Na Veronica Mrema
Usalama wa abiria, kila ndege inaporuka hadi kutua si jambo la kubahatisha, ni suala linaloangaziwa kwa kina na kufuatiliwa kwa ukaribu, katika kila hatua.
Si rubani pekee anayeendesha 'mwewe' au pamoja na msaidizi wake la hasha, kuna wataalamu wengine wanaotekeleza wajibu sambamba nao.
Nyuma yao pia kuna mfumo mkubwa, madhubuti wa kitaalamu wanaouzingatia kwa pamoja katika utendaji kazi wao, kwa usahihi wa hali ya juu, kila sekunde, kila dakika na kila siku.
Ni mfumo unaounganisha binadamu, teknolojia na taratibu za kimataifa kuhakikisha anga la Tanzania linabaki salama wakati wote.
M24 TANZANIA imefika ndani ya Aviation House, Makao Makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania [TCAA] na kufanya mahojiano haya maalum.
Afisa wa Taarifa za Anga Kennedy Kaaya na Mhandisi [Air Navigation Engineer] Cleophace Charles wanaeleza mambo.
Makala haya yatakupa uelewa jinsi usalama wa anga unavyosimamiwa kwa upekee na umuhimu mkubwa, karibu ufuatane nasi;
MLINZI WA ANGA
TCAA ni taasisi mahususi inayosimamia ulinzi wa anga la Tanzania, Kennedy anafafanua "TCAA tupo na tunasimamia udhibiti wa usafiri na usalama wa anga, kwa mujibu wa Sheria.
Kaaya anasisitiza "Lengo kuu ni kuhakikisha usafiri wa anga unakuwa salama, wa kisasa na unaokidhi viwango vya kimataifa.
MFUMO ULIVYO
Mfumo wa wataalamu wanaoendesha anga unategemea ushirikiano wa makundi matatu muhimu ya mfumo mmoja.
Pia kuna wahandisi wa mifumo ya uongozaji wa ndege wanaohakikisha mitambo ya kiteknolojia inafanya kazi bila hitilafu.
Kundi la tatu ni Maafisa wa Taarifa za Anga [AIS] wanaohakikisha marubani wanapata taarifa sahihi kabla ya safari.
Kaaya anasema Serikali inaendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali inayoboresha utoaji wa taarifa za anga.
Anasema mabadiliko hayo yamepunguza matumizi ya karatasi na kuongeza kasi, usahihi na ufanisi wa huduma.
Kimsingi safari ya ndege haianzi angani, bali huanza ardhini. Kaaya anasema kila rubani hupitia 'Briefing Office' kabla ya safari kupata taarifa muhimu.
Taarifa hizo zinajumuisha hali ya hewa, usalama, na taarifa za njia za anga. Kaaya anasema TCAA kwa sasa inahudumia viwanja 15 vya ndege nchini, ikiwa ni mtandao mkubwa wa usimamizi wa anga.
MIFUMO TEKNOLOJIA
Usimamizi wa usalama wa anga haujaacha mbali mifumo ya teknolojia, Serikali imekuwa ikiwekeza nguvu kubwa katika kuipatia TCAA vifaa vya kisasa [latest version] sawa na vile vinavyotumika duniani.
Mfumo wa Tanzania unazingatia viwango vya International Civil Aviation Organization kupitia Standards and Recommended Practices [SARPs].
Hatua hiyo imeiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kimataifa ya usalama wa anga. Mhandisi Cleophace aanasema teknolojia ndiyo msingi wa kuhakikisha ndege zinaongozwa kwa usahihi na usalama.
Anasisitiza bila mifumo sahihi ya kiteknolojia haiwezekani kudhibiti safari za anga kwa kiwango ambacho kinahitajika kimataifa.
Anasema miaka ya sasa TCAA imewekeza kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya kisasa ya uongozaji wa ndege ili kupunguza hatari na kuongeza ufanisi.
"Uwekezaji wa vifaa vya kisasa vya teknolojia vya ufuatiliaji usalama wa anga unafanywa kwa kuzingatia vifaa sawa sawa na vile vinavyotumika kwengineko duniani tunaita [latest version].
"Hii yote ni kwa sababu, tunataka anga letu liendelee kuwa salama na tunakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kufuatilia kwa ubora na ufanisi zaidi," anasema.
ANGA LA KISASA
Tanzania imeanza safari ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050, ni wazi hatua zinazoendelea kufanywa na Serikali katika uwekezaji wa vifaa vya kisasa vya kiteknolojia vinaifanya anga ya Tanzania iwe salama zaidi.
"Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza vifaa vya kisasa vya ufuatiliaji na utoaji taarifa za anga," anasema Kaaya.
Uwekezaji mkubwa unaendelea katika mifumo ya kidijitali, miundombinu na mafunzo ya wataalamu.
Kaaya anasisitiza lengo ni kuwa na usafiri wa anga salama zaidi, wa kisasa zaidi na wenye ufanisi wa hali ya juu.
Mhandisi Cleophace anasema kila safari ya ndege salama ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa nyuma ya pazia na wataalamu wa anga.
Ni mchanganyiko wa teknolojia, ujuzi na usimamizi wa kitaalamu unaoifanya Tanzania kuendelea kuwa na anga salama.
Anasisitiza teknolojia itaendelea kuwa msingi mkuu wa usalama wa anga, huku maboresho yakiendelea kufanyika kila siku, kuhakikisha kila safari ya anga inakuwa salama.

Chapisha Maoni