Na Veronica Mrema - Dar es Salaam
Chukulia mfano halisi, inapotokea janga fulani zito ndani ya jamii, mathalani ajali ya barabarani au majini au matukio ya kutisha nakadhalika.
Ni jambo la kawaida mwandishi wa habari kuagizwa na ofisi yake kwenda eneo la tukio ili kuchukua taarifa ambazo atazichakata na kuwa habari au makala kwa ajili ya chombo anachokitumikia.
Kundi la waandishi wa habari limekuwa likikutana na mambo yanayoathiri afya zao za akili kwa namna moja au nyingine.
"Kwa mfano kama ni ajali unaweza kuona miili ya marehemu au damu zimetapakaa, ni hali inayoumiza saikolojia," amesema Mhariri wa Habari kutoka Clouds Media Group Joyce Shebe.
Shebe alikuwa sehemu ya wachechemuzi wa mada katika mjadala ulioandaliwa kwenye Kongamano la kwanza la Malikia wa Habari.
Ameongeza "Unakusanya habari, unarudi ofisini, unaandika na inatoka kwenye media yako, lakini sasa unaondoka ukiwa na ile 'trauma'.
"Kwa sababu ya mazingira ya kazi yao ikiwemo kufanya habari za uchunguzi, kuripoti matukio ya kutisha, pamoja na kukabiliana na unyanyasaji wa kimtandao.
Shebe ameongeza "Tunakumbana na changamoto zinazoweza kuacha majeraha ya kihisia, msongo wa mawazo, na hata kuathiri afya yao ya akili kwa ujumla.
"Sasa, kwa kweli 'neswroom' zetu hazina program za usaidizi wa kisaikolojia, lakini kiuhalisia tunapata changamoto ya akili, kutokana na mazingira ya kazi zetu za kila siku," amesema.
Hoja ya Shebe zinawiana sawia na wasilisho la mada ya Daktari Raymond Mgeni kutoka Taasisi ya Waandishi wa Habari za Afya ya Akili Tanzania [TAMHJO] katika kongamano hilo.
TAMHJO ilikuwa miongoni mwa wadhamini, ikiwa pia ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati yake ya kuhakikisha inawafikia kundi kubwa zaidi la waandishi wa habari nchini Tanzania.
Dkt. Raymond amesisitiza kuna haja ya kuwapo kwa huduma za msaada wa kisaikolojia kwa kundi la waandishi wa habari pasipo kuwaacha nyuma wanawake.
"Ni muhimu kuzungumzia afya ya akili kwa uwazi, pamoja na kuunda mazingira rafiki yanayowezesha upatikanaji wa msaada wa kisaikolojia," amesisitiza Dkt. Raymond.
Ameongeza ".., hasa kwa waandishi ambalo mnakutana na unyanyasaji wa kimtandao, kimwili, au kushuhudia matukio ya kutisha wanapotekeleza majukumu yenu ya kazi.
Pamoja na hilo, aliwapa elimu ya jinsi ya kutunza afya zao za akili, huku akiwahimiza pia kuwasilisha vema taarifa zinazohusu afya ya akili kwa jamii nzima.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuendelea kupunguza unyanyapaa ndani ya jamii, kuwapa maarifa sahihi wananchi na hivyo kujenga afya njema ya akili..
Kongamano la Malikia wa Habari limefanyika Machi 28, 2026 Mkoani Dar es Salaam na kujumuisha waandishi wa habari wanawake wapatao 60 kutoka vyumba mbalimbali vya habari.
Akilifungua Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki amesema ni wazi lina tija kwa waandishi wa habari na jamii pia.
Amesema Serikali inatambua na kupongeza mchango mkubwa wa waandishi wanawake katika kukuza na kuimarisha sekta ya habari nchini.
"Kuna fursa nyingi, tasnia ya habari na mawasiliano ambazo wanawake mnapaswa kuzichangamkia na Serikali ipo tayari kushirikiana nanyi, kuhakikisha mnazifikia,".
Amehimiza pia, ni muhimu wa umoja kwa waandishi wa habari wanawake wote waliopata ithibati, ili kurahisisha utambuzi wao rasmi Serikalini.
Mratibu wa Kongamano hilo, Penina Malundo, amesema lengo kuu ni kuwaleta pamoja waandishi wa habari wanawake ili kujadili changamoto zinazowakabili na kuinua sauti yao kwa pamoja.
Lengo jingine ni kushirikiana katika shughuli za kijamii ili kila mmoja aweze kufikia malengo na kutimiza ndoto alizonazo.


Chapisha Maoni