Na Veronica Mrema
Ulinzi wa afya ya mlaji [mteja] na usalama wake na mazingira yake kwa ujumla kwa bidhaa aliyonunua kwa ajili ya matumizi, unaendelea kufuatiliwa kwa ukaribu hasa nyakati hizi za kasi ya kidigitali.
Tume ya Ushindani [FCC], nchini Tanzania imezidi kupanua wigo zaidi wa ufuatiliaji thabiti ikiwa ni pamoja na kujiimarisha mifumo yake ki-digitali pia kisheria.
FCC pia inatambua nguvu na thamani ya kalamu ya waandishi wa habari katika kujiimarisha kwa sababu sekta hiyo nyeti inafikia walaji wengi zaidi, huku ikihimiza zaidi habari za uchunguzi kuibua yaliyo gizani.
"Wananchi wanajua mengi kupitia kalamu za wanahabari, hivyo FCC tumejipanga kufanya kazi kwa ukaribu na kutoa ushirikiano wote unaohitajika kwa manufaa ya Watanzania,".
Kaimu Mkurugenzi wa FCC Khadija Ngasongwa amesema hayo alipokuwa akifungua semina ya siku moja kwa waandishi wa habari za masuala ya biashara na uchumi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Ameongeza "Kuna marekebisho ya Sheria yamefanywa na Bunge mwaka jana yameongeza majukumu ya FCC, ikiwemo mamlaka ya kurekodi alama za bidhaa kwa lengo la kuwalinda walaji.
Pamoja na maboresho hayo, pia wanajiimarisha mifumo yao kidigitali ili kufuatilia mwenendo wa bidhaa na soko, akitolea mfano...
"Bidhaa nyingi kusajiliwa BRELA, ni muhimu kwa FCC kurekodi na kutambua mnyororo mzima wa thamani wa bidhaa hizo ili kuimarisha ufuatiliaji na uwajibikaji.
"Kurekodi bidhaa maana yake unaifahamu; ukimfahamu mzalishaji, msambazaji mkuu, msambazaji mdogo na wakala, inarahisisha kufuatilia pale tatizo linapotokea,” amesisitiza.
Amebainisha "Utekelezaji wa sera ya repair, replace and refund ili kuhakikisha mlaji anayenunua bidhaa yenye kasoro anapata haki yake bila usumbufu.
"Kwa mfano unanunua laptop, ina waranti ila inafanya kazi siku moja au mbili haifanyi tena, unaenda kulalamika dukani hawakusikilizi na kutatua, ukija kwetu tunamuandikia barua muhusika,
"Akishaona barua yetu, anashughulikia tatizo lako. FCC [imeendelea] kuweka mifumo ya kisheria ambayo itawezesha ngazi ya awali ya utatuzi wa migogoro kati ya mlaji na mfanyabiashara.
Ngasongwa aliongeza kuwa udhibiti wa bidhaa una mchango mkubwa katika usalama wa nchi, hasa kwa bidhaa nyeti kama dawa, viuatilifu, vifaa vya umeme na ujenzi.
"Bidhaa hizi ni muhimu mno kuzifuatilia kwa sababu zisipodhibitiwa zinaweza kuathiri afya, mali na nguvu kazi ya Taifa.
"Kupitia mfumo wa TAMOGA unaounganishwa na forodha chini ya TRA pamoja na taasisi kama TBS na TMDA, FCC ina uwezo wa kufuatilia bidhaa zinazoingia nchini," amesema.
Hatua hiyo inawezesha pia kupunguza urasimu pamoja na gharama zisizo za lazima kwa wafanyabiashara na walaji.
Amewataka waandishi kuimarisha habari za uchunguzi ili kusaidia kuibua kasoro na mienendo isiyo ya haki katika soko.
Taarifa wanazoziibua zinaweza kuwa nyenzo muhimu kwa FCC kuchukua hatua na kuimarisha ushindani wa haki.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam [DAR-PC], Mary Mashina, amesema semina hiyo imekuwa ya manufaa makubwa kwa wanahabari.
"Imetupa uelewa wa kina kuhusu mabadiliko ya sheria za ushindani na alama za bidhaa na tunashukuru Kaimu Mkurugenzi umesema semina ya namna hii itatolewa kwa wanachama wetu pia walio zaidi ya 180.
"Kwa sababu kupitia mwandishi mmoja aliyepatiwa elimu hii, mnakuwa na uwezo wa kufikia wananchi wengi zaidi.
"Chukulia mfano mwandishi mmoja mwenye blog yake yenye wafuatilia 4000, umempa elimu hii maana yake wananchi hao wamefikiwa na elimu kwa usahihi zaidi," amesisitiza.
Ameongeza "Waandishi wakielimishwa vizuri, jamii nzima itanufaika kwa kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
Sambamba na hilo, ameiomba FCC kuendelea kufungua milango na kutoa ushirikiano pale waandishi wanapohitaji ufafanuzi.
Akidokeza, "Mwandishi anapohitaji ufafanuzi akikosa ushirikiano kunaweza kusababisha taarifa kutoka bila maelezo ya kutosha.
"Umetolea mfano wa laptop hapa, kuna wananchi wanaodhurumiwa bila kujua wanaweza kuwasilisha malalamiko yao FCC na kupata msaada.
"Ni jukumu la wanahabari kuifikisha elimu hiyo kwa umma. Tukipewa taarifa sahihi, tutazifikisha kwa wananchi kama inavyopaswa,” amesema.
Amesema DAR-PC ipo tayari kushirikiana kwa ukaribu na FCC katika kuendeleza elimu kwa jamii nzima.


Chapisha Maoni