Uamuzi wa kihistoria kwa kupunguza kwa takribani 90% za leseni kwa watoa maudhui mtandaoni, hatua inayotajwa kuwa mabadiliko makubwa katika safari ya kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
Hatua hiyo imeibua matumaini mapya kwa vijana, hususan wahitimu wa taaluma ya habari, waliokuwa wakilalamikia gharama kubwa za leseni ni kikwazo cha kuingia rasmi katika tasnia ya maudhui ya mtandaoni.
Ada hiyo imepunguzwa kutoka kiasi cha TZS 50,000 kwa kuwasilisha ombi la kupatiwa leseni hiyo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania [TCRA] hadi TZS 10,000 Tu.
Leseni hiyo ilipaswa kulipiwa kiasi cha TZS 500,000 kila mwaka na kuanzia sasa italipiwa TZS 50,000.
Vijana wamepata ahueni kubwa, hatua ambayo inawafungulia mlango wa kipekee wa kuonesha ujuzi wao kupitia uwanja wa majukwaa ya kidigitali [ikiwamo blogs, youtubes na mengineyo].
Ni fursa ya vijana kuitumikia jamii yao kwa weledi na kwa kuzingatia miiko na maadili ya taaluma yao ya habari ambapo waliketi vyuoni na kufundwa na walimu nguli.
Serikali imetangaza punguzo hilo mapema leo katika Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma za Utangazaji nchini [ABC 2026] ulioandaliwa na TCRA.
Hatua hiyo imekuja kufuatilia utafiti wa kina na mikutano ya kimkakati iliyofanyika takribani mwaka mzima kati ya Tanzania Bloggers Network [TBN] na TCRA.
TBN kupitia vikao hivyo ilijenga hoja madhubuti kwa Serikali ikichambua namna vikwazo vya gharama vilivyokuwa vinakwamisha uandishi wa habari wa kidigitali nchini.
Kwa mantiki hiyo, hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kurasimisha shughuli za wahabarishaji wa mitandao.
"Ada ya leseni kwa watoa maudhui mtandaoni imeshushwa kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000 tu, huku ada ya maombi ikiwa ni Sh10,000 pekee,".
Ametangaza Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma katika mkutano huo.
Mageuzi hayo pia yamegusa kundi la wakusanyaji wa maudhui [Online Content Aggregators], ambao ada yao imeshushwa kutoka Sh1,000,000 hadi Sh100,000 pekee.
Kundi jingine la "Amateteur" limeanzishwa ili vijana wanaochipukia ili waweze kujitambulisha rasmi na kukuza vipaji vyao bila vikwazo vya kifedha.
TEKNOLOJIA DSB
Mageuzi mengine yaliyotangazwa katika mkutano huo ni ujio wa teknolojia mpya ya utangazaji wa redio ya kidigitali nchini [Digital Sound Broadcasting - DSB].
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari amesema teknolojia hiyo itaanza kufanya kazi katika mikoa mitano ya majaribio ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, na Mbeya.
Lengo la kuanzishwa kwa DSB ni kuongeza ubora wa sauti na huduma za utangazaji nchini. Dkt. Bakari amesisitiza:
"Tumekamilisha maandalizi yote ya kiudhibiti na watoa huduma wa miundombinu wameshapatikana.
"Hii ni hatua kubwa ya kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani na kuimarisha utangazaji, hususan maeneo ya vijijini,".
UTAFITI: REDIO BADO KINARA
Ni nyenzo iliyotumiwa kwa karne nyingi katika kupata maudhui mbalimbali, redio bado imeendelea kuwa kinara nchini Tanzania.
Mhandisi Andrew Kisaka wa TCRA amewasilisha matokeo ya utafiti wa hali ya utangazaji kwa mwaka 2025/2026, na unaonesha redio inaendelea kuwa chanzo kikuu cha habari kwa 85% ya Watanzania.
Hata hivyo, utafiti huo umebaini ukuaji mkubwa wa matumizi ya intaneti miongoni mwa vijana.
Utafiti unaeleza 45% ya Watanzania hupata habari kupitia mitandao ya kijamii kabla ya kusikiliza redio au kutazama televisheni.
Upande wa televisheni, utafiti unaonesha 65% ya watazamaji wanatumia ving'amuzi, huku maudhui ya ndani yakipendwa zaidi kwa 70%.
Serikali imewahimiza watoa huduma za kienyeji kuwekeza zaidi kwenye majukwaa ya kidijitali (OTT) ili kukidhi mahitaji ya soko la sasa.
ULINZI HAKIMILIKI & MIKOPO
Kwa ajili ya kuhakikisha wanahabari wa kidijitali wanufaika na kazi zao, Serikali imezielekeza taasisi za COSOTA na TCRA kuandaa mpango wa kulinda hakimiliki na kudhibiti uharamia mtandaoni.
Serikali pia imeanza kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa watengeneza maudhui kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.
Hadi kufikia Desemba 2025, TCRA imetoa jumla ya leseni 707 za utangazaji, zikiwemo 318 za maudhui mtandaoni, jambo linaloashiria kukua kwa uhuru wa habari na demokrasia nchini Tanzania.


Chapisha Maoni