moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Unapoona leo hii mabadiliko ya hali ya hewa yasiyo ya kawaida, ujue basi kuna kundi kubwa la watu wanaoumia ki-afya, ki-jamii na hata ki-uchumi.

Ni hivi miaka ya zamani wazee wetu waliweza kung’amua kwa urahisi kwamba huu ni msimu wa jua la kawaida au la utosi.

Je? ni msimu wa joto la kawaida, la kati au kali, vivyo hivyo kwa upande wa mvua ni msimu wa vuli, masika na wakaweza kuishi vema kulingana na hali husika.

Kwa miaka ya karibuni, licha ya ukweli kwamba kuna maendeleo makubwa ya teknolojia na vifaa vya kisasa zaidi vya kufuatilia hali ya hewa.

Lakini binadamu tunashuhudia mabadiliko ya tabianchi yanayoleta athari kubwa katika mifumo ya hali ya hewa na ikolojia ya dunia.

“Ni hali ngumu, kwetu ukiamua kulima zako mahindi kwa mfano, mara mvua haiendelei inavyopaswa, hivyo unakosa mavuno,” anasema Karim Mwaituza Mkazi wa Kimanzichana, nje kidogo ya Mji wa Dar es Salaam.

Ripoti ya mwaka 2024 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa [TMA] inaeleza Tanzania ilikumbwa na hali ya hewa isiyo ya kawaida.

Ikiwa ni pamoja na ongezeko la joto kali na mvua nyingi hali ambayo inaashiria athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ni hali ya hatari, Ripoti ya mwaka 2024 ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani [WMO] inaeleza kipindi cha miaka kumi mfululizo [2015 - 2024] kuna rekodi ya kasi ya ongezeko la joto duniani.

WMO inatoa tahadhari kali zaidi kuhusu kasi hiyo, msisitizo ukiwekwa hali hiyo inachochea athari kubwa kwa maisha ya watu, mazingira na uchumi kwa ujumla.

Kiwango cha bahari nacho kimeendelea kuongezeka kwa kasi pia na mabadiliko hayo yanatarajiwa kuwa ya kudumu kwa mamia ya miaka ijayo.

Joto la bahari linapozidi kuongezeka si jambo jema kwani hali hiyo inazidi kuathiri mifumo ya hali ya hewa na maisha ya baharini.

‘MIILI YETU INALIA’

Makala haya yatajikita zaidi kuangazia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kundi la watu wanaoishi na ugonjwa wa Siko Seli.

“Miezi kadhaa Dar es Salaam tulishuhudia mvua ambazo si kipindi chake pia joto kali sana, mimi ninayeishi na ugonjwa wa Siko Seli inanigharimu,”.

Kauli yake Neema Mohamed ni miongoni mwa vijana nchini Tanzania wanaoishi na ugonjwa huo adimu ulio katika kundi la magonjwa ya damu na magonjwa yasiyoambukiza [NCDs].

Kila mwaka Tanzania watoto wapatao 8,000 hadi 11,000 wanazaliwa na ugonjwa huo, kulingana na tafiti zilizowahi kufanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili [MUHAS].

Kabla ya athari za mabadiliko ya tabianchi ilikuwa rahisi kwa wenye ugonjwa wa Siko Seli kujua hali fulani itatokea katika kipindi gani.

Anaongeza “Tulikuwa tunajua joto litakuja kwa kipindi fulani baada ya hapo mvua. Baada ya hapo kipindi fulani tena.

“Sisi tunavyoishi tunakuwa na 'balancing' [ili kuepuka maumivu makali ya viungo vya mwili / crisis].

“Lakini sasa ni tofauti. Kipindi cha nyuma tumeshuhudia joto kali sana ambalo limepeleka kupoteza maji mwilini,” anasema Neema.

NINI HUTOKEA?

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu wanaeleza si kila mgonjwa wa Siko Seli muda wote hupata maumivu, lakini ni pale tu kunapokuwa na vitu vinavyopelekea maumivu makali kutokea.

