moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Ni mtoto mwenye umri wa miaka 15 sasa, Sabrina alizaliwa na tatizo la mtindio wa ubongo, tatizo la macho pia anaishi na ugonjwa wa Siko Seli.

“Nilijifungua kabla ya wakati, alichelewa kulia na kutokulia kwake kulisababisha kupata ulemavu wa mtindio wa ubongo,”.

Simulizi hiyo inatolewa na Rehema Kitindi ambaye ni mama mzazi wa Sabrina, tulipomtembelea hivi karibuni nyumbani kwao, Mbezi Makabe nje kidogo ya Mji wa Dar es Salaam.

“Tuliruhusiwa kurudi nyumbani aliendelea vizuri ila alipofikisha umri wa miezi miwili alipata homa kali ya degedege, alilazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH],” anasema.

Anaongeza “Alipungukiwa damu, kwa mara ya pili walimpima tena na kuona ana ugonjwa wa Siko Seli.

“Baada ya miezi sita walimpima tena ili kujiridhisha na awamu hii tena walithibitisha amezaliwa na ugonjwa wa Siko Seli.

Anasema akiwa na umri wa miezi sita ndipo aligundulika ana matatizo ya macho, alikuwa haoni, ilibidi afanyiwe upasuaji na kupatiwa miwani ya tiba.

UPENDO WA MAMA

Rehema anasimulia “Akiwa na mwaka na miezi minane, mwanawe alipata ‘strock’ ikawa changamoto nyingine katika kumuhudumia.

“Lazima nimbebe na ninachoka kwa sababu ameongezeka uzito sasa. Ilifika wakati hata mazoezi ile ‘speed’ ikarudi nyuma, maendeleo yake yakarudi nyuma.

Pamoja na yote hayo mwanamama huyu shupavu anamshukuru Mungu kumpatia mtoto Sabrina kwani anampa ujasiri mpya kila siku kupambania maisha ya familia yake.

“Namshukuru Mungu ameendelea vizuri akiwa na ‘strock’, Siko Seli, na mtindio wa ubongo alionao.

“Ana uhitaji wa vitu vingi, kliniki niliendelea ila kwa kuwa anakua nikawa na maumivu ya mgongo, tuna changamoto ya usafiri.

“Sina shughuli yenye kuniingizia kipato kuweza kumuhudumia huyu mtoto kwa kila kitu, kutoka nyumbani hadi kituoni ni mbali, inabidi nimbebe mgongo.

Anaongeza “… wakati mwingine sina hela ya usfafiri wa bodaboda hiyo hali ilifika hatua naumia.

SIKUMFICHA NDANI

“Nikaendelea na kliniki ya Siko Seli, mazoezi, macho na kichwa pia,” anasema Rehema.

Anasema lakini kila alipokwenda kufanyiwa tiba ya mazoezi alipata maumivu makali mno ya mwili.

Alipofikisha umri wa miezi sita alianzishiwa dawa aina ya ya hydroxyulea ambayo kwa kiasi kikubwa imemsaidia kupunguza maumivu ya mwili yatokanayo na Siko Seli.

“Lakini changamoto sasa ikawa namna ya kumfikisha kliniki zake, amekuwa sasa na ameongezeka uzito wa mwili wake.

Anasema japokuwa mwanawe anaishi na changamoto hizo alizozaliwa nazo hakumficha ndani.

Shule alimpeleka kama watoto wengine wasio na changamoto yoyote ile na amejaliwa pia mtoto mwingine wa kiume, hata hivyo baba yao sasa ni marehemu.

“[Sabrina] sasa yupo darasa la saba, japo hajui kusoma wala kuandika lakini [nina furaha akienda shule, kwa sababu ] akiwa na wale wenzake anafurahi [naamini kuna kitu anajifunza],” anasema.

MMETUPA TABASAMU

Ukafika muda wa kukabidhi msaada wa kiti cha usaidizi [wheelchair] kwa Sabrina, ambacho ni zawadi iliyonunuliwa na rafiki wa mashujaa wa Siko Seli  The Blood Drive Network.

Taasisi hiyo yenye makao yake makuu nchini Nigeria iliwasilisha msaada huo kwa Bone and Blood Foundation na Jumuiya ya Watu wanaoishi na Siko Seli Tanzania ili kufikisha kwa familia hiyo.

Sabrina alipoketishwa katika kiti hicho, tulishuhudia furaha yake, hasa pale alipokuwa akimtazama mama yake, alicheka kwa furaha kubwa.

Kwa sababu ya changamoto aliyonayo ya mtindio wa ubongo Sabrina hawezi kuzungumza kama watoto wengine isipokuwa kushirikisha hisia zake kwa vitendo.

“Leo amefurahi mwanangu,” anasema Rehema huku naye akifurahia msaada huo wa ‘wheelchair’.

“Nashukuru [taasisi hizi] wameniletea ‘wheelchair’ imenisaidia, wamekuja kututembelea wameniletea zawdi hii itanisaidia mno.

“Kumpeleka shule, hata hospitali nilikuwa nikimbeba mgongoni miguu inaning’inia chini, nikifika hospitali nitafute ‘wheelchair’ [wakati mwingine] pale nakosa,” anasema.

Anaongeza “[Basi inabidi] uzunguke naye [kupata huduma mbalimbali ndani ya hospitali] huku unachoka.

“[Sasa] nitachukua bajaji itanipeleka mpaka Muhimbili au kwa mwendokasi [wheelchair] itanisaidia mno.

MAUMIVU YATAPUNGUA

“Hata marafiki zake pia watafurahia huwa wanakuja kumchekesha na kumfurahia watakuwa wanamsukuma atafurahi,” anasema.

Rehema anabainisha “Hata mimi maumivu ya mgongo yatapungua, nilikuwa napata shida ya kumbeba mgongoni,”.

Anasisitiza wazazi na walezi wenye watoto waliozaliwa na changamoto mbalimbali kama mwanawe Sabrina wasiwafiche ndani.

“[Ukija hapa kwetu] watoto wote wanamjua, hata uulize mama Sabrina anakaa wapi utaletwa.

“Wazazi [jamii] wanamfahamu,” anasema na kuongeza “Namshukuru Mungu na nawashukuru madaktari wa Muhimbili tangu nimejifungua wanamuhudumia kwa moyo mmoja.

“Bila wao ningemkosa ameumwa sana, tangu amezaliwa mpaka leo anakunywa kidonge katika maisha yake.

“Dkt. Soka, Zamir, kombo, madaktari wa kitengo cha mazoezi, macho wote nawashukuru sana,” anasisitiza Rehema.

TUMEFUNGUA MILANGO

Mkurugenzi wa Bone and Blood Foundation Neema Mohamed anasema imekuwa jambo la furaha kukabidhi msaada huo kwa familia ya Sabrina.

Anasema ni jambo jema kushirikiana kusaidia jamii, “Bone and Blood Foundation, kazi yetu ni kutoa elimu ya msingi kuhusu Siko Seli [kwa jamii].

“… pia kuhamasisha jamii kuchangia damu kwa hiyari ili wagonjwa wanaohitaji ikiwamo wa Siko Seli wasikose huduma,” anasema.

Anafafanua kuhusu msaada waliokabidhi kwa Sabrina, “Tunaamini kiti hiki kitamsaidia. Mtoto ana miaka 15 ameshakuwa mzito, inampelekea mama yake kupata maumivu ya kifua [na mgongo].

“TBDN [The Blood Drive Network] wamekileta na sisi tumekabidhi kitamsaidia Sabrina nyumbani na shule.

“Tumefungua milango yetu tunakaribisha taasisi zinazotamani kufanya kazi na sisi [Bone and Blood Foundation pia Jumuiya ya Watu wanaoishi na Siko Seli Tanzania] kusaidia watoto kama Sabrina,”.

Pamoja na hayo ametoa rai “Wazazi si vizuri kumficha mtoto wako kumuweka mbali na huduma za afya, sasa zipo na zipo karibu nasi.

“Mpeleke apate huduma za msingi, tunaamini katika kila kitu mzazi ukimpeleka hospitalini kupata huduma vile vile usiache kumpeleka shule apate elimu,”.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement