Na Veronica Mrema - Afrika Kusini
Ongezeko kubwa la idadi ya wavutaji sigara limeshuhudiwa katika kipindi cha miaka 15 mfululizo, ndani ya Bara la Afrika licha ya kuwapo juhudi za muda mrefu kwa mataifa yake, kupambana na janga hilo.
Afrika hasa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na zile zilizopo Mashariki ya Kati, ni miongoni mwa maeneo machache duniani ambako idadi ya wavutaji sigara zinazotoa moshi, imeendelea kuongezeka maradufu.
Shirika la Afya Duniani [WHO], inataja idadi ya wavutaji Barani Afrika hususan nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara imetoka watu milioni 52 mwaka 2000 hadi watu milioni 66 mwaka 2015.
WHO iliyo chini ya Umoja wa Mataifa [UN] inaonya huenda idadi hiyo itaongezeka zaidi hadi watu milioni 84 kufikia mwishoni mwa mwaka 2025
Ni sawa na ongezeko la 60%, ikiwa juhudi zaidi hazitachukuliwa na dunia dhidi ya janga hilo.
Ni suala linaloibua hoja nzito katika mkutano wa TECHNOVATION - 2025 [Smoke Free] uliofanyika Cape Town nchini Afrika Kusini.
Jukwaa ambalo linawaleta pamoja madaktari, watafiti na waandishi wa habari kutoka kona nchi mbalimbali za Afrika, kujadili kwa kina.
Msisitizo ukielezwa kwamba ni wakati sasa kwa Bara hilo kugeukia mbinu za ki-teknolojia ambazo zitasaidia kupunguza athari.
Kwamba zimefanyiwa utafiti kwa miaka zaidi ya 10 na kuonesha matokeo chanya katika baadhi ya mataifa yaliyoendelea.
"Wakati idadi ya watumiaji inaongezeka zad Afrika, duniani kote hasa katika nchi zilizoendelea kama Ulaya, Amerika Kaskazini na baadhi ya maeneo ya Asia, idadi hiyo imekuwa ikipungia,".
Yameelezwa hayo na Makamu wa Rais, Mawasiliano na Ushirikishwaji wa kampuni ya Philip Morris International [PMI] Tommaso Di Giovanni alipokuwa akifungua mkutano huo.
Maafisa wa PMI, watafiti, madaktari na waandishi wa habari wa mataifa mbalimbali Barani humo, wameketi pamoja kujadiliana kwa kina kuhusu nafasi ya teknolojia katika kutatua changamoto hiyo.
"Bidhaa za teknolojia zimesaidia kutatua changamoto nyingi katika maisha ya binadamu, duniani," amesema Tommaso na kusisitiza zaidi..,
"Afrika imeonesha mafanikio makubwa katika kukumbatia teknolojia kama vile Wi-Fi, simu janja, benki mtandao kwa njia ya simu, nishati ya jua vile vile huduma za afya kwa njia ya masafa ya mtandao [telemedicine],".
PMI imewekeza zaidi ya Dola Bilioni 14 katika tafiti, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za ki-teknolojia za sigara zisizotoa Moshi ikiwa ni jitihada zake katika kukabiliana na janga hilo.
PMI imeweka wazi, zaidi ya 40% ya mapato yake ya kimataifa sasa hivi yanatokana na bidhaa zisizo na moshi.
"Tunahitaji sera zinazotofautisha kati ya sigara na bidhaa mbadala. Kodi nafuu, upatikanaji wa taarifa sahihi, na sheria rafiki kwa bidhaa hizi, vitachochea mabadiliko ya haraka," alisema mmoja wa wakurugenzi wa PMI.
"Teknolojia hizo ni pamoja na sigara za kupasha joto [heated tobacco], vifaa vya kielektroniki vya kuvuta [e-vapes] na pakiti za nikotini [nicotine pouches]," amebainisha Dkt. Buhle Binta.
Binta ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Ushirikiano wa Kisayansi katika Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara - PMI.
Hata hivyo si mataifa yote ya Afrika, ikiwamo Tanzania ambayo yameridhia moja kwa moja bidhaa hizo za PMI.
Mataifa mengi ya Afrika pia bado hayana kabisa Sera zilizotungwa kwa ajili ya bidhaa hizo, kuzikubali, kuzipokea na kuruhusu ziingie rasmi katika masoko yao.
PMI yenyewe imesisitiza bidhaa hizo ni njia mbadala itakayosaidia kupunguza idadi ya wavutaji kwa siku zijazo.
"Mtumiaji wa sigara anaendelea kuiwasha na kuitumia kwa sababu anahitaji ile nikotini iliyopo mule ndani, [sasa] bidhaa hizi za ki-teknolojia ambazo PMI imetengeneza zipo tofauti," amesema Dkt. na kuongeza,
"[Ni kweli] huendelea kutoa nikotini ambayo wavutaji huitafuta, lakini zenyewe hazitoi moshi wa tumbaku ambao huo ndiyo huleta athari kwa kusababisha magonjwa hatari kama saratani, matatizo ya moyo na mapafu.
"Tafiti zimeonesha bidhaa hizi kwa kiasi kikubwa zinaweza kupunguza kemikali hatarishi zinazopatikana kwenye moshi wa sigara [pindi inapochomwa],".
TECHNOVATION - 2025 inahimiza zaidi nchi za Afrika kuchagua sayansi katika kutatua changamoto zake badala ya hisia, vile vile kujikita katika ubunifu badala ya mazoea.
Mkurugenzi wa Masuala ya Nje kwa Kanda ya Kusini kwa Afrika - PMI Themba Mathebula amesema wana Imani kubwa ushirikiano wa sekta binafsi, Serikali na jamii, utaleta matokeo chanya ndani ya Bara la Afrika.
"Teknolojia hizi mpya za tumbaku zisizo na moshi zinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika kulinda afya ya jamii dhidi ya sigara zinazotoa moshi,” amesema.
Amesisitiza "Teknolojia mpya ya sigara za [kupasha] joto, e-vapes, na pakiti za nikotini ni suluhisho mbadala zinazoweza kusaidia kupunguza madhara ya tumbaku kwa wavutaji sigara watu wazima.
Wakichangia mjadala huo, baadhi ya wadau wametoa wito kwa Serikali za nchi za Afrika kuachana na sera za zamani zinazokwamisha matumizi ya bidhaa mbadala zisizo na moshi.
Badala yake wazingatie ushahidi wa tafiti za kisayansi na kuunda Sera zinazoendana na wakati ili kuokoa maisha ya mamilioni ya Waafrika wanaovuta sigara na kundi la wale wasiovuta moja kwa moja.
Mkutano huo uliandaliwa na PMI kwa dhima ya kuweka mtizamo chanya kuelekea kupunguza athari za uvutaji sigara kwa watumiaji 'Tobacco Harm Reduction'.
Pia athari za moshi utakaonao na tumbaku kwa afya ya jamii, ulipewa kauli mbinu ambayo inaweka msisitizo na msimamo thabiti juu ya kile wanachokipambania.
"Ikiwa haujawahi kuvuta sigara, Usianze. Ikiwa unavuta, acha kabisa. Lakini ikiwa umeshindwa kuacha, chagua mabadiliko, tumia bidhaa mbadala zisizotoa Moshi ili kuwalinda wengine na afya yako pia,".
Chapisha Maoni