Kwa lugha ya kitaalamu wanaita vitu hivyo ‘triggers’ na mojawapo ya vitu hivyo ni mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mfano kunapokuwa na joto kali sana au baridi sana au pale mgonjwa wa Siko Seli anapokuwa sehemu yenye oksijeni ndogo anaweza kupata maumivu makali yasiyoelezeka.

Kitaalamu wanaita hali hiyo ‘crisis’ na inaweza kuwa ya muda mrefu na yakamsumbua mno mgonjwa husika na kulazimika kuuguzwa mara kwa mara.

Kuna athari za moja kwa moja yanapotokea mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la vipindi vya ‘crisis’ kwa mgonjwa wa Siko Seli.

M24 TANZANIA Media imefanya mahojiano ya kina na Dkt. Emmanuel Kataga kutoka Program ya  Siko Seli Program ndani ya MUHAS.

Awali anachambua namna ilivyo utofauti kati ya seli nyekundu za damu kwa mtu asiye na Siko Seli na yule mwenye ugonjwa wa Siko Seli.

Uhalisia seli nyekundu za damu za mtu asiye na ugonjwa zina umbo la duara kamili, ambazo huweza kuishi hadi wastani wa siku 90 ndipo hufa na kuzaliwa nyingine.

Lakini seli nyekundu za damu kwa mgonjwa wa Siko Seli ipo katika umbo la nusu duara mfano wa ndizi / mundu / nusu mwezi na hufa kwa wastani wa ndani ya siku 10.

MFUMO MZIMA

Anasema ule ukamilifu wa seli nyekundu ya damu katika umbo la duara huzifanya kuwa na uwezo wa kupitika kwa urahisi katika mishipa ya damu hata kama ni midogo.

“Ile mishipa ya damu ni midogo kuliko size ya seli nyekundu za damu na seli hizo zina uwezo wa kujikinga na kupita bila shida.

“Lakini sasa kwa zile za mgonjwa wa Siko Seli kwa kuwa zina shida, zinakuwa na umbo nusu duara zinapoteza ule uwezo wa kufanya zipite kirahisi kwenye mishipa ya damu,” anasema.

Seli hizo hushindwa kujikunja ili kupita kwenye mishipa ya damu na kukwama njiani, hali hiyo inapotokea sehemu husika hukosa damu na oksijeni pia.

“[Hali hiyo] ndiyo huleta maumivu. Pia hizi seli ambazo zipo kama ndizi zinakuwa zina ule uwezo wa kushikana [kunatana] zenyewe kwa zenyewe.

“[Lakini seli] za kawaida haziwezi kushikana,  kwa hiyo zinaposhikana seli za siko seli zinatengeneza mrundikano wa seli nyekundu za damu zilizokwama kwenye mshipa wa damu,”.

VIPINDI VYA HOFU

Kwa kuwa pia seli hizo hufa mapema ndani ya muda mfupi ndiyo maana wagonjwa wa Siko Seli wengi hupungukiwa damu mara kwa mara na kuhitaji huduma ya kuongezwa.

Jarome [si jina lake halisi] ameieleza M24 TANZANIA Media kwamba sasa amekuwa na vipindi vingi vya maumivu ya mwili tofauti na miaka mitatu nyuma.

“Ni hali inanipa hofu juu ya mustakabali wa maendeleo yangu kimasomo, kwa sababu nalazwa mara kwa mara,” anasema.

Anaongeza “Wananichoma sindano kupunguza maumivu, nashindwa kwenda shule, nimeelekezwa kuzingatia unywaji maji ya kutosha, mlo kamili na dawa za hydroxyulea, huwa naongezwa damu pia”.

Neema anasema kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kuna kipindi baadhi yao hushindwa kabisa kwenda shughuli zake za kila siku kujitafutia kipato au za kujumuika na makundi mengine ndani ya jamii.

"Kwa sababu ya jua kali kupita kiasi [unakuta] maeneo ninayokwenda ukisema utoke nje, jua utakalokutana nalo ukirudi kichwa kinauma, viungo vinauma na ukijiangalia unajiona kabisa huna maji.

“Tunapata maumivu ambayo kungekuwa hakuna mabadiliko ya tabianchi vingezuilika,” anasema.

Mwingine anaongeza hoja “Kutokana hiyo changamoto tumejikuta kuna ile hali kama kudhoofu ambayo imepelekea nashindwa ku-balance [niishi namna gani hasa],”.

“Kwa sababu sijui hili joto litakwenda kwa muda gani, hii hali ya mvua itakwenda kwa muda gani?.

“Kwa hiyo imetupelekea kupata msongo wa mawazo [yaani kuna kule kujiwazia na kufikiri zaidi kuhusu hali ya miili yetu.

Neema anasisitiza “Sasa hivi ukilala usiku [kuna hali ya joto kali] lakini usiku wa manane inakuja baridi [au] inakuja mvua.

“Unajikuta ulivyoingia kulala ulijua mavazi hayo yatakusaidia mpaka unaamka,”. Pale mabadiliko hayo yanapotokea huhisi baridi kali, mwili hupata vichomi, huhisi maumivu makali.

MALARIA & ‘INFECTIONS’

Changamoto nyingine ambayo hivi sasa imekuwa ikiwakabili mara kwa mara watu wenye ugonjwa wa Siko Seli ni kupata maambukizi mbalimbali ya magonjwa.

Tathmini ya hivi karibuni inaonesha wengi wamekuwa wakiripoti katika vituo mbalimbali vya afya kufuata matibabu.

Dkt. Emmanuel anasema “Upande wa Dar es Salaam [tunaona] wagonjwa wengi wanakuja kwa sababu ya kupata mara kwa mara vipindi vya maumivu na kupungukiwa damu sana.

“Kipindi cha joto wanakuwa wagonjwa wengi wale ambao hawazingatii matumizi ya maji mara kwa mara.

“Mabadiliko ya tabianchi yanakuja na kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali,” anasema.

Anataja mfano malaria, kwamba wale vimelea vya wadudu [mbu] huzaliana kwa wingi hasa sehemu yenye joto.

“Hivyo, kipindi cha joto [wagonjwa wa Siko Seli] wanapata malaria sana na tunafahamu malaria huathiri seli nyekundu za damu.

“Sasa kumbuka huyu ni mgonjwa seli zake nyekundu zinakufa mapema na akipata malaria athari inakuwa kubwa zaidi,” anabainisha.

Anasisitiza “Anapata kupungukiwa damu sana na kuhitaji kuongezwa mara kwa mara.

Anasema kwa kipindi cha miezi mitatu [kabla ya makala haya kuchapwa] kliniki ya Mwananyamala na Amana wamepokea idadi kubwa ya wagonjwa.

“Wengi wanakuja na ‘infections sign’, malaria, damu ipo chini walihitaji kuongezwa damu wengine kulazwa.

“Wengi pia wamekuja kabla ya muda wao [wa kurudi hospitali kwa tarehe waliyopewa] kwa sababu ya maudhi wanayopata,” anabainisha na kuongeza,

“Kwa mwezi katika kliniki ya mwananyamala kuna wagonjwa zaidi ya 100 wanaofika kliniki ya kawaida.

“Ukiangalia kuna kama 15 walikuja na maudhi / malalamiko ya kupata ‘crisis’, kuna walioletwa wakiwa ‘serious’.

MAHITAJI YA TIBADAMU

Wagonjwa wa Siko Seli ni kati ya wahitaji wakubwa wa tibadamu, kwani mara kwa mara hupungukiwa na hivyo kulazimu kuongezewa tena hospitalini.

Neema ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa Bone and Blood Foundation, taasisi isiyo ya kiserikali ambayo inajihusisha na uelimishaji jamii kuhusu ugonjwa huo pamoja na kuhimiza uchangiaji damu.

Ndani ya taasisi yake anashuhudia ongezeko kubwa la mahitaji ya damu kwa kundi la wagonjwa wa Siko Seli na wakati mwingine hata wahitaji watokanao na magonjwa mengine.

“[Mahitaji] ni makubwa, 2021 tulipoanza ulikuwa unajua ikifika kipindi cha Jan-March huwa kuna changamoto ya damu.

“Kwa sababu Desemba watu wengi hawachangii kwa sababu wanakuwa wapo mapumziko ya likizo, pamoja na kundi la wanafunzi ambao ni wachangiaji shule na vyuo huwa vimefungwa.

“[Hivyo] kunakuwa na uhaba wa damu, ni hali inayotambulika,” anasema lakini sasa ni tofauti kwani kuna changamoto kubwa katika benki yao ya damu, uhitaji umeongezeka mara tatu zaidi.

Anahesabu hiyo ni miongoni mwa hasara/athari za mabadiliko ya tabianchi kwani kundi la watu wanaochangia halipo na kundi la wanaohitaji damu ni kubwa.

“[Kwa mabadiliko ya hali ya hewa] wachangjia pia wanapata changamoto, unakuta kuna ambao hawana afya nzuri kuweza kuchangia, unakuta miili yao imepungukiwa maji.

“Kuna ongezeko la wahitaji wa damu, napokea simu nyingi mno, miezi mitatu sasa, changamoto ni kubwa si tu kwa wagonjwa wa Siko Seli, pia kwa wenye magonjwa mengine,” anasema.

Suala la mabadiliko ya tabianchi na athari zake kwa wagonjwa wa Siko Seli ni suala linalomgusa Mkami Wanyancha Mkazi wa Tabata, Msomi wa kozi ya Famasi katika Chuo cha Noble.

Anaishi na rafiki yake anayekabiliwa na ugonjwa huo anasema "Kuna changamoto anapitia, jua likiwa kali joto linapozidi anapoteza maji, anazidi kupata matatizo, maumivu makali.

"Huwa namshauri anywe maji ya kutosha na kuepuka safari zisizo za lazima, kwenye baridi napo huwa na changamoto namuhimiza kuvaa nguo nzito, ili asipate madhara kama kupooza mwili," anasema.

Dkt. Emmanuel anasisitiza “Kuna kipindi joto lilikuwa kali, [wagonjwa] walilalamika kupata maumivu makali, tunawapa dawa ya ‘hydroxyulea’ inasaidia kupandisha kiwango cha damu kwa mgonjwa wa Siko Seli.

“Inasaidia kuliko yule ambaye hatumii, tunawahimiza pia kuzingatia unywaji maji ya kutosha hata ikiwa hawahisi kiu, kwani yanawasaidia mno,”.

Anashauri pia wale ambao bado hawajaingia kwenye mahusiano ya ki-mapenzi na ndoa wapime vinasaba vyao kujua hali zao mapema.

“Tunajua huu ni ugonjwa wa kurithi na ukiangalia Tanzania ni nchi ya tano dunia kati ya zenye wagonwja wengi wa Siko Seli,

“Hatupo kwenye ‘position’ nzuri [hivyo] tuangalie namna ya kukinga tusiendelee kupata wagonjwa wengi wa Siko Seli.

“Tuweke huu utaratibu watu kupima mapema kabla hawajaamua kupata mtoto / watoto, kliniki ya wakina mama na wajawazito [ni vema, napo] wapime vinasaba,” anashauri.

Mkami anashauri pia jamii kuzingatia utunzaji wa mazingira ili kuepuka athari zaidi za mabadiliko ya tabianchi.

"Uharibifu wa mazingira unaweza kusababisha kuharibika kwa mazingira, o-zone layer inaharibika na kusababisha joto kuwa kali, na kuchangia athari nyingi za ki-afya ikiwamo kundi la wagonjwa wa Siko Seli.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement