Na
Veronica Mrema
Si
jambo la kukalia kimya tena. Ni mada muhimu, ya lazima na mahususi ambayo
inapaswa mno kuzungumzwa wazi-wazi.
Afya
ya akili si jambo la kulipa kisogo ndani ya jamii. Sasa, vijana wanaamua
kuiweka mezani kama agenda ya wazi kwa hoja madhubuti na mjadala unaohitaji
majibu.
Swali
la msingi ni wapi tulipotoka, tulipo sasa, na tunapoelekea? Visa na mikasa
vimetawala miaka ya karibuni mashuleni, ambavyo vinahusishwa moja kwa moja na
changamoto za akili.
Ndani
ya vyuo mbalimbali imeripotiwa wanafunzi kadhaa kujizuru mathalani kujitoa uhai
na nyuma ya hayo, msongo wa mawazo unatajwa kuwa chanzo kikuu.
Mwalimu
wa Maadili katika Chuo Kikuu cha Kairuki, Abraham Mwalugeni, anasema hivi sasa
changamoto ya afya ya akili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ni kubwa.
“Tunayo
‘challenge’ kubwa ya ‘mental health’. Wanafunzi wanajiua, wengine wanaacha
shule,” anasema kauli ambayo inafungua mjadala mpana, je namna gani
tutajikwamua tulipo?!.
UHALISIA
UPOJE?
Kijana
anapojiunga chuo ana wastani wa mwaka mmoja, miwili, mitatu hadi mitano aondoke
na ‘qualification’ yake anayoitarajia.
“Masomo
yana ‘demand’ kubwa pia kuna ‘presha’ yake binafsi [mwanachuo], kuna ‘presha’
kutoka kwa wazazi/walezi, pia kwa walimu ‘wana-demand’ afikie ‘pass mark’
fulani.
“Mitihani
ya mara kwa mara, kwa hiyo hii inamlazimisha mwanafunzi, kufanya vitu ambavyo
ni nje ya kanuni au matakwa ya kuzingatia kwa mfano kutokulala au kula
vizuri,”
Kauli yake Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Kairuki [KUSA Kairuki] Ayoub Daffa.
Kwa
mujibu wake yote hayo huathiri afya ya wanafunzi na saikolojia yao na matokeo
yake wengi pia hupata matokeo mabaya kwenye mitihani yao.
Mwal.
Mwalugeni anadokeza “Labda mifumo yetu inashindwa kuwapokea [vijana] sawa
sawa,”.
Kauli yake inaungwa mkono na tafiti mbalimbali nchini. Utafiti uliochapishwa katika jarida la BMC Psychiatry kuhusu wanafunzi wa vyuo Tanzania.
Unaonesha
kuwa kiwango kikubwa cha wanafunzi wanaripoti dalili za ‘mental distress’.
Pamoja
na utafiti huo, kuna baadhi ya tafiti nyingine zinaonesha takriban 70% ya
wanafunzi wanakabiliwa na changamoto za afya ya akili kama msongo wa mawazo na
wasiwasi.
Upo,
utafiti uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma unaonesha zaidi ya nusu ya
wanafunzi [51.8%] waliripoti dalili za mental distress.
Watafiti
wanaeleza hali hiyo inaonesha ukubwa wa tatizo ndani ya taasisi za elimu ya
juu.
Ndani
ya Mkoa wa Mwanza, utafiti uliohusisha vyuo visivyo vya tiba ulibaini takriban
35.7% ya wanafunzi walikuwa na dalili za unyogovu .
Takwimu
inayodhihirisha kwamba afya ya akili kwa vijana wa vyuo si hoja ya nadharia,
bali ni uhalisia unaohitaji hatua.
MABADILIKO
GHAFLA
Mwal.
Mwalugeni anasema safari ya mtoto ki-elimu nchini Tanzania hubadilika ghafla
anapofika chuo kikuu.
“..,
kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, mtoto huwa chini ya uangalizi wa wazazi
na walezi. Akiwa sekondari, bado anafuatiliwa kwa karibu na kukumbushwa wajibu
wake wa masomo.
“Lakini
anapofika chuo, anajikuta chini ya utawala wake mwenyewe [utawala na maamuzi
binafsi] na majukumu mapya,” anasema.
Anasisitiza
“Huku chuo ni tofauti na kule msingi na sekondari, hapa hakuna anayekulazimisha
kuandika, kusoma, ni wewe uwe makini na uzingatie ulichokifuata.
“Ninachokiona
mimi, huyu kijana anashindwa ‘ku-transform’ maisha yake,” anaeleza Mwl.
Mwalugeni.
BOOM
‘LINAWAVURUGA’
Anagusia
pia suala la mikopo ya elimu ya juu [boom]. Kwa baadhi ya wanafunzi, fedha hizi
badala ya kuwa msaada wa masomo hugeuka chanzo cha kuyumbisha mwelekeo.
“Akipata
‘boom’ ndiyo linamvuruga kabisa. Kuna ambao wanaacha chuo na kwenda kutumia
fedha walizopata mpaka zitakapoisha ndiyo wanarudi.”
Kwa
mtazamo wake, si suala la fedha pekee, bali ni ukosefu wa maandalizi ya
kisaikolojia na kifedha.
Uhuru
wa ghafla bila mwongozo wa kutosha huwafanya baadhi ya vijana kushindwa
kusimamia maisha yao mapya.
Hapa
ndipo hoja ya wataalamu na tafiti zinapokutana, vijana wengi wanaingia chuoni
bila maandalizi ya kutosha.
Suala
la kukabiliana na presha ya masomo, changamoto za kifedha, mabadiliko ya
kijamii na upweke.
Mambo
hayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa dalili za msongo wa mawazo na
unyogovu.
CHANGAMOTO
YA DUNIA
Kwa
mtazamo wa kitaifa na kimataifa, Profesa Mstaafu wa Afya ya Akili na mshauri wa
Akili Platform Tanzania, Profesa Gadi Kilonzo, anasema tatizo la afya ya akili
si la vyuo na vyuo vikuu pekee.
Ni
changamoto ya dunia nzima, ndiyo maana kumekuwa na juhudi mbalimbali
zinazofanyika na kila nchi ili kukomboa hatma ya raia wake.
Anabainisha
takwimu zinaonesha kuna watu takribani milioni 450 wanaoishi na matatizo ya
akili kila mwaka, huku zaidi ya milioni moja wakijiua kila mwaka.
Pia,
takribani watu milioni 150 wanaishi na sonona [depression], milioni 25 wana
tatizo la skizofrenia, milioni 28 wanaugua kifafa na takribani milioni 90
wanakabiliwa na matatizo ya ulevi wa pombe.
Kwa
upande wa Tanzania, tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa matatizo ya afya ya akili
yapo kati ya 0.32% hadi 31 ya wananchi.
Tafiti
zinaeleza katika kliniki za magonjwa ya kawaida, mahudhurio ya awali yanaonesha
49% ya wagonjwa wana matatizo yanayotokana na msongo wa mawazo.
Mkurugenzi
wa Akili Platform Tanzania, Roghat Robert, anasema vijana ndio wanaoongoza
kuathiriwa na changamoto zinazoathiri afya ya akili.
"Ikiwamo hali ngumu ya uchumi, matumizi ya dawa za kulevya na
kuporomoka kwa maadili," anasema.
TUNATOKAJE?
Mwl.
Mwalugeni anapendekeza kuwepo kwa programu za ‘financial management mentorship’
na ushauri nasaha ndani ya vyuo vikuu.
“Kama
angalau mara moja hadi nne kwa mwaka wanafunzi watapatiwa mafunzo ya usimamizi
wa fedha na maisha kwa ujumla, itawasaidia na itatusaidia sana.”
Afya
ya akili ya vijana vyuoni si suala la mtu binafsi pekee. Ni taswira ya mifumo
yetu ya malezi, elimu na msaada wa kijamii.
Profesa
Kilonzo anasisitiza kila hatua ndogo ya kuimarisha ustawi wa akili ni muhimu,
ikiwemo kuanzisha huduma rafiki za saikolojia, kuelimisha wazazi na walimu.
Pamoja
na kuhakikisha vijana wanapata msaada mapema kabla ya matatizo kuwa makubwa.
Daffa anasema ndiyo maana walichukua hatua zaidi
kuanzisha jukwaa la KUSA YOUTH MENTAL HEALTH CONFERENCE.
“Ni
jukwaa letu muhimu, linatuleta pamoja na wataalamu wa masuala ya afya na
magonjwa ya akili, pia wanasaikolojia, tunajadili kwa uwazi,” anasema.
Anaongeza
“Vijana tunapata kujifunza kati yetu, kuna wale ambao wamewahi kupitia
changamoto basi wanatueleza, mwengine anapata cha kujifunza nia hasa ni
kuijenga afya ya akili tukiwa hapa chuoni.
“Kimsingi,
‘mentorship’ ina umuhimu mkubwa, unajifunza kwa mwenzako aliyewahi kupata
changamoto na unapata kitu cha kukusaidia siku za usoni.
“Moja
ya tiba kubwa ni kuzungumza, mimi ni muumini kabla sijakanyaga hatua moja, mtu
ambaye amewahi kukanyaga hatua ile, nitamfuata na kuzungumza.
“Alipopitia,
alitokaje?, unajua hizi changamoto huja kama ‘suplize’ ila unapofanya ‘recall’
niliwahi kuzungumza na mtu kuhusu hili, alitoka namna gani, unafanya nawe
unatoka salama,”.
Kauli
inayotiliwa mkazo na Mkurugenzi wa Akili Platform, Robert anasisitiza “Tunalenga
kupaza sauti za vijana na kuwahamasisha kuvunja ukimya kwani ukimya hauponyi
afya ya akili.
"Ni
muhimu kuwa na mifumo ya msaada, 'mentorship' na ushauri mapema,” anasema huku
akibainisha suluhisho la muda mrefu ili kunusuru vijana.
Ni
pamoja na kuimarisha eimu na uelewa wa afya ya akili katika jamii na vyuo
vikuu, kuhamasisha utunzaji wa familia na mahusiano chanya.
Kuweka
mikakati ya kutambua na kusaidia mapema vijana wanaokabiliana na msongo wa
mawazo, unyogovu au hali nyingine ya kisaikolojia.
Kuongeza
upatikanaji wa 'mentors', wataalamu wa saikolojia na madawati ya jinsia kwa
wanafunzi wa vyuo
Hii inaashiria kuwa afya ya akili si jukumu la mtu binafsi pekee,
ni jukumu la jamii nzima, vyuo, familia, wadau wa afya na Serikali.
Hatua hizo zitasaidia kuhakikisha vijana wanapata msaada, elimu na fursa za kujenga ustawi wa akili, ili waweze kufanikisha ndoto zao na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Chapisha Maoni