Na Veronica Mrema
Anga ni tulivu, jua kwa mbali upande wa mashariki naliona likianza kuchomoza. Ni mapema alfajiri nipo kituo cha daladala tayari kuanza safari.
Heka-heka za siku mpya zimeanza ndani ya Dar es Salaam, watu ni wengi barabarani kumekucha. Napanda daladala iliyofika tayari kuelekea mjini kati.
Nafika salama na kuingia ndani ya viunga vya Shule ya Sekondari Azania [boys], namsalimu mlinzi kisha naelekea walipotuandalia kwa ajili ya tukio la kipekee, lililotuleta hapa.
Namuona Daktari Kanza, huyu ni mwenzetu katika Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli Tanzania.
Tunasalimia na ananipa taarifa “Karibu, ila umechelewa kidogo mno. Ndiyo tumetoka mstarini punde kuzungumza na wanafunzi, ila uongozi umetutaka tusubiri mpaka saa tatu hivi tuanze tukio letu,”.
Ninacheka kidogo na kumueleza “Ndiyo jiji letu hili Daktari, yaani unadamka mapema unafika kwa kuchelewa,” tunacheka kwa pamoja na stori za hapa na pale zinaendelea.
Tumeketi kwenye kimbweta kimoja kilichopo eneo hili. Punde wanafika vijana wapatao watano na kwenda kuketi kwenye kimbweta kilicho jirani kidogo na sisi.
Mmoja wa vijana hao amevaa miwani, tunawaona wakiwa wanajadiliana jambo fulani. Kisha yule aliyevaa miwani anakuja pale tulipoketi sisi.
Anatusalia, tunaitika kisha anatuuliza “Je, tunaweza kuanza kuchangia damu sasa hivi? Nipo na wale wenzangu tupo tayari kujitolea,”.
Daktari Kanza anamueleza, “Karibuni sana, lakini itabidi tusubiri kidogo, wenzetu punde wanakuja si mbali na hapa wanakuja na vifaa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH].
Kijana yule mtanashati anaitika kwa tabasamu, kisha anaelekea walipoketi wenzake anawadokeza, wanaonekana kukubaliana kusubiri kidogo, wanaondoka wakiahidi kurudi punde tutakapoanza.
Nasi tuliendelea na hadithi za hapa na pale, dakika chache mbele wakafika maafisa wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama wa Kanda ya Mashariki [EZBTS-MNH] na kuanza maandalizi yao.
Waliambatana na Mkurugenzi wa Bone and Blood Foundation Neema Mohamed, anatueleza “Sasa tunaanza tukio letu”.
Nikawaona vijana tena wale wakirejea eneo la tukio na wakawa sehemu ya wale wa kwanza ambao walijitolea damu.
Sasa ilibidi nimuite yule kijana mwenye miwani “Unaonekana
kijana jasiri na mwenye nidhamu sana. Hongera kwa kuchangia damu,” nilimueleza
naye alipokea.
M24 TANZANIA: Mimi ni
Veronica Mrema, ni mwandishi wa habari kitaaluma, pia ni Afisa Habari na
Mawasiliano ya Umma wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli Tanzania.
KIJANA: Oh! Nashukuru kukufahamu, mimi ni Godfrey James, mwanafunzi wa hapa Azania. Nimefurahi mno leo mmekuja shuleni kwetu, tumepata elimu kuhusu Siko Seli na kuhamasishwa uchangiaji damu.
M24 TANZANIA: Je,
unaweza kudhani kwanini nimekuita wewe kwa mahojiano na si wale wengine?
JAMES: Hapana, nimekuwa ‘very surprised’ na ningependa kujua.
M24 TANZANIA: Ulikuja
na wenzako mapema mno tukiwa hapa hata vifaa vikiwa bado havijafika, mlitaka
kuchangia damu. Nikapenda ujasiri wenu na utayari wenu. Mmekuwa na mtizamo
tofauti na vijana wengine ambao huogopa kujitokeza.
JAMES: Binafsi ilikuwa ndoto yangu ya miaka mingi sana, siku moja niwe mchangia damu. Sasa mwalimu wetu alivyotueleza kuhusu ujio wenu, nilifarijika sana na nikaanza kuhamasisha wenzangu tusisite kabisa kujitolea damu.
M24 TANZANIA: Ndoto
yako ya miaka mingi. Una maana gani?
JAMES: Nikiwa kijana mdogo, ambaye ameanza kujitambua, jirani yetu mmoja alifariki dunia akiwa katika hatua za kujifungua. Nilisikia wakisema amefariki kwa kuishiwa damu. Nikawa najiuliza maswali mengi, kumbe inaweza kutokea mtu kuishiwa damu? Nikamuuliza mama yangu siku moja akanieleza ni kweli inaweza kutokea mtu akaishiwa damu.
Nikawa naendelea kukua, mimi ni mpenzi wa taarifa za habari pamoja na filamu. Baba yangu nyumbani hupendelea kuweka ITV na pamoja tunaangalia habari, nikawa naona madaktari wanahamasisha watu kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wengine. Nikaanza kupata hamasa.
Kuna filamu moja pia niliwahi kuitazama nikaona kisa cha namna hiyo na nikaona kuna ambao walienda kujitolea damu kuokoa maisha ya mtu aliyekuwa anahitaji, ikasaidia kuokoa uhai wake. Basi nikazidi kupata hamasa zaidi. Siku moja nikamwambia mama, nipeleke hospitali nikajitolee damu.
M24 TANZANIA: Ukiwa na umri wako mdogo au ulishafikia umri wa miaka 18 ambao ndiyo haswa wanahimizwa kuanza kujitokeza kuchangia damu kwa hiyari?
JAMES: Akitabasamu. Nilikuwa mdogo [anacheka], nimepata tu hamasa. Mama akaniambia bado sijafikia umri, kwa hiyo itabidi nisubiri. Nilikuwa naomba Mwenyezi Mungu nifikie umri huo. Lakini nilipofika miaka 17 ndiyo nimeanza shule hapa Azania.
Kuna taasisi pia ilikuja, nikazungumza na daktari, nikamuelezea shauku yangu, aliniambia kwa kuwa nimekaribia umri husika, watanipima uzito na wingi wa damu, ninaweza kuchangia au la! ndiyo nikajua kumbe kuna suala la uzito na wingi wa damu pia. Basi waliona nimefikia vigezo hivyo, wakanipa nafasi. Siku hiyo nilifurahi mno.
Kwa hiyo, hii ni mara yangu ya pili kuchangia damu na sasa nina furaha zaidi kwa sababu nimetimiza umri wa miaka 18 furaha yangu ni kwamba ile nia yangu ya tangu nikiwa kijana mdogo, kusaidia kuokoa uhai wa mwengine, nimeifikia. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu.
M24 TANZANIA: Hongera
sana, kwa simulizi yako sasa naelewa kwanini ulikuwa wa kwanza kufika hapa
ukiwa umeambatana na wale wenzako, bila shaka ulifanya juhudi kubwa kuwahamasisha?
JAMES: Ni kweli kabisa, nimekuwa nazungumza nao tangu mwalimu alipotupa taarifa ya ujio wenu, ni zaidi ya vijana 30 niliozungumza nao, wengi wao walikuwa na uwoga, kuna taarifa nyingi potofu kuhusu uchangiaji damu mitaani. Kuna maswali mengi walikuwa wananiuliza. Kuna aliyeniambia wanasema ukichangia damu utaishiwa, utakufa.
Kuna aliyesema ukichangia damu utakuwa unaumwa mara kwa mara na hoja nyinginezo nyingi. Mimi nikawaambia wanitazame mbona nimechangia damu na sijapata tatizo lolote. Pia niliwatoa hofu si kwamba unafika na damu yako kuchukuliwa, unapewa ushauri nasihi, pia unapimwa uzito na wingi wako wa damu.
Nikawapa na simulizi ya kisa cha yule jirani yetu, niliwaeleza faida za kuwa mchangiaji wa hiyari ni pamoja na kupata kadi maalum inayokutambua hata ikitokea unahitaji msaada ukiwa popote ni rahisi kusaidiwa, basi hawa zaidi ya watano uliowaona wamekuja ndiyo walihamasika, najua wale wengine wataendelea kuelimika na kuhamasika kadri siku zinavyoenda, siku moja nao watafanya uamuzi.
M24 TANZANIA: Kwa
namna unavyoongea unaonekana pia wewe ni mtu mwenye ushawishi shuleni hapa.
JAMES: Ndiyo, mimi ni Rais wa shule ama wengine wanasema kaka mkuu wa shule.
M24 TANZANIA: Oh!
Hongera sana.
JAMES: Nashukuru sana.
M24 TANZANIA: Je, na
vipi kuhusu elimu ya Siko Seli?
JAMES: Tumeipokea vema, daktari ametueleza vizuri namna mtoto mwenye ugonjwa wa Siko Seli anavyopatikana, kwamba ni lazima wazazi wake wote wawili [baba na mama] wawe wamebeba kile kinasaba. Ametuhimiza vijana ni muhimu kufanya uchunguzi wa mapema kujua hali zetu za vinasaba.
Kwa sababu mtu aliyebeba kinasaba cha Siko Seli si rahisi kumtambua kwa macho, anakuwa haugui. Ukipima mapema ukifikia kutaka kuoa unashauriwa pia mwenza wako kupima.
M24 TANZANIA:
Unaonekana somo umelielewa vema. Hebu niambie ndoto zako siku zijazo unataka
kuwa nani ndani ya jamii?
JAMES: Natamani niwe mwandishi wa habari. Pia mjasiriamali na mfanyabiashara mkubwa.
M24 TANZANIA: Mara
nyingi vijana wenye upeo kama wako hunieleza wanataka kuwa madaktari, lakini
wewe ni tofauti, unaweza kunieleza kwanini fani hizo?
JAMES: Napenda kuwa sauti ya wasio na sauti. Napenda biashara kwa sababu najifunza pia kwa familia yangu, wengi walionizunguka ni wachapakazi.
M24 TANZANIA: Je, una
role model wako ambao unawafuatilia?
JAMES: Ndiyo, nampenda mno Godfrey Monyo, wajina wangu namna anavyoripoti ITV huwa namtizama kujifunza. Wafanyabiashara wakubwa pia kama Bakhresa na Mo nawafuatilia kwa ukaribu, naamini siku moja ndoto zangu nitazifikia.
M24 TANZANIA: Upi
ujumbe wako kwa vijana, jamii, wadau na Serikali?
JAMES: Vijana nawahimiza wasiogope kujitokeza kuchangia damu pale wanapoitisha, pia elimu ya Siko Seli ni muhimu kuzingatia kabla ya kuamua kuoa au kuolewa, nenda hospitali ukapime kinasaba. Jamii [wazazi na walezi] napenda kuwasihi wafuatilie nyendo za watoto wao, waendelee kuwapa malezi mazuri, pia wawasaidie kupata taarifa sahihi wanapokuwa na maswali mbalimbali.
Kwa wadau hasa waandaaji wa filamu waendelee kuweka elimu za magonjwa mbalimbali kwenye kazi zao. Jamii pia iwe inawapa muda watoto kujifunza, si kila wakati unampa katuni, anastahili kufurahi ndiyo lakini pia ni muhimu apate msingi mzuri wa elimu ikiwamo hii ya afya.
Kwa Serikali naomba waendelee kushirikiana na wadau kufikisha huduma hizi za elimu hii ya Siko Seli pia hamasa ya uchangiaji damu ili ndugu zetu wenye uhitaji huko mahospitalini waweze kusaidiwa kuokoa uhai.
M24 TANZANIA:
Nashukuru sana James kwa kushiriki mahojiano haya, nakutakia kheri nyingi
kwenye masomo yako.
JAMES: Asante sana pia kwa kunihoji, nimefurahi mno, ujumbe wangu utaifikia jamii kwa ukubwa zaidi. Tunawakaribisha tena na tena Azania Boys.


Chapisha Maoni