moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Umewahi kufikiri, mgonjwa anapokuwa kitandani akihitaji Tiba Damu kwa haraka ili kuokolewa uhai wake? Ila ndani ya hospitali alipo hakuna kundi lake la damu au kuna upungufu mkubwa wa damu?

Hali ambayo huwalazimu madaktari kuanza kuhangaika mawasiliano kati ya hospitali moja na nyingine, au katika benki kuu ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama kuuliza iwapo watapata?

Ni wakati mgumu hasa pale kunapokuwa na idadi kubwa ya wahitaji huku kiwango kilichohifadhiwa benki ya damu hakitoshelezi uhalisia.

Kwa mazingira ya namna hiyo, mara nyingine mgonjwa hushindwa kuhimili kusubiri hadi ipatikane, kuna ambao hupoteza maisha.

“Niliwahi kukutana nalo, kuna mgonjwa alikuwa anahitaji damu aina fulani … nakumbuka ilikuwa B+ kwa wakati huo haikuwapo,”.

 Kwa Adoph Jumanne Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili hii si simulizi ya kusimuliwa, ni hali anayokutana nayo kazini kwake, japokuwa si mara zote.

“Bahati nzuri Wizara ya Afya ina mawasiliano kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa mfano  Muhimbili kuna wakati tunazidiwa tunaenda lugalo.

“Tunaenda mpaka mikoani huko kuna muungano unakuta mgonjwa anahitaji damu na wakati huo tumeishiwa,’ anasema.

Anaongeza “Inabidi tuwasiliane kujua damu itakayoendana na yeye itapatikana wapi?

“Unakuta … mnaweza kuipata ipo mbali lakini mpaka ifike unaambiwa ameshafariki, lakini kama tungekuwa na ‘stock’ kubwa watu wanajitolea kwa hiyari ingekuwa inasaidia tungeokoa wengi zaidi,”.

JE, HALI IPOJE?

Nchini Tanzania bado kuna kundi kubwa la watu wasio na hamasa ya kujitokeza kuchangia damu kwa hiyari.

Hali ambayo inafanya ishindwe kufikia kiwango cha asilimia moja ya idadi ya watu wake ili kutosheleza mahitaji halisi, kama inavyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani [WHO].

Kwa mantiki hiyo ikiwa idadi ya Watanzania ni watu milioni 60 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 hivyo inahitaji wastani wa chupa 600,000 za damu salama kwa mwaka.

Lakini kwa mwaka 2025 pekee imeweza kufikia kiwango cha 71% ya makusanyo, ni wazi bado kuna upungufu.

Makundi yanayohitaji zaidi Tiba Damu ni pamoja na wakina mama hasa wakati wa kujifungua, wagonjwa hasa wa Siko Seli na Saratani mbalimbali, majeruhi wa ajali hasa za barabarani na kundi la watoto.

Licha ya wakina mama kuwa miongoni mwa wahitaji wakubwa wa damu lakini bado ni kundi linalosalia kuwa nyuma kujitokeza kwa hiyari kuchangia damu ikinganishwa na kundi la wanaume, kulikoni?

“Baadhi wanaogopa kwa sababu ya mabadiliko ya ki-mwili, uwoga tu… kwa sababu si unajua sisi kila mwezi tunapata hedhi, hivyo mtu anaogopa anahisi atapungukiwa zaidi,” anaeleza Anitha Magese.

Suala hili halina ukweli wala ushahidi wowote ule wa kisayansi, ni mtizamo tu ambao umejengeka miongoni mwa wanawake.

Kuna wengine ambao pia wana mitazamo kwamba mwanamke anapojitolea damu hujiweka kwenye hatari ya kupata magonjwa mbalimbali, hii huwarudisha nyuma juu ya suala la kuchangia damu.

‘NGUVU YA ZIADA’

“Watu wengi bado wana imani zao tofauti tofauti nadhani tuna kazi kubwa kama watu wa afya kuendelea kuelimisha jamii,”

Kauli yake Daktari Rhobi Jeremiah, anaongeza “.., ukweli ni kwamba jamii yote inatakiwa ijue na ichukue hatua. Suala la uchangiaji damu, kina mama tuna hurum.

“Tuna upendo na mara nyingi tunatamani kuleta mabadiliko ambayo yatagusa jamii moja kwa moja.

“Wengi wanaogopa kwa sababu ya uwoga, [ile] sindano kwamba watazimia, [lakini] wakina baba wanaona tunaweza [‘why not’].

“.., kina dada, kina mama tunaweza kufanya kitu. Ule uwoga ututoke kama wanawake.

“Sisi wataalamu wa afya tuna kazi kubwa kuendelea kuelimisha. Wakina mama wasiogope pale wanapoelimishwa wachukue hatua.

Ni miaka minne mfululizo sasa Anitha amekuwa akijitolea damu na anashuhudia wazi kwamba hajawahi kupata upungufu wala ugonjwa wa aina yoyote ile.

“Nilianza mwaka 2022 baada ya kuhitimu kidato cha nne … mama yangu tu alikuwa anaenda kuchangia akaniambia Anitha twende tukachangie damu, nikamwambia naogopa.

“.., akaniambia usiogope ni kawaida tu. Hiyo ndiyo ilikuwa siku yangu ya kwanza kuchangia damu, ilikuwa kambi za kidini.

Anaongeza “Hiyo siku nikachangia nilikuwa naogopa sema sikujisikia utofauti wowote ule, nilijisikia kawaida.

“Tangu hapo kwa ‘influence’ ya mama yangu,ni mpenzi sana wa kuchangia damu, alikuwa anasema tuchangie damu kwa kuwa watu wengi wana uhitaji wa damu, hivyo nikapata ule moyo wa kujitoa.

“Sikuona utofauti wowote kwenye kutoa damu, niliona kawaida tu. Hamna kitu chochote kilichonitokea. Tangu hapo nikawa mchangiaji wa damu mpaka sasa ni mara yangu ya tano,” anasimulia.

VIJANA NA MTINDO WA MAISHA

Kikwazo kingine kinatajwa kwa kundi la vijana kwamba wengi wao huogopa kujitokeza na kujitolea damu kwa hiyari wakihofia hali zao kiafya.

Johnson Focus ni miongoni mwa wachangia damu wa hiyari anafichua kwa kina “Moja ya changamoto kubwa ambayo tunakutana nayo vijana wa kiume kwa upande wetu ni uwoga, hofu na presha.

“Vijana wengi wa kiume kutokana na kujihusisha na mahusiano bila kupata elimu, kuwa na wapenzi wengi inawapelekea kuwa na hofu.

“Hajui sasa mpenzi wangu yupi anaweza akawa na changamoto fulani, fulani. Kwa hiyo kwenye ‘ishu’ ya kwenda kuchangia damu anajua nitapimwa UKIMWI na magonjwa mengine.

Anaongeza “Kwa hiyo kutokana na kujua kwamba nitapimwa ukimwi, anakuwa na mawazo ikitokea nina ukimwi? Anakuwa na presha.

Hoja hii inaungwa mkono na Mkurugenzi wa Bone and Blood Foundation Neema Mohamed anasema “Vijana wapo wanachipukia katika mahusiano … mwingine … anakuuliza mnapima UKIMWI?.

“Unakuta ujana unamuita, hofu inamuandama, mambo ya kupima anashindwa kujiamini, tofauti na watu wazima unakuyta ameoa, ana watoto anajisimamia na inakuwa rahisi kuchangia damu mara kwa mara”.

Mnandwa Mnandwa anaongeza “Elimu imekosekana jinsi ya kuchangia damu, tumekuwa na akili potofu.

“.., [kwenye jamii] kwamba unapochangia damu leo unapofikia kipindi fulani umeshindwa kuchangia kwa wakati  unaweza kupata madhara fulani.

“Sasa zile ‘story’ [potofu] nahisi zikiondoshwa na elimu ikapatikana sahihi, nahisi tutapata wimbi kubwa sana la vijana watahamasika na kuchangia damu na tukaokoa maisha ya watu wengi,” anasisitiza.

Ni mara ya nane sasa anachangia damu kwa hiyari yake mwenyewe, anasema “Sikuhamasika kwa sababu nilishawahi kupata tatizo au ndugu yangu alipata tatizo hapana.

“Tangu elimu ya sekondari muda ambao umri, kimo na kilo ziliruhusu nilianza uchangiaji damu. Kilichonisukuma ni moyo.

“Kwa sababu tunawachangia wenye uhitaji, sikuweza tu kuanza niliambiwa elimu kuna watu wana shida sana na wanahitaji kupata faraja kutoka kwetu.

“Ule moyo wa upendo kwamba ninachotoa kinaenda kuokoa watu, nilipata hamasa,” anasema.

Neema anasema suala la elimu kwa vijana ni la kutilia mkazo kwani ikiwa watafikiwa zaidi ni wazi kwamba itakuwa rahisi kwa Tanzania kufikia 100% ya mahitaji yake ya damu.

“Kwa Bone and Blood Foundation watu wetu wa hiyari kundi ni miaka ya vijana kuanzia 25 hadi 45 ni sawa na kusema 90% ndilo lililobeba ile data base yetu.

“Imefikia sasa kupitia elimu unaweza kuamka asubuhi ukakuta mtu amekutumia ujumbe leo naenda kuchangia damu,” anasema.

Hata hivyo changamoto inasalia si asilimia kubwa ambao wanaendelea kuwa na uendelevu wa kuchangia kwa hiyari.

“Vijana ni watu ambao bado wanajaribu tofauti na lile lingine la watu wazima, leo ukimpa elimu atakuja na kuchangia ila kesho na michakato ya maisha inakuwa inaingia na kutoka kwa hili kundi.

“Sababu nyingine watu wanahama… tunakosa ‘follow-up’ na kule anakoenda anaosa hamasa ni lazima utamkosa,” anasema.

Johnson anashauri madaktari na wataalamu wa afya pia kutumia njia rafiki zaidi ya jinsi ya kuwasiliana na kundi la vijana ili waendelee kupata hamasa ya kujitokeza na kuchangia damu kwa hiyari.

“Changamoto pia kwa madaktari wajue kizazi chetu si kama kile cha mwaka 1900 vile ambavyo walikuwa wanaweza kuongea nao,”.

Anaongeza “Sisi kizazi chetu kina mabadiliko, kuna lugha ya kwetu [Genz], kuna u-tofauti hata wa misimu na maneno mbalimbali.

“Kuna lugha ambayo ukiongea na kijana mtaelewana. Lakini ukiongea na mtu mzima hamtaelewana,”.

Msisitizo zaidi unawekwa pia, kuongeza nguvu ya  hamsa na mawasiliano kwa njia mbalimbali za kidigitali ili kuvutia kundi hili la vijana wa kizazi kipya, kujenga desturi ya kuchangia damu kwa hiyari.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement