moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Ukaguzi mahususi upo mkoa kwa mkoa ndani ya vyumba vya habari nchini, kuhakikisha kila aliyepo na anayefanya kazi ya habari amekidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria.

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari [JAB] yenye jukumu la kusimamia tasnia hiyo imesisitiza haitalegeza 'kamba'.

Waandishi wa habari ambao bado hawajakidhi vigezo vya kitaaluma vya kupata ithibati, waende vyuoni ili kuongeza ujuzi na kufikia viwango vinavyotakiwa kwa mfumo wa sasa.

Rai hiyo imetolewa na wadau wa sekta ya habari wakati wa mdahalo wa JAB Day uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba, ndani ya eneo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam [DAR-PC], Bakari Kimwanga, amesema

"Waandishi wanapaswa kuona elimu kama nyenzo ya kuongeza uwezo wao kitaaluma na si kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao," Kimwanga alikuwa akichangia hoja wakati wa mjadala huo.

Amesema mafunzo ya ngazi ya astashahada na kuendelea yanaweza kuwasaidia waandishi kuongeza ujuzi, kuimarisha weledi na kufikia sifa zinazohitajika katika mfumo wa ithibati.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Elius Msuya ambaye amesema waandishi wanaweza kuendelea na masomo wakiwa kazini ili kuboresha uwezo wao kitaaluma.

Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesisitiza wanaendelea kufanya ukaguzi mkoa kwa mkoa kuhakikisha wanaofanya kazi ni wale waliotimiza masharti ya kitaaluma na kisheria.

Amesema tayari ukaguzi huo umefanyika Mkoa wa Dodoma, Iringa na Morogoro, wakijiridhisha kuwa waandishi waliopo wana sifa zinazotakiwa.

“Sasa hivi tumeanza kufanya ukaguzi mkoa kwa mkoa kuhakikisha wale waliopo na wanaofanya kazi wamekidhi vigezo vya kitaaluma na kisheria,” amesema.

Kipangula amesema utoaji wa ithibati unategemea uhakiki wa sifa na vigezo vya mwombaji, na kwamba JAB imeendelea kushughulikia masuala yanayohusu utekelezaji wa mfumo huo.

Amesema hadi sasa Bodi hiyo imeshughulikia jumla ya mashauri 19 yanayohusiana na masuala mbalimbali ya ithibati.

Amesisitiza, mtu ambaye hana sifa zinazotakiwa hawezi kurejea katika shughuli za uandishi wa habari au utangazaji hadi atakapokidhi masharti yaliyowekwa.

Mfumo wa ithibati unaendelea kujenga mazingira yanayolenga kuhakikisha sekta ya habari inakuwa na wataalamu wenye sifa.

Pamoja na hayo, waandishi wa habari wameendelea kuhimizwa kujifunza na kutumia vema teknolojia za kisasa ili kuboresha taaluma hiyo.

PICHA: Imani Nathaniel.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement