moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Unajua kwamba wazo unaloliona dogo leo linaweza kuwa mwanzo wa jambo kubwa litakalookoa maisha ya maelfu ya watu kesho?

Au nikuulize swali lingine. 

Je, vipi basi ungechagua nafasi ya kuunga mkono juhudi zilizoanzishwa na watu wachache lakini sasa zimebadilisha maisha ya watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia matibabu?

Hayo si maswali tu ya kufikirika. Hatua iliyochukuliwa miaka sita iliyopita, Mfuko wa Msaada wa Matibabu wa Muslimah [Muslimah Medical Support Fund - MMSF], ina simulizi ya kipekee.

Taasisi hii ya madaktari wanawake ambao waliunganishwa na jambo moja, imani kwamba mchango mdogo wa kila mwezi unaweza kuwa tofauti kati ya maisha na kifo kwa mtoto anayehitaji matibabu.

Lakini hawakuanza kwa ufadhili wa mamilioni ya shilingi, wala kwa ofisi kubwa, bali kwa kundi dogo la WhatsApp na kujitolea sadaka kila mmoja wao kiasi cha TZS 10,000, kila mwezi.

"Ilianza mwaka 2020, tulikubaliana kuchangia fedha kila mwezi kama sadaka kwa ajili ya kuwakatia bima ya afya watoto kutoka familia zisizo na uwezo," anasema Dkt. Asha Mahita.

Ndiye mwanzilishi mkuu wa wazo hili, akiwa sasa Mwenyekiti wa MMSF Dkt. Mahita anasema wakati huo, lengo lao lilionekana la kawaida kuwasaidia angalau watoto 100 kila mwaka. 

Lakini miaka sita baadaye, matokeo yake yamevuka matarajio yao, kiasi cha TZS 10,000 kimepata thamani kubwa, wameweza kukusanya zaidi ya TZS Mil. 95 na kuwasaidia huduma watoto.

MMSF imeweza kugharamia matibabu ya wengine waliohitaji huduma za dharura, ikiwemo upasuaji.

"Kwa hiyo, tulianza kama kundi la WhatsApp kwa nia ya kutoa sadaka. Tulikubaliana kila mmoja wetu atoe mchango kila mwezi ili kila mwaka tuweze kuwasaidia watoto wasiopungua 100.

"Leo tunashukuru kuona zaidi ya watoto 1,000 wamepata msaada kupitia juhudi hizi," anasema.

Anachanganua hadi sasa watoto zaidi ya 850 wamekatiwa bima za afya, huku zaidi ya 150 wengine wakigharamiwa matibabu kutokana na familia zao kushindwa kumudu gharama hizo.

Mariam Hamisi ni mmoja wa wazazi ambaye amesaidiwa na MMSF kwa kupatiwa bima ya matibabu ya TZS 240,000 kwa mwaka ili mtoto wake aweze kupata matibabu stahiki dhidi ya ugonjwa alionao.

"Nilikuwa katika wakati mgumu, mume alinikimbia, naishi na mama yangu, maisha yetu ni ya kubangaiza, sikuwa na uwezo wa kulipia bima ya mwanangu.

"Mimi ni mfanyabiashara ndogo ndogo tu, natafuta hela ya kula kwa siku napata 2,000 inanitosha na mwanangu, nilikata tamaa maana anahitaji tiba mazoezi," amesema.

Amesema akiwa katika hali ya kukata tamaa alipewa maelekezo na rafiki yake kuwatafuta MMSF na wao walimsaidia bima hiyo, sasa ana tumaini mwanawe anaendelea vema na matibabu. 

Dkt. Mahita amesisitiza "Hatuwapi fedha mkononi, tunalipia matibabu moja kwa moja katika control number ambayo mzazi anakuwa amepewa hospitalini na tumejiridhisha kweli hana uwezo.

Kwa Dkt. Mahita, mafanikio hayo yanaonesha kwamba mawazo makubwa si lazima yaanze kwa rasilimali kubwa. Mara nyingi huanza na watu wachache wenye dhamira ya kutenda.

"Tunafanya kile ambacho Serikali inahimiza, kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanakuwa chini ya bima ya afya," amesema na kusisitiza,

"Lakini Serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake. Tunahitaji wadau zaidi kuungana nasi ili watoto wengi zaidi wapate fursa ya kupata huduma za afya kwa wakati,".

MMSF haichagui watoto kwa kuzingatia aina ya ugonjwa walionao, bali hali ya uchumi wa familia zao. 

"Tunashirikiana na maafisa ustawi wa jamii na wadau wengine kuwabaini watoto wanaohitaji msaada kutoka Tanzania Bara na Zanzibar," amesema.

Licha ya mafanikio hayo, anasema mahitaji bado ni makubwa. Karibu kila siku hupokea maombi mapya ya kulipia bima za afya kupitia control number zinazotumwa kwa taasisi yao.

Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, zaidi ya nusu ya Watanzania ni watoto na vijana, jambo linaloonesha ukubwa wa mahitaji ya huduma za afya kwa kundi hilo.

Dkt. Mahita ametoa rai kwa wadau mbalimbali kuwaunga mkono katika kusaidia kufikia watoto ambao bado wanauhitaji na hawajaweza kuwalipia bado.

"Kwa siku tunaweza kupokea wahitaji 10 au hata 20 na kuna siku hatuna mhitaji,hutegemea siku na siku. Lakini kwa picha hii unaweza kuona kuna uhitaji wa kiwango gani," amesema.

Serikali inatambua juhudi kubwa inayofanywa na MMSF na imeipongeza kwa kusaidia jamii kupitia mfuko huu.

Akimwakilisha Kaimu Waziri wa Afya wa Zanzibar Saada Mkuya kwenye kongamano lililowaleta pamoja wanachama wa MMSF na wadau mbalimbali wa afya, Afisa Mwandamizi wa Serikali na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro [MUM]. Mwantumu Malale amesema hayo.

Amesema "Serikali pekee haiwezi kumudu kutoa huduma zote za afya kwa wananchi bila kushirikiana na wadau.

"Hivyo mchango wa mashirika, wafanyabiashara, watu binafsi, taasisi kama MMSF ni muhimu katika kuongeza wigo wa huduma kwa jamii,".

Amesisitiza kazi iliyofanywa na MMSF inavutia hasa juhudi kubwa waliyoifanya katika kuokoa maisha ya watoto wenye uhitaji.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement