Na Mwandishi Maalum
"Nimejifunza wagonjwa wa Siko Seli tusiwatenge, tuwapende na tuwaheshimu ili wasijione kuwa wao si binadamu, bali ni binadamu waliokamilika,".
Kauli yake Editha Edward mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari Kibamba.
Sasa Editha ametambua, jamii inapaswa kuwaunga mkono ili wasijione wanyonge na kuchangamana nao ili wafikie ndoto na malengo yao ya baadae.
Ni miongoni mwa wanafunzi waliokuwapo shuleni hapa leo Juni 19, 2026 ambapo Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli Tanzania [SCDPCT] imefika kuwapatia elimu kuhusu Siko Seli.
SCDPCT ilifika shuleni hapo kuadhimisha Siku ya Siko Seli Duniani kwa ushirikiano na Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH].
Pamoja na uelimishaji pia wanafunzi wamepata fursa ya kupimwa kinasaba cha Siko Seli kwa hiyari.
Kwa nyakati tofauti wakizungumza na M24 TANZANIA baadhi yao, wamesisitiza wataendelea kuwa mabalozi wazuri ndani ya jamii kwa kufikisha elimu sahihi waliyopatiwa pamoja na vipeperushi.
Elimu waliyopatiwa imewasaidia kuwajengea ufahamu na kujua ukweli halisi dhidi ya imani potofu zinazochangia unyanyapaa kwa wagonjwa wa Siko Seli kwenye jamii.
Asnath Mohamed amesema kabla ya kupata elimu hiyo alikuwa akisikia imani potofu kutoka kwa baadhi ya watu kwamba ugonjwa wa Siko Seli unasababishwa na uchawi na mambo ya giza.
lakini sasa ameelewa kuwa ugonjwa huo hurithiwa kupitia vinasaba kutoka kwa wazazi.
"Mtaani wanasema mtu mwenye Siko Seli amerogwa, lakini sisi tumepata elimu kutoka kwa madaktari. Tumejifunza kuwa ugonjwa huu hurithiwa kupitia vinasaba vya wazazi.
"Hivyo mtu hapaswi kupelekwa kwa waganga bali hospitalini. Tusiwatenge watu wenye Siko Seli, tuwapende kama watu wengine," amesema.
Zacharia Adam amewashukuru madaktari pamoja na mashujaa wa Siko Seli kwa kufika shuleni hapo na kuwapatia elimu pamoja na huduma za upimaji wa Siko Seli.
Akitoa ushuhuda wake, shujaa wa Siko Seli Julius Joseph amesema taarifa nyingine potofu ndani ya jamii, wanadai kwamba mtu mwenye Siko Seli hawezi kuishi zaidi ya miaka 18.
Amesema kauli hiyo na nyinginezo zilizo potofu huwafanya baadhi ya mashujaa wa Siko Seli kukata tamaa ya maisha na kuacha kuzikimbilia ndoto zao.
"Mimi nina zaidi ya miaka 18, nimesoma na sasa ni Afisa Utabibu. Ndoto yangu ni kuwa daktari," amesema.
Ametoa rai kwa wanafunzi kujitokeza kupima kwa hiari ili kufahamu hali zao za vinasaba mapema.
Amesisitiza hatua hiyo itawasaidia kufanya maamuzi sahihi ya maisha na kuchangia kuvunja mnyororo wa kurithisha ugonjwa wa Siko Seli kwa vizazi vijavyo.
Afisa Habari wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Ugonjwa wa Siko Seli Tanzania, Veronica Mrema, amewasihi wanafunzi hao kufikisha elimu sahihi waliyoipata kwa familia na jamii.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuendelea kuondosha imani potofu na kupunguza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na ugonjwa huu.
"Tumekuja hapa mmesikia ukweli halisi kutoka kwa madaktari bingwa kabisa wa Muhimbili. Tumekuja pia na shujaa wetu, mmemuona na amewaeleza uzoefu wake.
"Basi mkirudi majumbani tuwe mabalozi wazuri wa elimu kuhusu Siko Seli.
"Tunahitaji kwa pamoja tuuvunje mduara wa Siko Seli na tuvunje unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na ugonjwa huu," amesema Veronica.
Akizungumza Mtaalamu wa Sayansi za Maabara wa MNH–Mloganzila, Wilson Hape, amesema ni muhimu wananchi kupima mapema kabla ya kuamua kuanzisha familia.
"Kwa sababu ukiwa na kinasaba na ukaoana na mtu mwenye kinasaba ndiyo mnakuwa na uwezekano mkubwa wa kutengeneza mtoto mwenye ugonjwa wa Siko Seli,".
Amesema ugonjwa huo huambatana na changamoto nyingi ikiwamo kupungukiwa damu mara kwa mara na hivyo kuhitaji kuongezwa hospitalini.
Amehimiza pia jamii kuendelea kujitokeza kuchangia damu ili pale inapohitajika iweze kutumika kuokoa maisha ya wengine ikiwamo wagonjwa wa Siko Seli.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Tuchukue Hatua kwa Usawa: Kuongeza Nafasi ya Kuishi kwa Wagonjwa wa Siko Seli."
Jumla ya wanafunzi 36 walijitokeza kufanyiwa uchunguzi wa awamu, ambapo sita kati yao walikutwa ni wabebaji wa kinasaba [AS], hakukuwa na aliyekutwa na ugonjwa [SS], na 30 walikutwa na vinasaba vya kawaida [AA].
Uongozi wa Shule ya Sekondari Kibamba umeishukuru SCDPCT na MNH kwa kufikisha elimu kwa wananfunzi wao pamoja na uchunguzi wa hali zao za vinasaba.




Chapisha Maoni