Na Veronica Mrema
Tanzania imeendelea kuchukua hatua kubwa katika kuimarisha usalama wa anga, kwa usimikaji wa vifaa vya kisasa vya teknolojia na vinavyoendana na wakati [latest version].
Vifaa vya kisasa vinawawezesha wataalamu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga tanzania [TCAA] kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kufuatilia usalama kwa viwango vya kimataifa vya usafiri wa anga.
M24 TANZANIA imetembelea Aviation House ya TCAA iliyopo ndani ya viwanja vya Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara [SABASABA].
Afisa Taarifa za Anga wa TCAA, Kennedy Kaaya, amesema TCAA ina jukumu la msingi la kusimamia usalama, ulinzi na ufanisi wa sekta ya anga nchini kwa mujibu wa Sheria ya Usafiri wa Anga.
Kaaya amesema huduma za uongozaji wa ndege nchini zinahusisha makundi matatu muhimu.
Ni pamoja na waongozaji wa ndege [Air Traffic Controllers], wahandisi wa mifumo ya uongozaji, na Maafisa wa Taarifa za Anga [AIS] wanaosambaza taarifa muhimu kabla na wakati wa safari za ndege.
Kaaya amesema Tanzania inaendelea kuhamia mifumo ya kidijitali ili kuongeza ufanisi na kupunguza matumizi ya karatasi.
Mhandisi ]Air Navigation Engineer] Cleophace Charles amesema uwekezaji mkubwa umefanyika katika mifumo ya kiteknolojia ya uongozaji ndege.
"Ikiwemo mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji hadi kutua salama, inayosaidia ndege kutua hata katika hali mbaya ya hewa.
Usalama wa anga unategemea zaidi ubora wa miundombinu na matengenezo ya mara kwa mara ya vifaa vya uongozaji.
Mhandisi Cleophace amesisitiza TCAA inaendelea kuboresha viwango hivyo kulingana na miongozo ya International Civil Aviation Organization [ICAO].
"Kwa sasa TCAA tunatoa huduma katika viwanja 15 vya ndege nchini na tuna malengo ya kuhakikisha sekta ya anga inachangia kikamilifu maendeleo ya taifa kupitia Dira ya Maendeleo 2050.
Mamlaka hiyo imewahimiza wananchi kutembelea maonesho ya Sabasaba pamoja na makao makuu yake Aviation House ili kujifunza zaidi kuhusu namna sekta ya usafiri wa anga inavyofanya kazi.


Chapisha Maoni