moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema – Afrika Kusini

Uhai wa dunia hadi sasa ni takriban miaka zaidi ya bilioni 3.6 kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na wanasayansi, hii ni sayari yenye historia isiyo na kifani.

Kuna shahidi za kusisimua, tafiti zinaeleza kuna miamba ya zamani zaidi duniani, ambayo ipo mbali upande wa Mashariki mwa Australia na mengine ipo Kaskazini mwa Perth.

Miamba mingine ipo Kusini mwa Afrika karibu na Kruger Park katika eneo la Barberton.

Wanasayansi wanaeleza huko kwenye maeneo hayo kuna ushahidi wa awali wa maisha ya kale, ikiwa ni pamoja na mimea vile vile wanyama hadi zana zilizowahi kutumiwa na binadamu wa kale.

Kwa mantiki ya shahidi hizo za tafiti za wanasayansi, historia inaonesha wigo wa maisha kwa miaka zaidi ya bilioni 3.6 kufikia sasa.

Chuo Kikuu cha WITS kilichopo hapa Pretoria, Afrika Kusini, jitihada kubwa zilifanyika katika tafiti na bado zinaendelea kufanyika, wakiangazia kwa kina asili ya binadamu, duniani.

M24 TANZANIA MEDIA imefika ndani ya chuo hiki, miongoni mwa vyuo vikongwe zaidi Barani Afrika.

Mafuvu ya viumbe vya kale, mifupa, nyaraka nyingi zenye vielelezo zipo hapa, mengi tumejionea na tumeelezwa, ndiyo msingi wa kuandikwa kwa makala haya.

Desemba 5, 2025 tupo ndani ya chumba maalum cha makumbusho ya kale, ambamo pia ni sehemu ya maabara maalum ya chuo Kikuu cha WITS.

Hii ni ziara maalum ya ki-mafunzo, ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizoandaliwa na waandaaji wa mkutano wa 13 wa Kimataifa wa Waandishi wa Habari za Sayansi Duniani [WCSJ - 2025].

Kwa mara ya kwanza WCSJ umekutanisha waandishi wa habari wa masuala ya sayansi kutoka nchi zipatazo 80 duniani.

Chuo hiki kimeweka jitihada kubwa, ikiwamo taasisi maalum Evolutionary Studies Institute [hapa tulipotembelea].

Hii ni moja ya sehemu bora zaidi duniani zinazochunguza historia ya maisha ya binadamu na dunia kwa ujumla.

Taasisi hii ina wanyama na mimea ya ajabu kutoka kipindi cha kale, lakini moja ya maeneo yake muhimu ni ‘evolusheni ya hominid’.

Simulizi ya makala haya imebeba maelezo ya msingi kabisa, ya kuvutia ambayo tulipatiwa na Prof. Bernard Zipfel ambaye alikuwa mwenyeji wetu katika ziara hii, karibu ufutane nasi.

UNDANI WA HOMINID

Unaweza sasa kuwa unajiuliza ni kitu gani hiki, ndugu msomaji wetu, Hominid ni kiumbe aliyekuwa anakalia miguu miwili na aliishi kwenye miti.

Kiumbe huyu alikuwa na maumbile yanayofanana kwa ukaribu sana na nyani pamoja na binadamu kama ilivyo sasa.

Prof. ambaye alikuwa mwenyeji wetu katika ziara hii anasema kiumbe huyu aliishi takriban miaka milioni 15 iliyopita.

Kwa hiyo tumetokana na kiumbe huyu mmoja kutoka hapo ‘mizizi’ [vizazi] mbalimbali ya binadamu na nyani ilitokea.

Nyani wa kisasa na binadamu wa kisasa wote ni sehemu ya mchakato huu wa ‘evolusheni’. Kuna tafiti zinaeleza Hominid wa zamani zaidi aliyeonekana hadi sasa ni wa takriban miaka milioni 7.

Sampuli yake imepatikana Chad, Afrika Magharibi na maumbile ya awali [mifupa] yamepatikana Uruguay, Kenya, Ethiopia, na kusini mwa Afrika.

Hominid wa zamani zaidi utakaoonekana katika maktaba ya hapa WITS ina takriban miaka milioni 3.5.

Jambo linaloonekana kama miaka kidogo pale ikilinganishwa na muda maisha yamekuwa duniani, milioni 3.5 dhidi ya bilioni 3.6, kwa mujibu wa Prof.

BINADAMU WA SASA

Kwa historia ya mwanadamu, kuna sehemu ya ‘Origin Center’ ndani ya Chuo Kikuu cha WITS ambamo inasimulia hadithi ya binadamu wa kisasa [tutaeleza katika makala ijayo].

Binadamu wa sasa wamekuwa duniani kwa takriban miaka 300,000 tu. Hominid na binadamu wa sasa wote asili yao ni Afrika, baadae wakahama kwenda Asia, kisha Ulaya.

Prof. anasema kwa kuwa Australia na Marekani zilikuwa mbali sana, binadamu wa sasa walifika pale miaka 40,000 iliyopita.

Ni binadamu wa sasa tu waliokuwa na uwepo wa mbali, hominid hawakuwahi kuenea nje ya Asia na Ulaya, isipokuwa Neanderthals na baadhi ya spishi zinazofanana.

SIRI YA MAUAJI YA KALE

Upo ushahidi wa moja ya mifano ya kuvutia ambayo ni ‘Taung Child’, huyu ni kiumbe mdogo umri wake ni takriban miaka milioni 2.5, ki-historia jina lake ni Australopithecus africanus

Fuvu lake lipo hapa ndani ya Chuo Kikuu cha WITS huyu alikuwa mtoto wa takriban miaka mitano, na alikuwa hominid pekee aliyeonekana pale ‘Taung’.

Uchunguzi wa kisayansi umeonesha kwamba Taung Child aliuwawa na tai, jambo ambalo lilikuwa siri kwa muda mrefu.

Watafiti Profesa Lieberger na Profesa Ron Clark waliangalia alama za mapigo nyuma ya macho na alama ndogo za kuungua kwenye mfupa.

Uthibitisho ulipatikana baada ya Profesa Berger kuona nyani waliouawa na tai waliokuwa na taji, ambapo makucha ya tai yalipita kwenye sehemu ya nyuma ya macho.

SIRI ILIJULIKANA VIPI?

Tai hao walichukua ubongo wa hominid huyo kwa sababu ya protini nyingi. CT scan na uchunguzi wa makini wa mfupa unaonesha alama za makucha na kuchomwa katika sehemu yake ya uso.

Sababu za ki-sayansi za kuchunguza mtoto mdogo ni nyingi: ukubwa, mdogo wa ubongo, kuwa ni mtoto, na sababu za kisiasa.

Wakati huo, mtazamo wa kikoloni wa kifalme ulikuwa binadamu lazima atoke Ulaya. Wanasayansi wa wakati huo walikataa kwa muda mrefu asili yetu Afrika.

Ilibidi kusubiri takriban miaka 25 kabla ya kushughulikia ushahidi huu vyema. Leo, bila shaka, tunajua binadamu anatokea Afrika.

AFRIKA MASHARIKI

Kuna ushahidi mwingine wa kuvutia wa hominid wa awali [maisha ya binadamu wa kale], sampuli ya kwanza ya Australopithecus afarensis kutoka Afrika Mashariki.

Pia kuna Paranthropus robustus kutoka Afrika Kusini na ushahidi wa viumbe Australopithecus africanus waliopatikana kusini mwa Afrika.

Ushahidi huu unaonesha kwa wazi kuwa Afrika ni asili ya mwanadamu wa awali.

Aidha, kwa binadamu wa sasa ushahidi wa molekuli unaonesha protini na vinasaba vya mwanadamu vinathibitisha kuwa binadamu wote wanatoka Afrika.

Ingawa ‘fosili’ [mabaki ya mifupa ya viumbe vya kale] nyingi zinapatikana mashariki na kusini mwa Afrika, si lazima kwamba pale ndiko walikokuwa binadamu wote.

Bali pale ndipo ‘fosili’ zilipohifadhiwa. Hivyo, wanapaita maeneo haya ‘Cradle of Humankind’, hii maana yake ni pale ambapo historia ya mwanadamu ilihifadhiwa vyema.

‘LITTLEFOOT NA HOMO NALEDI’

Ndani ya maabara hii kuna hominid mwingine wa ajabu aliyeitwa Australopithecus prometheus, au Littlefoot, aliishi duniani takriban miaka milioni 3.6 iliyopita.

Mfupa wake wa mguu ulipatikana kwanza na Profesa Ron Clark, na mfupa mzima ukapatikana baada ya miaka 21 kutoka pango la Stankfontein, nje kidogo ya Johannesburg.

Littlefoot ni mfupa kamili zaidi wa Australopithecus duniani na bado unasomwa na wanasayansi.

Upo mfano mwingine uliochapwa mnamo 2008, kutoka Malaka, pamoja na Australopithecus prometheus, ulio na umri wa takriban miaka 2.6 hadi 1.5.

Mfano huu bado unasomwa kwa makini na wanasayansi, pamoja na sampuli nyingi mpya nazo zinaendelea kuongeza uelewa wao kuhusu hominid hao.

Mfano huu ni mtoto wa kiume wa takriban miaka 11 na upande mwingine kuna mwanamke mzima.

Ndani ya makumbusho ya WITS pia wana Homo naledi, sampuli zilizopatikana mnamo mwaka 2013, zikiwa na zaidi ya sampuli 3,000, katika pango dogo takriban mita 30 chini ya ardhi.

Wanasayansi wanasema Homo naledi ni [viumbe] wa kuvutia kwa sababu walikuwepo takriban miaka 240,000 iliyopita, wakati binadamu wa sasa tayari walikuwa duniani.

AFRIKA MSINGI WA HISTORIA

Historia ya mwanadamu ni ya kipekee yenye maajabu mengi, yanayoenda sambamba na msururu wa shahidi za kisayansi usio na kifani.

Umeona msisimko wake tangu hominid wa milioni 7 hadi binadamu wa sasa wenye miaka 300,000 ndani ya sayari ya dunia.

Historia hii inaonesha ukuaji wa akili, sura, mwili na mabadiliko yake ya maisha. Afrika si tu asili ya  mwanadamu alipoanza, bali ni msingi wa historia ya binadamu wa sasa.

Unapoanzia pale Barberton, Taung, Stankfontein, Malaka hadi Homo naledi, unaona jinsi historia ya dunia inatufundisha kwa ajabu na kutupa nafasi ya kuelewa sisi ni wakina nani!.

Historia hii ni changamoto, ya kuvutia na yenye mvuto mkubwa kwa kila mtu anayetaka kuelewa asili yetu na safari ya binadamu.

Mfululizo wa simulizi kuanzia jicho la mwanadamu mdogo lililokatwa na tai, hadi Littlefoot na Homo naledi.

Ushahidi wa tafiti za ki-sayansi na ki-historia unaendelea kutufundisha kuwa historia ya mwanadamu ni tajiri, yenye ushahidi wa kisayansi na ajabu zisizoisha.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement