Na Veronica Mrema
Ndani ya Jiji la Lagos, waanzilishi wa taasisi na wadau wa masuala ya afya wanaoangazia magonjwa ya Siko Seli [SCD] pia Saratani kwa watoto kutoka nchi zaidi ya 10, wamekutana pamoja.
Siku mbili [April 12 & 13, 2026] wamekuwa hapa, lengo ikiwa kujifunza baina yao, kushirikiana na kuimarisha juhudi za kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa na magonjwa hayo, Afrika.
Ni jukwaa la wazi la kubadilishana uzoefu wa namna taasisi hizi zinavyofanya kazi ndani ya nchi zao na namna bora ya kusonga mbele kwa pamoja.
Ukweli wa mambo kila kitu huanza na dhamira, kikao hiki ni matokeo ya juhudi za St. Jude Children's Research Hospital.
Dhamira hii ilianzishwa na Danny Thomas ambaye historia inaeleza kabla ya mafanikio makubwa aliwahi kupitia kipindi kigumu cha maisha.
Katika hali ya kukata tamaa, alimlilia Saint Jude, akiomba si mali bali mwelekeo wa maisha.
Ahadi yake ya kujenga “heshima” ilikuja kuwa taasisi inayookoa maisha ya maelfu ya watoto duniani,"
Ili kuifanya ndoto hiyo iwe halisi, ALSAC ilianzishwa mwaka 1957 hata kabla ya hospitali kujengwa.
Leo, ALSAC ina jukumu la kukusanya rasilimali, kuendesha kampeni za uhamasishaji, na kuimarisha uwezo wa St. Jude Children's Research Hospital kufikia watoto wengi zaidi duniani.
Mfumo huu wa ushirikiano umeendelea kuwa somo muhimu kwa nchi nyingi zinazoendelea, hususan Barani Afrika,'.
“Ushirikiano huu unaonesha nguvu ya pamoja katika kubadilisha maisha ya watoto Barani Afrika. Tunapoleta pamoja uzoefu, rasilimali na dhamira ya dhati.
"Tunajenga msingi imara wa kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kuishi maisha yenye afya.
"Kazi hii haihusu taasisi moja pekee, bali ni mwitikio wa pamoja wa kuhakikisha hakuna mtoto anayesahaulika,” anasema Drew Phillips, Sr. Director Foundation Engagement.
PICHA YA AFRIKA
Pamoja na mafanikio ya tiba duniani, Bara la Afrika bado linabeba mzigo mkubwa wa magonjwa ya watoto.
Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, zaidi ya watoto 300,000 huzaliwa kila mwaka duniani wakiwa na Sickle Cell Disease, na zaidi ya asilimia 75 ya watoto hao wanatoka Afrika.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda na Tanzania ugonjwa huu unaendelea kuwa changamoto kubwa ya afya ya umma.
Kwa upande wa Tanzania, hali ni ya kutia wasiwasi zaidi. Nchi hii inatajwa miongoni mwa mataifa yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa Siko Seli Barani Afrika.
Hivi sasa idadi ya wanaozaliwa na ugonjwa huo imetoka wastani wa watoto kati ya 8,000 hadi 11,000 na kufikia hadi 14,000 kila mwaka.
Hali hii inaonesha bado kuna uhitaji mkubwa wa uelimishaji jamii kuchunguza mapema hali zao za vinasaba.
Changamoto nyingine ni kwamba bado kuna idadi kubwa ya watoto wanaofariki mapema kabla ya kufikia umri wa miaka mitano kwa ugonjwa huu.
Picha ya namna hii ipo pia kwa upanda wa saratani za watoto katika ukanda huu wa Kusini mwa Jangwa la Sahara bado zinakabiliwa na changamoto za kugunduliwa kwa kuchelewa.
Suala la upatikanaji mdogo wa huduma za kibingwa, na uelewa mdogo wa jamii hali inayopunguza uwezekano wa mafanikio ya matibabu.
Ni wazi bado kuna kazi kubwa ambayo taasisi hizi zinawajibika kutekeleza ili kusaidia kuokoa uhai wa watoto wanaozaliwa na magonjwa haya Barani Afrika.
Danny Thomas aliamini na kusisitiza , “hakuna mtoto anayepaswa kufa mwanzoni mwa maisha yake,”
Kauli ambayo inaungwa mkono na washiriki waliopo ndani ya ukumbi wakikubaliana kwamba mabadiliko huanza pale mtu mmoja, taasisi moja, au jamii moja inapochukua hatua.
