Na Veronica Mrema
Uzuri wa barabara una zaidi ya maana ya kupunguzaa mashimo au kufanya safari iwe fupi zaidi kwa Mkazi wa Dar es Salaam.
Barabara ni kiungo muhimu mno cha kumrahisishia maisha na shughuli zake za kila siku.
Mfanyabiashara anahitaji kufungua duka lake hata nyakati za usiku bila hofu ya giza, mgonjwa anayehitaji huduma ya haraka anafikishwa hospitalini kwa wakati.
Mwanafunzi anayekwneda shule anafika kwa wakati na dereva naye anapata ahueni ya kupunguza gharama za matengenezo ya gari lake.
Ukipita barabara kadhaa ndani ya Dar es Salaam, utashuhudia barabara zimechimbuliwa, mitambo ya ujenzi ipo na wakandarasi wanachakarika kuhakikisha wanakamilisha kazi za miradi husika.
Unachokiona si heka-heka hizo tu kwa barabara husika. Unachokiona ni sehemu ya safari ya kuijenga Dar es Salaam inayokusudiwa kuwa jiji lenye miundombinu bora na uchumi unaokua kwa kasi zaidi.
Mkoa huu una mtandao wa barabara wenye urefu wa km. 5,057.7 kati yake 12% ni za kiwango cha lami, 33% changarawe na 54% udongo.
Takwimu hii ni kwa mujibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini [TARURA] Mkoa wa Dar es Salaam.
Sasa, ili kubadili hali hiyo, TARURA inaendelea na matengenezo ya barabara katika wilaya zote za mkoa huu pamoja na ujenzi wa takribani km. 100.91 za barabara za lami.
"Ujenzi wa kilomita hizo za lami unafanyaka kupitia Mradi wa DMDP II [Dar es Salaam Metropolitan Development Project Awamu ya Pili], unaofadhiliwa na Benki ya Dunia [WB],".
Yameelezwa hayo na Mhandisi Nyamagaula Ndango akimwakilisha Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, katika mahojiano maalum na M24 TANZANIA, viwanda vya SABASABA.
Miradi hiyo inatekelezwa katika Halmashauri za Kinondoni, Temeke, Kigamboni na Jiji la Dar es Salaam.
Mradi huo unajumuisha pia ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua pamoja na uwekaji wa taa za barabarani.
Maboresho hayo yanalenga si tu kurahisisha usafiri, bali pia kuongeza muda wa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi kwa kuweka mazingira salama ya kufanya kazi hata wakati wa usiku.
Akizungumzia mwelekeo wa muda mrefu wa maendeleo ya jiji, mhandisi Ndango amesema maboresho hayo yanaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Serikali inalenga kuongeza kwa kiwango kikubwa mtandao wa barabara za lami na kupunguza barabara za changarawe na udongo.
"Lengo ni kuhakikisha wananchi wanafanya biashara kwa urahisi zaidi, wanasafiri kutoka eneo moja kwenda jingine bila changamoto za miundombinu.
"Jiji nalo linaendelea kukua sambamba na mahitaji ya wananchi," amesema Mhandisi Ndango.
Ameongeza "Sambamba na hilo, katika kukabiliana na changamoto za mafuriko, Serikali pia inaendelea na ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 390 katika eneo la Jangwani.
"Pia, ujenzi wa kingo za kisasa katika Bonde la Mto Msimbazi ili kupunguza athari za mafuriko ambazo zimekuwa zikiathiri usafiri na shughuli za kiuchumi kwa miaka mingi.
Kulingana na Mhandisi Ndango, kwa TARURA, uwekezaji unaoendelea leo hauhusu kujenga barabara pekee.
Unahusu kujenga mazingira ambayo yatamwezesha mwananchi kusafiri kwa urahisi, kufanya biashara kwa tija na kuona maendeleo yakigusa maisha yake ya kila siku.
Kwa TARURA tayari wameianza safari ya kuhakikisha Dar es Salaam inasonga mbele zaidi kuelekea malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Chapisha Maoni