Na Veronica Mrema - Dar es Salaam
Uhuru wa kifedha ni kati ya agenda zinazopewa kipaumbele hivi sasa kila kona, jambo la muhimu, mtu hupewa maarifa muhimu yanayoweza kumsaidia kujikomboa kiuchumi.
Kwa sababu ya upekee wake, wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania [TAMWA], wamejengewa uelewa wa msingi kuhusu uhuru wa kifedha.
Ni katika siku ya kwanza ya Mkutano Mkuu wa TAMWA unaofanyika makao makuu yake yaliyopo Sinza Mori, Dar es Salaam.
Pamoja na hilo, mkutano mkuu huo pia unafanyika kwa njia ya kidigitali kupitia mtandao wa zoom.
Rai imetolewa kwa waandishi wa habari kutafuta taarifa sahihi kuhusu taasisi mbalimbali zinazojihusisha na mifuko ya uwekezaji na kuchukua hatua ya kuanza kuwekeza.
Imesisitizwa pia ni muhimu kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii kwani husaidia mno pale mtu anapokumbana na changamoto mbalimbali katika shughuli zake za kila siku.
"NSSF tunatoa mafao aina mbili, kuna ya muda mrefu na ya muda mfupi, tumeboresha pia hasa wanachama wetu wanapofikia umri wa kustaafu,".
Amesema hayo Afisa Mafao wa NSSF Gloria Mackanja, alipokuwa akiwasilisha mada.
"Mfuko wa WCF unatoa mafao mbalimbali ikiwemo fao la utegemezi, pamoja na mafao ya ulemavu wa kudumu na wa muda mfupi,".
Amebainisha hilo, Mkuu wa Idara ya Operesheni na Tathmini kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Amri Kombo.
Amesema wana-TAMWA, taasisi na kampuni wanapaswa kujiunga na mfuko huo ili waweze kunufaika na huduma zake.
Afisa Masoko kutoka UTTAMIS Gosbat Rutasikala amesisitiza "Kuna faida kubwa kuwekeza katika taasisi hiyo, ikiwamo usalama wa fedha za muhusika.
"Tuna mifuko sita, mpaka mtoto/watoto wako unaweza kuwawekea fedha UTT na zikatengeneza faida," amesema.
Afisa Uhusiano kutoka Orbit Securities amewahimiza waandishi wa habari wanawake kutokusalia nyuma katika uwekezaji wa masoko ya hisa.
"Tunashauri uanze kujenga tabia na desturi ya kuwekeza kidogo kidogo, kutokana na mabadiliko ya bei katika soko la hisa," amesema.
Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa TAMWA, Dkt. Kaanaeli Kaale amehimiza waandishi wa habari kuandika habari zenye tija na zinazochochea maendeleo ya jamii.
Mkutano Mkuu wa TAMWA wa mwaka huu unafanyika kwa siku mbili April, 17 & 18 ambapo pia wajumbe watapitisha rasmi Katiba mpya.


Chapisha Maoni