Kwa kuunganisha nguvu, maarifa, na uzoefu, inawezekana kubadilisha simulizi ya afya ya watoto barani Afrika.
NGUVU YA PAMOJA
Meneja Progamu wa Lifeline for Childhood Cancer Ghana Portia Asantewaa Agyekum ni miongoni mwa wanufaika wa kwanza wa SSA St. Jude Global scholar program.
Anasema ni darasa lililompa mwanga mpya katika utekelezaji wa majukumu yake na taasisi hiyo kwa ujumla.
Mabadiliko yamekuwa ndani na nje kwa wakati mmoja hasa katika kupata mbinu mpya za kusaidia utafutaji wa rasilimali ili kuendesha taasisi yao.
“Baada ya mafunzo, tulianza kutumia mikakati mipya ikiwemo 'dinner', pamoja na kuimarisha uwepo wetu kwenye mitandao ya kijamii na redio,” anaeleza.
Changamoto kubwa ilikuwa ni imani ya jamii, katika mazingira ambayo baadhi ya mashirika yalipoteza uaminifu hapo awali, ilikuwa vigumu kuwashawishi wafadhili.
Hata hivyo, anasema programu hiyo imeleta uthibitisho wa kazi yao. “Sasa watu wanaona thamani ya kazi yetu na wanaanza kutuamini.”
Kwa upande binafsi, anasema amepitia mabadiliko makubwa ya kisaikolojia na kiutendaji.
Kutoka kuwa mtu wa aibu na asiyejiamini, sasa anaweza kuzungumza kwa ujasiri, kujenga mahusiano, na hata kuwafikia wadau kupitia njia rahisi kama ujumbe wa moja kwa moja.
MTIZAMO CHANYA
Ni mwaka wa 21 sasa Sidney Chahonyo kutoka Hope for Cancer Kids nchini Kenya anasherehekea ushindi wake dhidi ya saratani.
Uzoefu huo ndiyo ulimsukuma kuanzisha taasisi anayoisimamia akiwa amefikisha idadi ya zaidi ya watoto 500 wanaowapatia msaada kila mwezi hivi sasa.
Sidney naye ni mnufaika wa St. Jude Global Scholar program anasema watoto hao wanapatia matibabu, usafiri, malazi, msaada wa kisaikoloia na hata tiba kwa njia ya sanaa.
"Programu ya Global Scholars imebadili kabisa mtazamo wangu, kutoka kufikiria kwa kiwango kidogo hadi kupanga kimkakati kwa muda mrefu.
".., ikiwemo kushirikiana na wadau wakubwa na kuvutia rasilimali zaidi,' anasema.
MIFUMO UTENDAJI
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Uganda Child Cancer Foundation Moses Echodu - Uganda anasema darasa hilo limekuwa safari ya kujifunza na kujenga uaminifu zaidi kaika utendaji kazi wake.
"Kabla sijaanza darasa uwezo wetu kutafuta ufadhili ulikuwa duni, wengi hawakutumiani, lakini baada ya mafunzo tumeimarika.
"Kwa mfano kuhusu utafutaji wa rasilimali, mwelekeo wa taasisi yetu umebadilika sana, mapato yameongezeka kutoka Dola 15,000 hadi 36,000.
"Tulianzisha mfumo wa kuwasiliana na wafadhili wa kila mwezi, inajenga uaminifu zaidi, tunaonesha taarifa namna tunavyoenenda .
"Imeongeza ushirikiano zaidi, uwazi na uwajibika, uaminifu ni kila kitu katika utendaji kazi kwa sababu bila watu kukuamini, hawawezi kukuunga mkono,” anasisitiza.
Moja ya mafanikio makubwa yaliyojitokeza ni mabadiliko ya namna mashirika yanavyoendesha shughuli zao.
Awali, baadhi yao walikuwa wakifanya kazi katika hali isiyo rasmi “organized chaos.”
Lakini sasa kuna mabadiliko makubwa kila jambo lina mfumo, kila tukio lina mkakati na kila ujumbe una lenga hadhira
Somo kuu lililojitokeza ni kwamba mafanikio hayawezi kuwa ya mtu mmoja, ni juhudi za pamoja kati ya wafanyakazi, viongozi na bodi za wakurugenzi
Ndani ya taasisi kwa pamoja, wanahusika katika maamuzi, utekelezaji na utafutaji wa rasilimali.
Katika enzi ya mitandao ya kijamii, washiriki wanasisitiza umuhimu wa maadili katika kusimulia hadithi kw kuzingatia pia ulinzi wa faragha ya mtoto/watoto.

Chapisha Maoni