Baada ya takriban miezi 16 ya kusalia nje ya ulingo wa tasnia ya habari kutokana na mfumo rasmi wa ithibati, waandishi wa habari wakongwe nchini sasa wanatarajiwa kurejea kwa kutambuliwa kupitia Ithibati ya Maisha.
Mfumo huo ulianzishwa kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, ambayo pamoja na mambo mengine iliweka masharti ya kitaaluma kwa waandishi wa habari kupata ithibati.
Hata hivyo, baadhi ya waandishi wa habari wakongwe walikosa sifa hizo za kitaaluma na kulazimika kubaki nje ya mfumo rasmi wa ithibati, lakini sasa wanatarajiwa kutambuliwa kufuatia kuzinduliwa kwa Mwongozo wa Kisheria wa Utoaji wa Ithibati ya Maisha.
Mwongozo huo umeandaliwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), ukiweka utaratibu wa kutambua waandishi waliolitumikia taifa kwa muda mrefu.
Wakongwe watakaotambuliwa ni lazima pia wawe wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taaluma ya habari kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Huduma za Habari mwaka 2016.
Kwa mujibu wa JAB, mwongozo huo umeandaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 pamoja na kanuni zake.
Unalenga kutambua waandishi ambao wakati sheria hiyo ilipoanza kutumika walikuwa na umri wa miaka 50 au zaidi na tayari walikuwa wamejijengea historia ya utumishi katika taaluma hiyo.
Akizungumza kupitia hotuba iliyosomwa na Dkt. Egbert Mkoko wakati wa maadhimisho ya JAB Day yaliyofanyika katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mwenyekiti wa JAB, Bw. Tido Mhando, alisema mwongozo huo hautoi msamaha wa masharti ya kitaaluma yaliyowekwa na sheria.
"Bali unatekeleza mamlaka ya Bodi ya kutoa Ithibati ya Maisha kwa waandishi wenye utumishi uliotukuka na mchango wa kipekee katika sekta ya habari," amesema.
Amesema utaratibu huo pia utasaidia kuhifadhi historia ya taaluma ya habari nchini na kuhakikisha uzoefu wa waandishi wakongwe unaendelea kuwa sehemu ya urithi wa sekta hiyo.
"Huku ukitoa heshima kwa kizazi kilichoweka msingi wa maendeleo ya uandishi wa habari nchini," amesema.
Amesisitiza kuwa utoaji wa Ithibati ya Maisha hauondoi wala haupunguzi masharti ya msingi yaliyowekwa na Sheria ya Huduma za Habari kuhusu sifa za kupata ithibati kwa waandishi wa habari.
".., bali ni utekelezaji wa mamlaka ambayo sheria imeipa JAB ya kutambua watu wenye utumishi uliotukuka na mchango wa kipekee katika maendeleo ya sekta ya habari.
Pia ameipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kuiwezesha Bodi kutekeleza majukumu yake
"Ushirikiano huo umechangia kuimarisha mfumo wa ithibati pamoja na kukuza weledi, uwajibikaji na maadili katika taaluma ya uandishi wa habari.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema uzinduzi wa mwongozo huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari,
Unaonesha dhamira ya Bodi ya kuhakikisha mfumo wa ithibati unatambua mchango wa waandishi wa habari wakongwe sambamba na kuendelea kusimamia viwango vya taaluma.
Amesema waandishi hao wamechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa sekta ya habari nchini na wanastahili kutambuliwa kwa uaminifu, uzalendo na weledi waliouonesha katika kipindi chote cha utumishi wao.
Sambamba na uzinduzi wa mwongozo huo, JAB iliendesha mdahalo uliowakutanisha waandishi wa habari, wahariri, wa sekta hiyo kujadili utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari.
Mafanikio yaliyopatikana katika mwaka mmoja wa mfumo wa utoaji wa ithibati pamoja na changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kuendelea kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini.
Uzinduzi wa Mwongozo wa Kisheria wa Utoaji wa Ithibati ya Maisha unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha historia na mchango wa waandishi wa habari wakongwe vinaendelea kutambuliwa.
Vile vile ukijenga daraja kati ya mfumo mpya wa ithibati na kizazi cha waandishi walioasisi na kukuza taaluma hiyo nchini.

Chapisha Maoni