moja

Responsive Advertisement

Na Mwandishi Maalum

Licha ya juhudi zinazoendelea kuimarisha sekta ya afya nchini, bado sehemu kubwa ya Watanzania haina uelewa wa kutosha kuhusu huduma sahihi za famasi na matumizi salama ya dawa.

Nchini Tanzania jamii pia bado haina uelewa wa kutosha kuhusu majukumu ya Baraza la Famasi, ikiwamo kundi la waandishi wa habari na wahariri, hali iliyolazimu uongozi kuchukua hatua maalum.

Baraza la Famasi, limefanya semina ya siku moja kwa waandishi wa habari na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Dar es Salaam, na kueleza kwa kina nafasi yake katika kulinda afya ya jamii.

Akifungua semina hiyo Msajili wa Baraza la Famasi Mfamasia Boniface Magige amesema waliona vema kuiandaa kwa sababu bado kuna pengo la uelewa miongoni mwa wananchi na hata baadhi ya wanahabari.

Amesisitiza kutokana na hali hiyo liliona vema kuwajengea uwezo waandishi wa habari, waweze kuandika na kuripoti kwa usahihi masuala ya huduma za famasi, matumizi sahihi ya dawa na Sheria zinazosimamia sekta hii.

Amesema wanaamini waandishi wa habari ni kiungo muhimu kati ya taasisi za umma na wananchi. 

Aidha, kupitia taarifa sahihi zinazotolewa na vyombo vya habari, jamii inaweza kupata elimu inayohitajika kuhusu matumizi salama ya dawa na huduma za famasi.

Kwa mujibu wa Baraza, taasisi hiyo ni chombo cha Serikali kilicho chini ya Wizara ya Afya, kilichoanzishwa mwaka 2011 kwa mujibu wa Sheria ya Famasi, Sura ya 219.

Baraza la Famasi lina majukumu mbalimbali ikiwamo la kusimamia taaluma ya famasi na kuhakikisha huduma za famasi zinatolewa kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na viwango vya taaluma.

Hata hivyo, Baraza limesema bado wananchi wengi hawafahamu wajibu wake katika kulinda afya ya umma kupitia usimamizi wa wataalamu wa famasi, maduka ya dawa, huduma za famasi na matumizi sahihi ya dawa.

Limesema ukosefu wa uelewa huo unaweza kuchangia kuenea kwa taarifa potofu kuhusu dawa pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.

Baraza limeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari ili kuhakikisha taarifa zinazohusu sekta ya famasi zinafikishwa kwa wananchi kwa usahihi, kwa wakati na kupitia vyanzo vinavyoaminika.

Baraza la Famasi limewahimiza waandishi wa habari kuendelea kuzingatia weledi na maadili ya taaluma kwa kuthibitisha taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzirusha.

Msajili wa Baraza, Mfamasia Magige amesema hatua hiyo itasaidia kujenga jamii yenye uelewa sahihi kuhusu huduma za afya na matumizi ya dawa hatimaye kuokoa afya ya jamii.

Kwa nyakati tofauti, washiriki wa kikao hicho, wamepongeza Baraza kwa kuandaa semina hiyo, kwani wameweza kupata maarifa yatayowasaidia katika uandaaji wa maudhui bora ya kuelimisha jamii.

"Ni hatua muhimu, kujenga mahusiano na waandishi wa habari, wahariri na Baraza kwa sababu kwa pamoja tutakuwa na lugha moja, kusaidia jamii yetu, kwa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa upana,".

Naibu CEO wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam Veronica Mrema amesema hayo wakati akizungumza kwa niaba ya washiriki wote.

"Kundi hili tunawasiliana na wananchi wengi, kupitia vyombo vyetu vya habari, hapa kuna ambao wapo kwenye redio, runinga, magazeti na vyombo vya mtandaoni.

"Ukimpa mwandishi mmoja maarifa sahihi, maana yake anakwenda kuwasilisha kwa kundi kubwa zaidi linalofuatilia chombo anachokitumikia.

"Mmefanya jambo jema, kukutana nasi na tunakwenda kufanya kazi ya kuitumikia jamii, kwa weledi mkubwa na kwa kasi kubwa," amesema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement