moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Mfumo wa ithibati kwa waandishi wa habari umeanza kuleta mabadiliko katika tasnia ya habari kwa kuimarisha weledi, uwajibikaji na kurejesha heshima ya taaluma hiyo nchini.

Kwa matokeo chanya hayo, waandishi wa habari ambao bado hawajakidhi vigezo vya kitaaluma ili kupata ithibati wamehimizwa kuendelea kujiendeleza kielimu ili kukidhi viwango vinavyotakiwa.

Hayo yameelezwa na wadau wa sekta ya habari wakati wa mdahalo uliofanyika JAB Day, ndani ya viwanja vya Sabasaba katika kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Sheria ya Huduma za Habari ilipitishwa mwishoni mwa mwaka 2015 na kuanza kutumika mwaka 2016, pamoja na kanuni zake za mwaka 2017.

Hatua iliyoweka msingi wa kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa ithibati kwa waandishi wa habari.

"Iliweka msingi wa kutambua nani ni mwandishi wa habari na sifa anazopaswa kuwa nazo," amesema Deodatus Balile alipokuwa akizungumza kwenye mdahalo huo.

Balile ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema sheria hiyo ndiyo iliyopelekea kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari [JAB].

JAB imepewa majukumu ikiwamo kusimamia mfumo wa ithibati kwa waandishi wanaokidhi vigezo.

"Tangu hapo, maji na mafuta yakaanza kujitenga," amesema Balile.

Amesisitiza "Mfumo huo umeanza kuweka tofauti kati ya mwandishi anayetekeleza majukumu yake kwa misingi ya taaluma na mtu anayejihusisha na utoaji wa taarifa bila maandalizi ya kitaaluma.

Akitoa mfano wa taaluma nyingine, Balile amesema si kila mtu anaweza kurusha ndege kwa sababu tu ana kipaji cha kufanya hivyo, wala si kila mtu anaweza kutoa huduma za kitabibu bila kusomea taaluma husika.

Amesema uandishi wa habari nao unapaswa kupewa hadhi hiyo hiyo kwa kuhakikisha wanaofanya kazi hiyo wanakuwa na elimu na ujuzi unaohitajika.

"Anayetaka kufanya kazi ya uandishi wa habari aende akasome," amesisitiza.

Elimu, uwajibikaji na uimara wa vyombo vya habari

Mhariri Mtendaji Mkuu wa Nipashe, Salome Kitomary, amesema kuanzishwa kwa JAB kumesaidia kupunguza hali ya uholela katika sekta ya habari.

JAB imechangia kuimarika kwa uwajibikaji kuanzia kwa wamiliki wa vyombo vya habari hadi kwa waandishi wenyewe.

"Kuanzia kwa wamiliki wa vyombo vya habari hadi kwa waandishi wenyewe katika utendaji kazi wa kila siku," amesema.

Amesema elimu ina nafasi kubwa katika kumjengea mwandishi uwezo wa kufanya uchambuzi mpana wa masuala mbalimbali na kutoa habari zenye kina na ubora zaidi.

"Huwezi kulinganisha uwezo wa mtu aliyepitia mafunzo rasmi na yule ambaye hajapata msingi wa kitaaluma," amesema.

Hata hivyo, Salome amesisitiza pamoja na kusimamia viwango vya taaluma, ni muhimu pia kuangalia uchumi wa vyombo vya habari.

"Ili viweze kuwa imara na kuwa na uwezo wa kuajiri wataalamu wenye sifa pamoja na kuwapatia wafanyakazi stahiki zinazolingana na majukumu yao.

Amesema vyombo vya habari vyenye uwezo wa kiuchumi vina nafasi kubwa ya kuwekeza katika mafunzo, kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha wanahabari wanatekeleza majukumu yao kwa uhuru na weledi.

"Ni muhimu kuimarisha mazingira ya uendeshaji wa vyombo vya habari ili viweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi," amesema.

Mhariri kutoka MCL, Lilian Timbuka, amesema mfumo wa ithibati umechangia kurejesha heshima ya taaluma ya habari kwa kuwa kila mmoja sasa anatambua wajibu wake ndani ya vyumba vya habari.

Amesema baadhi ya waandishi ambao hawakuwa wamekidhi vigezo wameamua kurejea katika vyuo ili kujiendeleza na kupata sifa zinazohitajika.

MUSTAKABALI WA TASNIA

Pamoja na hatua za kuimarisha viwango vya taaluma, Mhariri wa Media Brains, Jesse Kwayu, amesema mchango wa waandishi wakongwe haupaswi kusahaulika.

Amesema kundi hilo lilichangia kwa kiasi kikubwa kujenga misingi ya taaluma ya habari nchini na kuwalea waandishi wengi ambao leo wanaendelea kuitumikia sekta hiyo.

Amesema uzoefu wa waandishi hao ni rasilimali muhimu inayopaswa kutumika katika kuimarisha kizazi kipya cha wanahabari.

Mbali na hilo, Kwayu amesema ni muhimu kuangalia mazingira ambayo waandishi wa habari wanafanyia kazi, hususan katika uandishi wa habari za uchunguzi.

Amesema majukwaa ya kidijitali yamefungua fursa mpya kwa waandishi kufikia maeneo na taarifa ambazo hapo awali zilikuwa na changamoto kubwa kufikiwa.

Amesisitiza kuwa teknolojia inapaswa kutumiwa kuongeza uwajibikaji, ufanisi na tija katika kazi ya uandishi wa habari.

RUDINI CHUO

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam [DAR-PC], Bakari Kimwanga, ametoa rai kwa waandishi wa habari nchini ambao bado hawajakidhi vigezo vya kitaaluma.

Akichangia hoja wakati wa mjadala huo, Kimwanga amesema waandishi wanapaswa kuona elimu kama nyenzo ya kuongeza uwezo wao kitaaluma na si kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema mafunzo ya ngazi ya astashahada na kuendelea yanaweza kuwasaidia waandishi kuongeza ujuzi, kuimarisha weledi na kufikia sifa zinazohitajika katika mfumo wa sasa wa ithibati.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Elius Msuya ambaye amesisitiza kuwa kila mtu anayetamani kuwa mwandishi wa habari nchini Tanzania anapaswa kusomea taaluma hiyo.

"Inawezekana, mimi nilipoingia kwenye chumba cha habari nilikuwa na cheti pekee, nikajiendeleza nikiwa kazini mpaka ngazi ya shahada na wengine wakanifuata nyuma," amesema.

JAB kuendelea kusimamia viwango

Sambamba na mdahalo huo, ulizinduliwa Mwongozo wa Kisheria wa Utoaji wa Ithibati ya Maisha kwa Waandishi wa Habari Wakongwe ulioandaliwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).

Uzinduzi wa mwongozo huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari na unaonesha dhamira ya JAB ya kuendelea kusimamia viwango vya taaluma ya habari.

Kupitia mwongozo huo, JAB inatambua na kuthamini mchango wa waandishi wa habari wakongwe waliolitumikia Taifa kwa uaminifu, uzalendo na weledi.

Mwenyekiti wa Bodi ya JAB, Bw. Tido Mhando amesema mwongozo huo umeandaliwa kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa Bodi chini ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 pamoja na kanuni zake.

Amesema lengo la mwongozo huo ni kuweka utaratibu wa kuwatambua waandishi wa habari wakongwe waliotoa mchango wa kipekee katika maendeleo ya taaluma hiyo.

Amesema mwongozo huo unalenga kuhakikisha historia na uzoefu wa waandishi hao vinaendelea kuwa sehemu ya urithi wa sekta ya habari nchini.

Amesema unawahusu waandishi ambao wakati Sheria ya Huduma za Habari ilipoanza kutumika mwaka 2016 walikuwa na umri wa miaka 50 au zaidi.

Wakongwe hao ni wale ambao tayari walikuwa wamejijengea historia ya utumishi katika taaluma ya habari, lakini hawakupata fursa ya kufikia baadhi ya sifa za kitaaluma zilizowekwa na sheria.

Amesisitiza utoaji wa Ithibati ya Maisha hauondoi wala kupunguza masharti ya msingi yaliyowekwa na Sheria ya Huduma za Habari kuhusu sifa za kupata ithibati kwa waandishi wa habari.

"Bali ni utekelezaji wa mamlaka ambayo sheria imeipa JAB ya kutambua watu wenye utumishi uliotukuka na mchango wa kipekee katika maendeleo ya sekta ya habari," amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema Bodi hiyo haitalegeza msimamo katika kuhakikisha wanaofanya kazi katika tasnia ya habari wanatimiza vigezo vya kitaaluma na kisheria.

Amesema JAB imeanza kufanya ukaguzi mkoa kwa mkoa ili kujiridhisha kuwa waandishi wanaofanya kazi katika sekta hiyo wanakidhi masharti yaliyowekwa.

"Sasa hivi tumeanza kufanya ukaguzi mkoa kwa mkoa. Tumeshafika Dodoma, Iringa na Morogoro kuhakikisha wale waliopo na wanaofanya kazi wamekidhi vigezo vya kitaaluma na kisheria," amesema.

Amesema utoaji wa ithibati unategemea uhakiki wa sifa na vigezo vya mwombaji, licha ya ongezeko la taarifa zinazozalishwa kupitia mitandao ya kijamii.

Amesema mtu ambaye hana sifa zinazotakiwa hawezi kurejea katika shughuli za uandishi wa habari au utangazaji hadi atakapokidhi masharti hayo.

Mfumo wa ithibati unaendelea kujenga mazingira ambayo yatahakikisha sekta ya habari inakuwa na wataalamu wenye sifa, huku historia na mchango wa wale walioitangulia ukiendelea kuhifadhiwa.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement