Na Veronica Mrema
Unapopita kwenye barabara mpya yenye lami au unapovuka daraja lililojengwa kwa viwango vya kisasa, mara nyingi kinachoonekana ni matokeo ya mwisho safari rahisi na usafiri salama.
Ahueni kubwa huonekana kwamba hakuna shughuli ya kiuchumi au kijamii inayosimama, zinafanyika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.
Lakini nyuma ya kila barabara na daraja imara kuna mchakato mkubwa wa kitaalamu unaohusisha tafiti, vipimo na uhakiki wa ubora kabla na wakati wa utekelezaji wa mradi.
Sehemu muhimu ya mchakato huo ni maabara za Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini [TARURA].
Maabara za TARURA zimekuwa nguzo katika kuhakikisha miradi ya miundombinu nchini inajengwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, kuwa salama na kudumu kwa muda mrefu.
Ndani ya maabara, wataalamu wa TARURA hufanya uchunguzi na uhakiki wa vifaa vya ujenzi pamoja na kazi zinazotekelezwa kwenye miradi mbalimbali ya barabara, madaraja na miundombinu mingine.
Fundi Sanifu kutoka Kitengo cha Utafiti na Udhibiti Ubora TARURA Makao Makuu, Jacob Manguye ameeleza mengi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam [Sabasaba].
Miongoni mwa jukumu muhimu la maabara hizo ni kuhakikisha miradi yote inakidhi viwango vya kitaalamu na masharti ya mikataba.
Wataalamu wa maabara hufanya vipimo vya kina vya vifaa vya ujenzi kabla havijatumika kwenye miradi.
Pia hufanya uhakiki wa ubora wa kazi zinazofanywa na wakandarasi ili kuhakikisha zinaendana na viwango vilivyowekwa.
"Tunafanya uhakiki wa kazi mbalimbali ikiwemo za vifusi, lami, madaraja na miundombinu mingine.
"Lengo ni kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na ubora wa hali ya juu na inadumu kwa muda mrefu," amesema Manguye.
Amesema kwa sasa TARURA ina maabara kuu iliyopo Makao Makuu Dodoma pamoja na maabara nyingine 14 zilizosambazwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Kigoma, Arusha na Moshi.
Maabara hizo zinatoa huduma za upimaji wa vifaa vya ujenzi na uhakiki wa ubora wa miradi kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Sambamba na hilo, maabara hizo zina jukumu la kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
GEOTECH
Pamoja na huduma za maabara, TARURA pia inamiliki mtambo maalumu wa uchunguzi wa udongo (Geotech).
Mtambo huo unawawezesha wataalamu kufanya tafiti za kina kuhusu uwezo wa udongo kuhimili ujenzi wa madaraja, majengo na miundombinu mingine mikubwa kabla ya kuanza kwa ujenzi.
Uchunguzi huo husaidia kupata taarifa muhimu kuhusu hali ya udongo na kupunguza hatari zinazoweza kuathiri uimara wa miundombinu, sambamba na kuongeza usalama kwa watumiaji.
Kwa mtazamo wa TARURA, ubora wa miundombinu hauanzii kwenye hatua ya mwisho ya ujenzi pekee, bali huanzia kwenye tafiti, vipimo na maamuzi sahihi ya kitaalamu yanayofanyika kabla kazi haijaanza.
Manguye ametoa wito kwa wakandarasi, wahandisi, taasisi za ujenzi na wadau wengine wa sekta hiyo kutumia huduma za maabara za TARURA.
"Ili kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inafikia viwango vinavyotakiwa na kutoa huduma bora kwa wananchi," amesisitiza.
Hatua zote hizi zinalenga kuhakikisha kila kilomita ya barabara na kila daraja linalojengwa kuna mchakato wa kisayansi.
Mchakato ambao unalenga kuhakikisha wananchi wanapatiwa miundombinu salama, yenye ubora na yenye thamani kwa wananchi wanaoitumia.

Chapisha Maoni