Na Veronica Mrema
Uhaba wa madaktari bingwa wa afya ya uzazi, uchunguzi na tiba dhidi ya magonjwa sugu bado ni tatizo linalokabili nchi nyingi ndani ya Bara la Afrika pamoja na Asia.
Nchi nyingi pia bado zinashuhudia vikwazo vya elimu kwa mtoto wa kike, hali inayohitaji jitihada za kimkakati na madhubuti kuendelea kusaidia kuchochea mabadiliko chanya kwa sekta hizi mbili.
Mstari wa mbele Merck Foundation inazidi kusimama kushirikiana na nchi mbalimbali zilizopo katika mabara haya mawili, kupambana dhidi ya changamoto zinazoendelea kukabili sekta hizo.
Afya na elimu ni sekta zinazogusa maisha ya kila siku moja kwa moja kwa ustawi bora ya jamii na Taifa zinahitajika kuwa imara.
Merck Foundation kwa miaka mingi sasa imekuwa mshirika mzuri kwa kuwekeza katika rasilimali watu kupitia ufadhili wa masomo kwa wataalamu wa afya.
Wakfu huo pia umekuwa ukifadhili program za kijamii zinazolenga kubadilisha mitazamo hasi kuwa chanya ikiwamo kupunguza unyanyapaa dhidi ya waliokosa watoto.
Mkutano wa 13 wa Merck Foundation Africa Asia Luminary 2026 umefanyika 18 & 19, Juni, 2026 kwa njia ya mtandao, ukiwaleta pamoja mabalozi wa wakfu huo katika mabara hayo mawili.
Ripoti nzuri iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Merck Foundation Seneta Dkt. Rasha Kelej inaongeza matumaini ya hatua ambazo zimefanyika katika kukabili changamoto kwa sekta hizo.
"Tumeshatoa ufadhili wa masomo kwa wataalamu wa afya 2,600 kutoka nchi 52 duniani, wamepata mafunzo katika zaidi ya fani 44 zinazohusiana na maeneo yenye uhaba mkubwa wa wataalamu,".
Fani hizo ni pamoja na tiba ya uzazi, embryology, afya ya wanawake, upasuaji wa laparoscopic, afya ya akili, mfumo wa mkojo, magonjwa yasiyoambukiza pamoja na tiba.
Takwimu zinaonesha sehemu kubwa ya wahitimu wa programu hizo sasa wamekuwa miongoni mwa wataalamu wa kwanza wa kibingwa katika nchi zao.
Jambo linalosaidia kubadilisha kwa kiasi kikubwa namna huduma za afya zinavyotolewa, hasa katika maeneo ya vijijini na yale yasiyofikiwa kwa urahisi.
Dkt. Rasha ameongeza "Ufadhili zaidi ya 800 umeelekezwa katika maeneo muhimu ya afya ya uzazi kama vile tiba ya uzazi, embryology, afya ya uzazi wa kijinsia.
"Afya ya wanawake, afya ya akili ya kitabibu, pamoja na ujuzi wa upasuaji na tiba ya familia,".
Lengo kuu la programu hizo si tu kuongeza idadi ya madaktari bingwa, bali kuhakikisha nchi zinakuwa na wataalamu wanaoweza kushughulikia changamoto halisi za kiafya zinazokabili raia wao kila siku.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Merck Foundation Profesa Frank Stangenberg-Haverkamp amesema taasisi hiyo inaendelea kujikita katika dhima ya kuimarisha mifumo ya afya.
".., kupitia uwekezaji wa muda mrefu katika mafunzo ya wataalamu pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma bora na zenye usawa.
"Ushirikiano kati ya serikali, wataalamu wa afya, watunga sera, taasisi za elimu, vyombo vya habari na wadau wa maendeleo umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya programu hizi.
Amesisitiza "Kwa pamoja tunaendelea kupanuka na kuleta matokeo chanya. Tunajitahidi kujenga dunia ambayo kila mtu anaweza kupata huduma bora za afya bila ubaguzi wa aina yoyote.
",,. na hii inawezekana kupitia uwekezaji endelevu katika rasilimali watu,” amesema Prof. Frank.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wake wa marais kutoka nchi mbalimbali ambao ni mabalozi wakuu wa taasisi hiyo.
Nchi hizo ni pamoja na Angola, Botswana, Cabo Verde, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Gabon, Gambia, Kenya, Liberia, Maldives, Msumbiji, Nigeria pamoja na São Tomé na PrÃncipe.
