Na Veronica Mrema
Sekta ya afya na elimu inaendelea kupata manufaa kupitia mipango mahususi ya Merck Foundation ambayo kwa kiasi kikubwa, imedhamiria kuifikia jamii moja kwa moja kuanzia ngazi ya msingi kwa Afrika na Asia.
Merck Foundation imekuwa ikitekeleza hilo kwa ushirikiano wa karibu na wake wa marais chini ya First Ladies Initiative [MFFLI]
Mkutano wa 7 wa MFFLI umefanyika mwaka huu 2025 Dubai, Mtendaji Mkuu wa Merck Foundation, Seneta Dkt. Rasha Kelej amesema mpaka sasa wamewezesha udhamini kwa madaktari 2,270.
Amesema madaktari hao ni kutoka nchi 52 katika fani 44 za tiba, nyingi zikiwa ni maalum na zilizokuwa hazina wataalamu katika nchi husika.
Amesema programu imeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya, hasa kuanzisha wataalamu bingwa katika magonjwa kama saratani, kisukari, afya ya akili, uzazi.
"Magonjwa ya watoto, na huduma za dharura. takwimu zetu zinaeleza kila daktari aliyefadhiliwa anahudumia zaidi ya wagonjwa 1,000 katika taifa lake.
"Wakiwemo wale wanaotoa huduma maeneo ya vijijini," amesema na kuongeza "Merck Foundation inatoa udhamini wa elimu kwa wasichana zaidi ya 1,000 katika nchi 17.
"Msaada huu ni pamoja na ada, sare, vifaa vya shule, na ufuatiliaji wa maendeleo yao hadi kumaliza masomo
"Lengo ni kuzuia ndoa za utotoni na kuendeleza elimu ya wasichana kama uwekezaji wa mustakabali wa taifa," amesema.
Amesema pia wataendelea kushirikiana na wake wa marais kutekeleza mpango huo, pia bado Merck Foundation inathamini mchango wa vyombo vya habari na sanaa.
"Ni wadau muhimu katika kuleta mabadiliko ya mitazamo ya jamii kuhusu afya, ndoa za utotoni, na unyanyapaa unaohusiana na magonjwa sugu," amesema.
MFFLI ni mpango unaoshirikisha wake wa marais kutoka nchi mbalimbali kama Nigeria, Kenya, Tanzania, Ghana, Malawi, Angola, Zimbabwe, Maldives na Senegal.
Mpango huu umeleta mapinduzi ya kweli kwa kuwezesha wataalamu bingwa katika magonjwa kama saratani, kisukari, afya ya akili, na huduma za dharura.
Mke wa Rais wa Nigeria, Oluremi Tinubu, ameahidi kuuendeleza mpango huo nchini kwake kupitia ofisi yake na wizara husika.
Amesisitiza umuhimu wa elimu kwa wasichana kwa kujenga jamii zenye afya na maendeleo.
Tanzania pia imekuwa ikinufaika kwa udhamini wa madaktari walioboreshwa katika fani mbalimbali.
Pia katika kampeni za uhamasishaji wa afya ya uzazi, kupinga unyanyapaa wa ukosefu wa uwezo wa kupata mimba, na magonjwa yasiyoambukiza.
Mke wa Rais wa Kenya, Rachel Ruto, amebainisha taifa hilo nalo limepata madaktari 244 waliopata udhamini, huku 50% wakiwa wanawake.
"Wasichana 47 wanaendelea kufadhiliwa kupitia mpango wa Educating Linda.
Wake wa marais wengine kama wa Ghana, Malawi na Maldives pia wamesisitiza ushirikiano wa karibu na Merck Foundation kuendeleza huduma za afya na elimu kwa wanawake na jamii kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Merck Foundation, Profesa Dr. Frank Stangenberg-Haverkamp, amesisitiza dhamira thabiti ya wakfu huo katika kuboresha sekta ya afya na maendeleo ya kijamii.
Amefurahia mafanikio ya programu za udhamini wa madaktari na kuunga mkono juhudi za wake wa marais kama mabalozi wa mpango huu.
".., katika kuleta mabadiliko chanya na kuondoa unyanyapaa unaohusiana na magonjwa kama ukosefu wa uwezo wa kupata mimba," amesisitiza.
Mkutano huo wa MFFLI umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 8 ya Merck Foundation na 13 ya programu zake za maendeleo.
Umehudhuriwa moja kwa moja na watu milioni 8 mtandaoni. Merck Foundation inaendelea kuwekeza katika mafunzo.
Kadhalika, elimu na kampeni za uhamasishaji ili kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora za afya na fursa za elimu.
Chapisha Maoni