Kila siku duniani kuna mamilioni ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaokatishwa ndoto na uhai wao, takwimu zinaonesha zaidi ya 45% ya vifo hivyo vinahusishwa na utapiamlo.
Lishe duni ni adui asiyeonekana anayeangamiza kimya kimya idadi kubwa ya watoto kila siku duniani.
Nchi ya Tanzania iliyopo Ukanda wa Afrika Mashariki nayo inaendelea kushuhudia viwango vya udumavu miongoni mwa watoto.
Licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania [TFNC] kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo, bado ni 'mtihani'.
Utapiamlo bado ni tatizo kubwa la ki-afya na ki-uchumi, rai ikitolewa juhudi zaidi na ushirikiano wa sekta nyingi zinahitahika, kukomboa kizazi chake kijacho.
"Kundi la waandishi wa habari ni miongoni mwa wadau muhimu wanaohitajika katika ushirikiano huu, ili kusaidia jamii kupata elimu na kuwa na uelewa sahihi kuhusu lishe kwa ujumla wake,".
Kauli yake Afisa Utafiti Mchumi ndani ya TFNC Geoffrey Chiduo wakati alipokuwa akiwasilisha mada katika warsha maalum kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Warsha hiyo iliandaliwa hivi karibuni na TFNC na Jukwaa la Lishe Tanzania [PANITA] lengo ikiwa kuwaongezea uelewa kuhusu changamoto, hatua na mikakati ya Kitaifa katika kukabili utapiamlo.
Utapiamlo ni tatizo mtambuka ambalo halihusiani na uhaba wa chakula pekee, bali pia mila, desturi, elimu, hali ya uchumi wa familia, na upatikanaji wa huduma bora za afya na maji safi.
Wataalamu wa masuala hayo ya lishe wanasema baadhi ya athari zake kama vile udumavu zinaweza kuwa za kudumu kwa maisha yote ya mtu.
"Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwamo kuanzishwa kwa TFNC mwaka 1973 kwa mujibu wa Sheria ya Bunge," anasema Chiduo.
Anasema pia Serikali imekuwa ilijiunga na majukwaa ya kimataifa yanayoangazia masuala ya lishe (Scaling Up Nutrition Movement) mwaka 2010.
"Upo utekelezaji wa mpango jumuishi wa kitaifa wa lishe unaojumuisha sekta mbalimbali kama afya, kilimo, elimu, maji na ulinzi wa jamii," anasema.
Tanzania pia ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza barani Afrika kuajiri Maafisa Lishe katika mikoa na halmashauri zote, na kuanzisha madawati ya lishe katika wizara 11.
Suala hilo uratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, "Ipo dhamira ya ki-siasa pia, mwaka 2013 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua kampeni ya kitaifa ya lishe," amesema Chiduo.
Kampeni hiyo ilipewa kauli mbiu: "Lishe bora ni msingi wa maendeleo endelevu, shiriki wajibu wako."
MATONE
TFNC pia ilieleza utekelezaji wa programu mahsusi kama vile utoaji wa matone ya Vitamin A na dawa za minyoo kwa watoto chini ya miaka mitano.
"utoaji wa vidonge vya madini chuma kwa wajawazito, uongezaji wa virutubishi kwenye unga na mafuta ya kula, lishe kwa wagonjwa wa UKIMWI.
".., pamoja na mpango wa maendeleo ya lishe kwa vijana balehe," anasisitiza na kuongeza,
"TFNC ilisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo wanahabari, sekta binafsi, viongozi wa dini, wasanii na mashirika ya kiraia.
"Kuhakikisha inaelimisha jamii, kuhimiza na kusisitiza kuhusu lishe bora, ndiyo maana tupo nanyi kwenye semina hii,".
TATIZO KIMATAIFA
Utapiamlo bado ni tatizo kubwa duniani, kuna nchi nyingi zinakabiliwa na aina zaidi ya moja ya utapiamlo.
"Takwimu zinaonesha kuwa watu zaidi ya bilioni mbili duniani wana uzito uliozidi au wana uzito mdogo.
"Pia, kuna zaidi ya watoto milioni 150 duniani wakiwa wamedumaa na kati yao milioni 58.7 wakiwa barani Afrika," anabainisha.
"Takwimu zikionesha zaidi ya watu bilioni mbili wakiwa na uzito mdogo au uliozidi, na watoto zaidi ya milioni 150 wakiwa wamedumaa, kati yao milioni 58.7 wakiwa barani Afrika," anasema Mkurugenzi wa PANITA Tumaini Mikindo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na hali hiyo kwa kiwango kikubwa, ambapo zaidi ya 30% ya watoto walio chini ya miaka mitano wamedumaa.
Kiwango hicho kimeiweka nchi katika kundi la mataifa yenye udumavu wa juu zaidi duniani.
Kwa mujibu wa Taarifa ya SUN Civil Society Alliance in Tanzania hadi kufikia mwaka 2022, watoto zaidi ya milioni 3 walikuwa wamedumaa, ikilinganishwa na milioni 2.7 mwaka 2014.
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la watoto 300,000 ndani ya kipindi cha miaka minane.
HALI HALISI TANZANIA
Takwimu za Utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS 2022) zinaonyesha kuna 30% ya watoto wamedumaa (udumavu), 3.3% wana uzito pungufu, 4% wana uzito uliozidi.
TDHS 2022 inaeleza pia 59% ya watoto walio chini ya miaka mitano wana upungufu wa damu nchini Tanzania.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa licha ya baadhi ya mikoa kupunguza viwango vya udumavu kwa zaidi ya 10%.
Bado kuna mikoa sita ambapo viwango hivyo vimeongezeka. Mikoa ya Iringa, Njombe na Rukwa imetajwa kuendelea kuwa kinara wa udumavu kitaifa.
Kwa mujibu wa SUN Alliance, utapiamlo huathiri si tu afya ya mtoto, bali pia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
"Athari kuu zinazotajwa ni pamoja na kudumaa kwa uwezo wa akili na mwili, kupungua kwa kinga ya mwili na kuongeza vifo vya watoto," anasema eneja Miradi wa PANITA Jane Msagati.
Anaongeza "[Athari nyingine ni pamoja na] gharama kubwa za matibabu kwa jamii [pia] kupungua kwa nguvu kazi na uzalishaji wa taifa, ambapo GDP hupungua hadi 2.56%.
UELEWA MDOGO TATIZO
Ripoti hiyo ya SUN Alliance inasisitiza chanzo kikuu cha hali hiyo ni pamoja na uelewa mdogo kuhusu lishe bora.
Pia, matumizi duni ya vyakula mchanganyiko licha ya uwezo mkubwa wa uzalishaji, ukosefu wa wataalamu wa lishe hasa katika ngazi ya vijiji na kata.
SUN Alliance inataja changamoto nyingine ni pamoja na uhaba wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe.
"SUN Alliance inatoa wito kwa Serikali na wadau kuongeza uwekezaji katika afua za lishe, kutoa elimu endelevu kuhusu lishe bora," anasema Mikindo.
Shirika hilo pia la kimataifa linasisitiza mataifa kuajiri wataalamu wa lishe hadi ngazi ya msingi na kuweka sera madhubuti za kuzuia na kutibu utapiamlo mapema.
Kwa sababu lishe ni msingi wa afya, elimu na maendeleo ya kiuchumi, hatua za haraka na jumuishi zinahitajika ili kuokoa kizazi kijacho dhidi ya janga hili linaloendelea kulikumba taifa kimya kimya.


Chapisha Maoni