Uchunguzi wa kinasaba pamoja na elimu kuhusu Siko Seli imefikishwa kwa wazazi na walezi wenye watoto wanaopatiwa huduma ndani ya Kituo cha Utengamao cha Antonia Verna, Dar es Salaam.
Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli Tanzania [SCDPCT] kwa ushirikiano na Serenox Africa wamefika katika kituo hicho ikiwa ni mwendelezo wa kusherehekea Siku ya Siko Seli Duniani.
Tukio hilo limefanyika Juni 20, 2026 ambapo Antonia Verna Community iliandaa marathon maalum iliyoshirikisha wanajamii pamoja na kuweka fursa ya uchunguzi na elimu ya afya kwa magonjwa mbalimbali.
Afisa Habari wa SCDPCT Veronica Mrema akizungumza na wananchi waliofika kwenye tukio hilo aliwahimiza hasa vijana kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi wa hali zao za vinasaba mapema.
"Ni muhimu kuchunguza kabla ya kuamua kuanzisha familia, tunawapa elimu hii ili muijue Siko Seli."Kwa kupata elimu sahihi, tunaamini mtakuwa mabalozi wazuri wa kuondosha unyanyapaa na dhana potofu nyingi zilizopo ndani ya jamii dhidi ya wenye Siko Seli ba ugonjwa huu kwa ujumla." alisema.
Jumla ya watu 15 walijitokeza kuchunguza vinasaba, ambapo matokeo yalionesha wote walikuwa na vya kawaida [AA].
Kwa nyakati tofauti wazazi na walezi wa watoto hao, wameeleza waandishi wa habari wamefarijika mno kwa kufikishiwa huduma hiyo.
Walisema baada ya kupata elimu hiyo walisema wameondoka na uelewa mpya kuhusu ugonjwa wa Siko Seli na kuahidi kuendelea kuelimisha wengine.
"Elimu hii imenisaidia kuelewa kuwa Siko Seli ni ugonjwa wa kurithi na si imani potofu kama ambavyo baadhi ya watu huamini.
"Leo nimeondoka nikiwa na maarifa ambayo sikuwa nayo. Sasa najua umuhimu wa kupima vinasaba mapema na nitawahamasisha ndugu na marafiki wangu kufanya hivyo," alisema mzazi mmoja.
Mzazi mwingine alisema huduma hiyo imewapa wazazi nafasi ya kuuliza maswali na kupata majibu kutoka kwa wataalamu.
"Tunahitaji elimu kama hii ifike kwenye maeneo mengi zaidi. Wazazi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu Siko Seli."
Elimu iliyotolewa itawasaidia wazazi kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya afya ya watoto wao na familia kwa ujumla na imejenga msingi wa kuendelea kuzuia na kuondoa unyanyapaa kwa jamii.
Wazazi hao waliishukuru SCDPCT na Serenox kwa kuendelea kuwafikia wananchi kupitia matukio ya kijamii, kwani wanazipata kwa urahisi katika maeneo waliko.
SCDPCT imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kufikisha elimu ya Siko Seli katika jamii, ikiamini kuwa uelewa sahihi, uchunguzi wa mapema na ushirikiano wa jamii ni hatua muhimu katika kuvunja mduara wa Siko Seli na kuboresha maisha ya watu wanaoishi na ugonjwa huo.

Chapisha Maoni