Na Mwandishi Maalum
Uwekezaji katika afya ya akili ni mtaji mzuri wa kusaidia binadamu kuwa na maisha bora, yenye fanaka na ukwasi.
Hata hivyo jambo ama elimu hiyo bado halijawafikia wengi, ndiyo maana ndani ya jamii bado kuna ambao wameendelea 'kukumbatia' imani potofu.
Baadhi ya watu bado wana dhana kwamba mtu mwenye tatizo la akili au ugonjwa wa akili amerogwa au amekumbwa na laana matokeo yake ni unyanyapaa.
Nchini Tanzania hivi sasa kunaripotiwa vijana wa vyuo vikuu wanakabiliana na changamoto ambazo hazionekani moja kwa moja, ambazo huathiri afya yao ya akili.
Mizozo ya kihisia, presha ya masomo na hali ngumu za kifedha ni baadhi ya vikwazo vinavyopelekea msongo wa mawazo na matatizo ya kisaikolojia.
"Kuna 'presha' nyingi, ya mtu binafsi, masomo, wazazi na walezi unakuta mwanafunzi anatamani amalize akiwa amefaulu lakini mambo mengi yanapoingiliana anapatwa msongo wa mawazo,".
Rais wa Serikali ya Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kairuki [KUSA] Ayoub Daffa amesema hayo katika Kongamano la kwanza la Afya ya Akili waliloliandaa chuoni hapo.
"Tuliona umuhimu wa kuandaa kongamano hili, tukutane tuelezane na wamekuja hapa wanasaikolojia hii ni miongoni mwa hatua tunazoamini zitatusaidia," amesema.
Mwalimu wa Maadili wa Chuo Kikuu cha Kairuki, Abraham Mwalugeni, amebainisha changamoto za kijamii ndani ya vyuo vikuu. 
Amesema wanafunzi, hususan wa kike, wanapaswa kutumia mentors, wataalamu wa saikolojia na madawati ya jinsia. “Usikae kimya, sema shida zako mapema. Hii inaweza kuokoa maisha yako,”.
Mkurugenzi wa Akili Platform Tanzania, Roghat Robert, amesema changamoto za afya ya akili zinaathiri zaidi vijana kutokana na hali ngumu ya uchumi.
Dawa za kulevya na kuporomoka kwa maadili. Akiongeza “Tunawahimiza kuvunja ukimya na kuzungumza na wataalamu.
"Programu za kutembelea vyuo vikuu zinafanya kazi ya kuwalinda kabla ya kurejea kwenye jamii,” amesema.
Profesa Mstaafu wa masuala ya Afya ya Akili, Profesa Gadi Kilonzo, amesema kwamba takribani watu milioni 450 duniani wanakabiliana na matatizo ya akili kila mwaka.
Kati ya hao, zaidi ya milioni moja hufariki kwa kujiua. “Tatizo hili si la Tanzania pekee, ni changamoto ya kimataifa,” anasema.
Profesa Kilonzo ameeleza milioni 150 wanaishi na sonona [depression], milioni 25 wana skizofrenia, milioni 28 wanaugua kifafa na milioni 90 wanakabiliwa na matatizo ya ulevi wa pombe.
Kwa Tanzania, amesema matatizo ya afya ya akili yanakadiriwa kuanzia 0.32% hadi 31 ya wananchi.
Aidha, mahudhurio ya awali katika kliniki za kawaida yakionesha 49% ya wagonjwa wana dalili zinazohusiana na msongo wa mawazo.
“Hii ni ishara kuwa changamoto bado ni kubwa na inahitaji ufumbuzi wa haraka,” amesisitiza.
Profesa Kilonzo ameshauri familia na jamii zinapaswa kuunda mazingira chanya, yenye kuaminiana na kushirikiana.
“Takribani 25% ya familia zina angalau mtu mmoja mwenye tatizo la afya ya akili. Mtu huyo anaweza kuathiri ustawi wa kiuchumi na kijamii wa familia nzima,” anabainisha. 
Pia, amewaonya wazazi na walimu dhidi ya adhabu za mwili, kwani huacha alama za hofu na hasira ambazo zinachangia matatizo ya akili baadaye.
Kwa upande wa uelimishaji na uhamasishaji wa jamii, Rais wa Taasisi ya Waandishi wa Habari za Afya ya Akili Tanzania [TAMHJO] Veronica Mrema,
Amesema ni muhimu vijana na jamii kufuata platform sahihi za elimu na huduma za afya ya akili.
“Waandishi wa habari tuna nafasi muhimu ya kuelimisha na kuhamasisha jamii kutafuta msaada mapema,” amesema.
Amebainisha TAMHJO hadi sasa kwa kushirikiana na Taasisi ya Afya ya Akili Mirembe na Hospitali ya Taifa Muhimbili imewafikia wanahabari zaidi ya 140 kwa mafunzo.
"Mafunzo haya yalifanyika kwa njia ya mtandaoni na ana kwa ana, wamejengewa uwezo namna bora ya kuripori afya na magonjwa ya akili na tumeona mwelekeo chanya.
"Kwa wale waliopewa mafunzo, wana uwezo wa kuchambua mambo na kuibua mijadala ya kijamii na kitaifa katika kuangazia kwa kina eneo hili," amebainisha.
Amesema kupitia kundi sogozi lililoanzishwa waandishi wa habari wana uwezo wa kuwapata wataalamu wa saikolojia na madaktari bingwa wa afya ya akili pale wanapowahitaji kwa mahojiano.
"Hii imetusaidia kuondoa 'gap' lililokuwapo kabla ambapo wataalamu na waandishi wa habari tulikuwa mbali, sasa tunazungumza lugha moja na nia moja, kusaidia jamii yetu,".
Kongamano la KUSA Mental Health Conference liliwaleta pamoja wanafunzi na wadau, kwa lengo la kuangalia tatizo la afya ya akili kwa vijana.
Hatua hizi zinasaidia kuhakikisha vijana wanapata msaada, kujifunza ustawi wa akili, na kuweza kuendeleza ndoto zao bila kuathirika na changamoto zisizohitajika.




Chapisha Maoni