Na Mwandishi Maalum
Tamwa treni lililo konga mioyo ya watu kwa miaka 36
Na Elizabeth Marealle
"Jamani naipenda Tamwa imenisomesha na imenipa fursa mbalimbali. Na sasa mimi ni mwanachama hai nalipia ada kila mwaka."
Haya ni maneno ya mdau ambaye si wanahabari aliyetaka watu wajue kuwa na yeye amependa kushiriki sherehe kubwa iliyoandaliwa jijini Dar es Salamu mwishoni mwa Novemba, kukumbuka miaka 36 tangu TAMWA iundwe. Na si mtu mmoja, wapo marafiki wengi wa TAMWA wanarudia maneno hayo.
TAMWA ni nini? Ni Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania. Na kimepata sifa nchini kwa kujipambanua kuwa miongoni mwa asasi za hiari zinazopigania haki za wanawake na watoto.
Bila kuhama misingi yake ya taaluma ya upashanaji habari; TAMWA imefanya kazi zake kwa kalamu, maikrofoni, kamera na kutumia mbinu ya uchunguzi katika harakati zake za kutetea haki za wanawake na watoto.
Waasisi 13 walioanzisha TAMWA walitoka vyombo vyote, yaani waandishi, watangazaji na wapiga picha za mnato na video. Lakini baadaye wigo wa uanachama uliongezwa baada ya kukua fani ya digiti na teknolojia ya habari. Wakawepo wanawake karibu wote wanaofanya kazi katika vyombo vya habari.
Miaka 36 iliyopita vyombo vya habari vilikuwa ni redio, magazeti na TV chache. Baada ya kukua kwa teknolojia na kuanzishwa mitandao ya kijamii sasa hivi tunazungumzia utitiri wa vyombo vya mawasiliano.
Kwa teknolojia ya sasa wafanyakazi wa vyombo vya mawasiliano, wapende wasipende, wanajikuta kwawa ni watoa habari walio mstari wa mbele. Na hapo ndipo unapoona kwa nini ukitaka kuuza habari ikiwa bado moto huna budi kutumia teknolojia ya mitandao ya kijamii kurusha "video clip" au ufupisho wa habari unayotaka kuiuza haraka.
Kwa hiyo usishangae kwa kuwa uanachama ni hiari kwa wana habari wanawake, TAMWA pia imejikuta ina wanachama marafiki (friends of TAMWA) kutoka kila fani. Na hilo ni jambo la afya ukizingatia usemi huu: "Wewe panda mbegu na sisi sote tule chakula."
Hawa marafiki wameridhika. Wanaona TAMWA ni yao pia. Inafurahisha sana. Maana sherehe ya miaka 36 ilifana sana na baadhi ya vionjo ilikuwa ni kutokana na uwepo wa washiriki toka maeneo mengi.
Kwenye sherehe hizo za tarehe 28 hadi 29 Novemba walikuwepo wanasiasa na wana harakati na hata toka nchi jirani. Pia walikuwepo waheshimiwa viongozi wa ngazi mbalimbali nchini ambao nao walitamka hadharani kuwa: "na mimi ni mwana TAMWA." Tunawashukuru. Tunawakaribisha. Tunawapenda. Hivyo tuingie treni tusafiri pamoja. Asiachwe kituoni hata mtu mmoja maadamu anayetupenda.
Treni letu la TAMWA hoyeeeee.
Picha zote kwa hisani ya TAMWA, zilipigwa katika Maadhimisho ya miaka 36 tangu kuanzishwa kwa Chama hicho.



Chapisha Maoni