Moja ya mada kuu zilizojadiliwa katika mkutano huo ilikuwa ni changamoto ya ugumba na unyanyapaa unaowakumba wanawake wasiopata watoto.
Wajumbe wa mkutano huo wamesisitiza, jamii bado inahitaji mabadiliko ya fikra ili kuhakikisha haki na heshima kwa wanawake wote.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, kampeni ya “More Than a Mother” inaendelea kutumika kama jukwaa la kimataifa la kupinga unyanyapaa wa ugumba.
kampeni hiyo inatumika pia kuendelea kuhamasisha jamii kuelewa thamani ya mwanamke zaidi ya majukumu ya uzazi pekee.
Pia mkutano huo uliadhimisha Siku ya Wagumba Duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Juni, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa na kuondoa ukimya kuhusu changamoto hizo za kiafya na kijamii.
Dkt. Rasha amesisitiza Merck Foundation imejikita katika kuleta mabadiliko ya muda mrefu kupitia elimu, afya na uhamasishaji wa jami.
Amesisitiza kila mradi unalenga kubadili maisha ya watu moja kwa moja. Taasisi hiyo pia imewekeza katika programu za elimu kwa wasichana kupitia mpango wa “Educating Linda”.
Mpango huo unalenga kuwasaidia wasichana kutoka familia zenye mazingira magumu kuendelea na masomo yao bila kukatishwa.
"Kuna zaidi ya wasichana 1,550 kutoka nchi 21 za Afrika wamepata msaada wa elimu unaojumuisha ada za shule, vitabu, sare na usafiri.
"Hatua hii inalenga kuhakikisha wanakamilisha elimu na kufikia malengo yao ya maisha,' amesema.
Mbali na hilo, Merck Foundation imekuwa ikiendesha kampeni mbalimbali za mabadiliko ya kijamii kupitia vyombo vya habari, sanaa, muziki na filamu ili kuifikia jamii kwa lugha rahisi yenye ushawishi.
Taasisi hiyo imewafikia zaidi ya wanahabari 4,000 kutoka nchi zaidi ya 42 kwa kuwapa mafunzo namna ya kuripoti masuala ya afya na kijamii kwa ufanisi zaidi.
Hatua inayosaidia kuleta uelewa mpana katika jamii. Pia taasisi hiyo imeanzisha tuzo nane za kila mwaka zinazohamasisha ubunifu katika uandishi wa habari, muziki, filamu na mitindo ya mavazi.
Lengo mahususi ikiwa ni kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya na kijamii.
Kwa upande wa sanaa, zaidi ya nyimbo 30 zimeandaliwa na wasanii wa ndani ya Afrika katika lugha mbalimbali zikiwemo Kiingereza, Kifaransa, Kireno na lugha za asili.
Nyimbo hizo zimekuwa na ujumbe wa kuelimisha kuhusu afya na kupinga unyanyapaa pamoja na kuhimiza mtindo bora wa maisha.
Tayari imetengeneza vitabu tisa vya hadithi za watoto vilivyoandikwa katika lugha nne pamoja na filamu sita.
Nyenzo hizo zimelenga kuelimisha kuhusu ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, saratani pamoja na changamoto za unyanyapaa wa ugumba.
Katika upande wa vyombo vya habari vya kidijitali, Merck Foundation pia inaendesha kipindi cha televisheni cha Afrika kinachojulikana kama “Our Africa”.
Kipindi hicho kinatumia sanaa na mitindo ya maisha kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya na kijamii.
Kwa sasa, taasisi hiyo ina zaidi ya wafuasi milioni 9 katika majukwaa 15 ya mitandao ya kijamii, jambo linaloonyesha ukubwa wa ushawishi wake katika kufikisha ujumbe kwa jamii ya kimataifa.
Kwa ujumla, mkutano wa 13 wa Merck Foundation Africa Asia Luminary 2026 umeendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuimarisha mifumo ya afya na elimu.
Taasisi hiyo imeendelea kusisitiza maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa bila kuwekeza katika watu, kubadilisha mitazamo ya jamii na kuhakikisha huduma za msingi zinawafikia wote bila ubaguzi.
Hatimaye, ujumbe mkuu uliotolewa ni kwamba mabadiliko ya kweli katika afya na jamii yanahitaji juhudi za pamoj.
Uwekezaji wa muda mrefu na dhamira ya kweli ya kuhakikisha kila mtu anaishi maisha yenye afya, heshima na fursa sawa.

Chapisha Maoni