moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Miaka kadhaa iliyopita ilikuwa nadra mno kusikia mtu mashuhuri akisimulia hadharani changamoto ya kiafya iliyowahi kuikumba yeye binafsi au familia yake.

Mara nyingi masuala ya afya, hasa magonjwa ya kurithi, yalibaki nyuma ya milango iliyofungwa na kufunikwa na ukimya mkubwa.

Suala la kuonekana dhaifu mbele ya jamii walihofia. Umaarufu mara nyingi ulihusishwa na picha ya ukamilifu na mafanikio, hivyo kuzungumzia ugonjwa kulionekana kama kufichua udhaifu.

Sababu nyingine ilikuwa ni unyanyapaa uliokuwepo dhidi ya magonjwa ya kurithi. Katika baadhi ya jamii, Siko Seli ilihusishwa na imani potofu kama laana, mikosi au adhabu ya kiroho.

Hali hiyo ilisababisha familia nyingi ziliamua kubeba maumivu yao kimya kimya. Matokeo yake ni kwamba ugonjwa uliendelea kuzungukwa na taarifa zisizo sahihi.

Idadi kubwa ya watu walikosa elimu sahihi / muhimu kuhusu namna unavyorithiwa, jinsi ya kuudhibiti na hatua zinazoweza kuchukuliwa kuzuia madhara yake.

Mathalan, ndani ya jamii nyingi za Afrika, familia zilizoathiriwa na magonjwa ya kurithi kama Siko Seli zilijikuta zikibeba mzigo mkubwa wa kimwili, kihisia na kifedha.

Familia zikipambana pia na dhana potofu kutoka kwa jamii inayowazunguka. Wengi walichagua kukaa kimya badala ya kuzungumza wazi kuhusu hali zao.

Lakini miaka ya sasa, simulizi hiyo inazidi kubadilika miongoni mwa jamii. Nchini Tanzania kuna watu mashuhuri wanaokabiliana na magonjwa sugu wamekuwa wakieleza hadharani hali zao.

Hii inatoa taswira mpya katika mapambano dhidi ya magonjwa haya yanayoathiri mamilioni ya watu duniani, kwa muktadha wa makala haya tutaangazia zaidi kumuhusu Nasseeb Abdul.

Diamond Platnumz ndilo hasa jina maarufu kwa walio wengi, akijizolea mamilioni ya mashabiki wa muziki wake duniani, hasa kundi la vijana wanaovutiwa na miondoko yake na midundo.

Usiku wa Juni 22, 2026 alifunguka namna ugonjwa wa Siko Seli ulivyoathiri familia yake, mtu wake wa karibu.

"Mwaka 2010 nilipoteza mtoto wa dada yangu, alikuwa anaitwa Othman.., tulimpoteza kwa sababu ya Siko Seli, nilivyofika na kuona Tanzania Serikali yetu imewekeza kwenye afya.

"Kwa namna inayomuokoa Mtanzania nilistaajabu sana, nilitamani mtoto wa dada yangu pengine angekuwepo sasa hivi naye angepata nusra, angeishi,".  "

Diamond maarufu pia kwa jina la Simba Dangote anakuwa msanii mkubwa wa kwanza, katika Ukanda wa Afrika Mashariki, mwenye idadi kubwa ya wafuasi kwenye mitandao ya kijamii, kufunguka, huku akiweka wazi ametenga TZS Mil. 100 kwa ajili ya kuchangia matibabu ya Uloto kwa watoto wenye Siko Seli.

Haikuwa kauli ya simulizi ya majonzi tu kwa familia yake, bali kauli inayobeba ujumbe mzito wenye dhamana ya kuvunja ukimya ambao kwa miaka mingi umeisonga jamii kuhusu Siko Seli.

Ni wazi kauli yake inafungua ukurasa mpya wa mjadala hasa kuhusu umuhimu wa elimu, uchunguzi wa vinasaba, matibabu na nafasi ya jamii katika kupambana na ugonjwa huo na watu mashuhuri wengine wameanza kuweka fedha kuunga mkono mpango wake.

Siku kadhaa zilizopita Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Taasisi ya WASAFI alitembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Ukanda wa Kati mwa Tanzania, yalipo pia Makao Makuu ya Nchi.

Safari ambayo ilimpa uelewa mpana kuhusu huduma za uchunguzi na tiba zinazotolewa na wataalamu ndani ya hospitali hiyo inayomilikiwa na Umma.

BMH ndiyo hospitali pekee nchini Tanzania inayotoa matibabu dhidi ya Siko Seli kwa upandikizaji Uloto, tiba ya ubingwa bobezi iliyoanzishwa na Serikali mnamo 2023.

Takwimu za BMH zinaeleza mpaka kufikia sasa jumla ya wagonjwa [watoto] 30 wametibiwa na kupona Siko Seli.

Diamond Platnumz ameguswa kupitia taasisi anayoisimamia amefanya maamuzi ya kushirikiana na BMH kufanya uhamasishaji ili kupata fedha zitakazokwenda kutumika kugharamia wasio na uwezo.

Tiba ya Uloto kwa kila mgonjwa mmoja kufanyiwa nchini Tanzania inahitaji wastani wa TZS Mil. 75 kiasi ambacho ni kingi na wengi hawajaweza kumudu, kwa waliofanyiwa wamelipiwa na Serikali.

Hafla aliyoifanya usiku huo ilikusanya makumi ya wasanii maarufu wakiwamo waigizaji, wachekeshaji, wana muziki, wana mitindo pamoja na viongozi wa juu wa Serikali na wataalamu wa afya.

MZIGO WA SIKO SELI - TANZANIA

Siko Seli ni miongoni mwa magonjwa ya kurithi yanayoathiri watu wengi zaidi duniani. Tanzania ni kati ya nchi tano zenye mzigo mkubwa zaidi wa ugonjwa huo duniani.

Idadi ya watoto wanaozaliwa na Siko Seli imeongezeka kutoka 8,000 - 11,000 kila mwaka  ilivyokuwa miaka zaidi ya 10 iliyopita, nchini Tanzania.

Sasa imefikia watoto 11,000 - 14,000. Kiwango hiki kinaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa idadi ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo barani Afrika na duniani.

Wataalamu wa afya wanakadiria kuwa kati ya asilimia 15 hadi 23 ya Watanzania wamebeba kinasaba cha ugonjwa [sickle cell trait], lakini wengi wao bado hawafahamu hali zao za kinasaba.

Kutofahamu hali hiyo kunamaanisha kuwa watu wengi huingia kwenye ndoa au kupata watoto bila kuelewa uwezekano wa kurithisha ugonjwa huo kwa kizazi kijacho.

Kwa wataalamu wa afya ya umma, hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika uchunguzi wa vinasaba, elimu kwa jamii na ushauri wa kijenetiki.

Hatua ambayo itasaidia watu wanaotaka kuanzisha familia kufanya maamuzi sahihi kwa sababu tayari wanakuwa na uelewa sahihi na wanajijua hali zao.


NGUVU YA USHAWISHI

Watafiti wa mawasiliano ya afya wamekuwa wakichunguza kwa miaka mingi athari za watu mashuhuri wanapozungumzia masuala ya afya.

Tafiti zilizochapishwa katika majarida ya kimataifa ya mawasiliano ya afya zinaonesha, mtu mashuhuri anapozungumzia ugonjwa fulani hadharani, kiwango cha umakini wa umma huongezeka kwa kasi.

Watu wengi huanza kutafuta taarifa zaidi na baadhi hujitokeza kupata huduma za afya walizokuwa wakiziahirisha.

Katika taaluma ya mawasiliano, hali hii hufahamika kama 'celebrity health disclosure effect'.

Nadharia ya 'Social Learning Theory' ya mwanasaikolojia Albert Bandura inaeleza "Watu hujifunza kwa kuangalia na kuiga tabia za wale wanaowaheshimu au kuwafuata".

Kwa mantiki hiyo, mtu mashuhuri anapozungumzia Siko Seli, anakuwa zaidi ya balozi wa kampeni; anakuwa kichocheo cha mabadiliko ya kijamii.

Ndiyo maana ushuhuda wa Diamond kuhusu kumpoteza mpwa wake unaweza kuwa na athari kubwa zaidi kuliko mabango mengi ya uhamasishaji yanayotolewa kwa wakati mmoja.

UPANDIKIZAJI ULOTO

Moja ya hoja kubwa zilizojitokeza katika kampeni hiyo ni umuhimu wa upandikizaji wa uloto (bone marrow transplant).

Kwa miaka mingi, huduma za Siko Seli zimejikita zaidi katika kupunguza maumivu, kuzuia madhara na kuboresha ubora wa maisha ya wagonjwa.

Hata hivyo, maendeleo ya sayansi yameonesha kuwa kwa baadhi ya wagonjwa, upandikizaji wa uloto unaweza kutoa nafasi ya matokeo makubwa zaidi ya kiafya.

Changamoto iliyopo ni kwamba huduma hiyo inahitaji utaalamu wa hali ya juu, vifaa maalum na gharama kubwa.

Hivyo, mafanikio yake yanahitaji ushirikiano wa hospitali, serikali, sekta binafsi, wafadhili na jamii kwa ujumla.

Katika mazingira hayo, kampeni za kuchangisha fedha na kuongeza uelewa wa jamii zinaweza kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata nafasi ya kufaidika na tiba hii.

NGUVU YA 'MEDIA'

Ikiwa watu mashuhuri wana nguvu ya kuvutia umma, vyombo vya habari vina nguvu ya kuendeleza mjadala huo na kuugeuza kuwa mabadiliko ya kijamii.

Ushahidi wa kisayansi unaonesha, kampeni za mawasiliano ya afya kupitia vyombo vya habari zina uwezo mkubwa wa kubadili maarifa, mitazamo na hata tabia za kiafya za jamii.

Tathmini moja ya kimfumo iliyochambua tafiti 22 za kampeni za afya ilibaini, kampeni zilizotumia vyombo vya habari na mikakati mingine ya kijamii ziliongeza mtindo bora kwa wastani wa 8.4%.

utafiti mwingine nchini Australia, kampeni ya afya iliyotumia televisheni, magazeti na njia nyingine za mawasiliano iliongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za afya kutoka 2.5% hadi 23.7%.

Aidha, idadi ya watu waliojitokeza kupata huduma ikiongezeka mara nne wakati kampeni ilipokuwa ikiendelea.

Tafiti zilizochapishwa katika jarida la The Lancet zimeonesha, kampeni za vyombo vya habari zina uwezo wa kubadilisha mtindo bora wa maisha unaoimarisha afya katika ngazi ya jamii.

Ni pamoja na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchunguzi wa magonjwa, uchangiaji damu, kinga dhidi ya saratani na matumizi ya huduma za afya.

Kwa Tanzania, vyombo vya habari vimekuwa nyenzo muhimu katika kampeni mbalimbali za afya ya umma ikiwemo chanjo, malaria, VVU na afya ya uzazi.

Katika muktadha wa Siko Seli, media zina nafasi ya kipekee ya kuongeza uelewa kuhusu uchunguzi wa vinasaba, kuhamasisha uchangiaji damu.

Kupunguza unyanyapaa na kuwasaidia wananchi kuelewa kuwa ugonjwa huo si laana bali ni hali ya kurithi inayoweza kudhibitiwa kwa huduma sahihi za afya.

Ni suala ambalo limekuwa likifanywa na vyombo vya habari vingi nchini ikiwamo vile vya Kitaifa lakini kwa muktadha wa WASAFI sasa imechukua taswira pana zaidi katika mapambano dhidi ya Siko Seli, ikizingatiwa kina wafuatiliaji wengi vijana.


ZAIDI YA HISANI

Wapo wanaoweza kuiona kampeni ya Wasafi kama shughuli ya kawaida ya kuchangisha fedha. Lakini kwa mtazamo wa afya ya umma, kampeni hiyo ina maana kubwa zaidi.

WASAFI imeonesha, media zinaweza kuwa sehemu ya suluhisho, si watazamaji wa changamoto za kijamii pekee.

Chombo hicho cha habari chenye mamilioni ya wafuatiliaji kimeonesha, watu mashuhuri wanaweza kutumia ushawishi wao kuhamasisha afya ya umma.

Aidha, kimeonesha hospitali, sekta binafsi, wanahabari na jamii wanaweza kushirikiana katika kuokoa maisha.

Kwa upande mwingine, kampeni hiyo imeibua mjadala muhimu kuhusu mustakabali wa huduma za Siko Seli nchini Tanzania.

Pamoja na namna ya kuhakikisha teknolojia za kisasa za matibabu zinawafikia watoto wengi zaidi wanaozihitaji.

Ni wazi kwamba mapambano dhidi ya Siko Seli yanahitaji nguvu na juhudi za kila mmoja kuuvunja mduara na si suala la kuachia wataalamu mabingwa wa tiba pekee.

Bali kwa upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wengi zaidi kufikiwa, kuibua mijadala chanya kunapanua wigo zaidi wa mapambano dhidi ya Siko Seli.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement