Dar es Salaam
Mchango wa waandishhi wa habari za mtandaoni unatambuliwa na Serikali ya Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza waandishi wa habari wa Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA).
Ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwalea vizuri na
kuwapa fursa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Pongezi na maelekezo hayo yamewasilishwa na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa
Serikali, Bw. Gerson Msigwa, alipofunga kikao cha pamoja cha wanachama wa TBN na JUMIKITA kilichoandaliwa na TCRA jijini Dar es Salaam, Desemba 18,
2025.
Bw. Msigwa alisema Rais Samia anatambua mchango mkubwa wa
waandishi wa habari za mtandaoni katika kusambaza taarifa na kuimarisha
mawasiliano kati ya serikali na wananchi, hivyo akaagiza wapewe malezi,
miongozo na fursa zitakazowawezesha kufanya kazi zao kwa weledi.
“Mheshimiwa Rais amewapongeza sana na anatambua kazi zenu
nzuri. Ni maelekezo yake kwamba kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Idara ya Habari MAELEZO na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari kupitia TCRA, waandishi wa habari za mitandaoni na bloga walelewe vizuri
na wapewe fursa ili wafanye kazi zao vizuri,” alisema Msigwa.
Alisisitiza kuwa maelekezo hayo ni maagizo ya moja kwa
moja kutoka kwa Rais na kwa utaratibu wa kiserikali, yanapaswa kutekelezwa bila
mjadala.
“Haya kwetu ni maelekezo. Kwa utaratibu wa serikali,
ukishapewa maelekezo kinachofuata ni utekelezaji. Ndiyo maana tupo hapa
kuhakikisha maagizo ya Mheshimiwa Rais yanatekelezwa,” alisema Msigwa huku
akishangiliwa na washiriki wa kikao hicho.
Aidha, alisema mwelekeo huo unaendana na falsafa ya
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
inayosisitiza ushirikiano kati ya serikali na wadau mbalimbali kwa manufaa ya
taifa.
Aliitaja Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la
Mitandao Tanzania (JUMIKITA) kuwa ni wadau wakubwa wa serikali katika tasnia ya
habari, akibainisha kuwa mchango wao ni muhimu katika kusambaza taarifa sahihi
na kujenga mawasiliano yenye tija kati ya serikali na wananchi.
“Serikali imewaamini waandishi wa mitandaoni. Sasa ni
wajibu wenu kuendeleza imani hiyo kwa kuzingatia maadili, ukweli na uzalendo
katika kazi zenu. Ushirikiano wetu umeendelea kuimarika na changamoto
zinazojitokeza tunazitatua kwa pamoja,” alisema Msigwa.
Kikao hicho kililenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wadau wa habari za mtandaoni pamoja na kujadili masuala ya maendeleo ya tasnia ya habari katika mazingira ya kidijitali.


Chapisha Maoni