yako kujua kama umebeba kinasaba cha Siko Seli au la, kabla ya kuamua kuzama kwenye huba na penzi nzito na mwenza wako, ni hatua unayopaswa kupongezwa kwa dhati.

Kundi la wanawake limechukua hatua kubwa zaidi ndani ya Chuo cha Elimu ya Biashara [CBE] kuliko kundi la wanaume.

Hatua hii inaleta mtizamo mpya kwamba, sasa vijana wa kike / wanawake wanaendelea kufikishiwa elimu sahihi kuhusu kinasaba hiki na kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuamua kuanzisha familia.

Tanzania bado haipo kwenye ngazi nzuri kimataifa, kwa sababu inashika nafasi ya nne kwa idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa Siko Seli.

Takwimu za Wizara ya Afya Tanzania zikionesha pia kuna ongezeko la watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo kutoka 11,000 kwa mwaka hadi 14,000 hali ambayo inahitaji hatua zaidi kuifikia jamii.

Joyce Lawrence ni mwanafunzi chuoni hapo, amesema baada ya kupatiwa elimu, alipata hamasa kubwa ya kufanyiwa uchunguzi wa hali yake.

"Nimepima na kupata majibu yangu baada ya muda mchache tu, najihisi faraja kubwa kwa hatua hii, sina ugonjwa na sijakutwa na kinasaba, vijana wasiogope wajitokeze kuchunguza,' ametoa rai.

Suala la elimu kuhusu ugonjwa huu, umuhimu wa kuchunguza kinasaba cha Siko Seli mapema kabla ya kuamua kuingia mahabani na kuanza kupata mtoto /  watoto ndipo ulipo haswa.

Kwa sababu, ni miaka mingi sasa, ugonjwa wa Siko Seli umeendelea kuwa miongoni mwa changamoto kubwa za afya zinazoathiri maelfu ya watoto na familia nchini Tanzania.

Licha ya maendeleo ya huduma za afya, wataalamu wanasema bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kuhakikisha vijana wanapata elimu sahihi na kupima mapema kujua iwapo wamebeba kinasaba au la.

Kampeni ya KETAN SCD imefikishwa CBE na Bone and Blood Foundation ikishirikiana na Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli, jambo moja lilijitokeza wazi. 

Wanachuo wengi walionesha hamu ya kujifunza kuhusu Siko Seli, huku wanawake wakionekana kuwa na mwitikio mkubwa zaidi katika kuuliza maswali na kutaka kufahamu hali zao.

Jumla ya wanachuo 4000+ wamepatiwa elimu ya Siko Seli, zaidi ya 92 wamefanya uchunguzi wa kinasaba. 

Hali hiyo inaonesha namna vijana wanavyoanza kutambua umuhimu wa elimu kuhusu ugonjwa huo.

"Kwa kweli mwamko wa kina dada umekuwa mkubwa kuliko wakina kaka, ni jambo lililonivutia. Hata waliokuwa curious na walihitaji kujua zaidi kuhusu Siko Seli walikuwa wakina dada,”.

Daktari Rhobi Jeremiah kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili [MUHAS] amesema hayo katika mahojiano maalum na M24 TANZANIA MEDIA.

Amesema miongoni mwa sababu zinazowasukuma wanawake kutafuta elimu kuhusu Siko Seli ni kushuhudia kwa karibu athari za ugonjwa huo kwa watoto na familia zinazowalea.

“Nakumbuka kuna dada aliniambia yeye ameshudia mtoto aliyekuwa anaishi kwenye mazingira magumu pamoja na mama yake kwa sababu ya Siko Seli,'.

Ameongeza "Hivyo, alisema hatamani kupitia yale aliyoyaona kwa yule mama na mtoto,”.

Kwa mujibu wa Dkt. Rhobi, mara nyingi wanawake hutambua kwa karibu zaidi changamoto ambazo hutokana na ugonjwa fulani, ikiwamo huu wa Siko Seli.

Kwa sababu wao ndiyo hubeba jukumu kubwa la malezi na matunzo ya watoto.

“Wakina mama sisi tuna huruma sana na hatutamani kupata mtoto atakayekuja kuteseka na ambaye mwisho wa siku tutakuwa tunamhudumia,” amefafanua.

Amesisitiza pamoja na mwitikio huo mzuri kutoka kwa wanawake, elimu kuhusu Siko Seli inapaswa kuwafikia vijana wote bila kujali jinsia.

“Jamii yote inatakiwa ijue na ichukue hatua. Mama au dada akijua atatamani kile alichojua kifanye kazi kwa sababu suala hili linaathiri familia nzima,” amesema.

Kwa kampeni hiyo, wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza na kufanya uchunguzi wa Siko Seli sambamba na elimu nyingine za afya.

Mkurugenzi wa Bone and Blood Foundation, Neema Mohamed, amesema elimu waliyopatiwa vijana wa CBE na uchunguzi wa kinasaba ni 'silaha' muhimu ya kuvunja mduara wa Siko Seli.

Amesisitiza kijana anapojitambua anafanya uamuzi sahihi pindi anapoanzisha mahusiano, hivyo ni wazi itasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa Siko Seli.

“Nawahamasisha watu waweze kujihusisha kwenye makongamano kama haya tunatoa elimu ya Siko Seli. Jamii ione hiki kitu ni kikubwa na wajihusishe ili tuvunje mduara huu,” anasema.

Anasema familia nyingi bado zinaendelea kubeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huo kutokana na ukosefu wa taarifa na uchunguzi wa mapema.

“Siko Seli inauma. Kulea mtoto mwenye changamoto vitu vingi vinarudi nyuma,” amesema.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi CBE Mnandwa Mnandwa ameshukuru kufikishwa kwa kampeni hiyo ndani ya chuo hicho.

"Tuko karibu 15,000 wanafunzi ndani ya siku moja kuna wimbi la 8000 hadi 9000 wanakuwa na vipindi siku hiyo, kwa kuwa ni asubuhi hadi jioni kuna kuwa na wanafunzi wengi.

"Tumepewa elimu kuhusu magonjwa mbalimbali na kulikuwa na upimaji wa Siko Seli," amesema.

Amesema vijana wanahitaji taarifa sahihi ili waweze kufanya maamuzi bora kuhusu afya zao na maisha yao ya baadaye.

Dkt. Rhobi amehimiza vijana kuchukua hatua, kujitokeza kwa wingi mahali ambapo kampeni hiyo itawafikia ili wapate elimu na fursa ya kuchunguza hali zao.

Amesisitiza, kwa sababu bado kuna vijana wengi ambao hawajui hali zao za vinasaba licha ya kuwa katika umri wa kuanzisha familia.

“Idadi ya watoto wanaozaliwa na Siko Seli inaongezeka. Vijana hawajui hali zetu na elimu bado ni ndogo. 

"Ukienda kuuliza wanaonyoosha mikono ni wale wenye watoto, lakini wengine wamekaa na hawajui kama wana vinasaba vya Siko Seli,” amesema.

Ameongeza kuwa kuwekeza katika elimu na uchunguzi wa mapema kwa vijana ni hatua muhimu katika kupunguza athari za ugonjwa huo kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement