Afrika Kusini
Uadilifu, ujasiri na maono ni nguzo muhimu kwa kila mwanamke anayedhamiria kuleta maendeleo na kuchangia mabadiliko chanya ndani ya jamii yake, kila siku.
Msimu wa 13 wa 'The Fabulous Woman Awards 2025' una lengo thabiti la kusherehekea safari ya mwanamke ndani ya Bara la Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa SLM Foundation ambaye pia ni mwanzilishi wa tuzo hiyo Pontsho Manzi amezungumza na M24 TANZANIA MEDIA hivi karibuni.
Amesema msimu huo wa 13 tangu kuanzishwa kwa tuzo hiyo wanakwenda kusherehekea na kutambua nguvu na thamani ya mwanamke wa Afrika.
"Kwa dunia ya sasa matokeo chanya yana nguvu zaidi kuliko vyeo, kauli mbiu yetu ya mwaka huu inasema 'Journey' [yaani safari].
"Ni kauli mbiu inayotualika si tu kuheshimu mafanikio katika hatua ya mwisho, bali kutafakari juu ya uvumilivu, maamuzi ya kishujaa na hatua za makusudi [uthubutu] katika kupambania malengo,".
Ameongeza "Ni wito wa kuchukua hatua kwa wana mabadiliko, kuanzia viongozi wanaochipukia, kuwa na uthubutu katika kuleta mabadiliko chanya, kwa kuwatambua, kuwainua na kuwasherehekea.
Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2013 na Pontsho ambaye ni mfanyabiashara na mwanahabari nchini Afrika Kusini.
Amekuwa akijikita katika kuchochea ndoto kwa vijana wa Afrika Kusini, hasa wale kutoka mazingira magumu, kwa kuwapa stadi na dira ya kuvuka vikwazo, kuanzisha biashara na kuongoza kwa moyo.
"Nina furaha kutambua wanawake wanaoleta mabadiliko na kutoa mchango mkubwa katika kutokomeza umaskini na kuwawezesha wanawake na vijana wa Afrika Kusini.
"Nasubiri kwa hamu kusikia mafanikio yao zaidi katika miezi ijayo. Tuzo hizi zimeundwa ili kuwatunuku wanawake wenye uongozi wa maadili, maono, ubunifu.
"Ubora, na mipango inayogusa jamii lengo kuu ni kuwapa wanawake wengine mfano wa kuigwa," amesema.
Tuzo za mwaka huu zinaungwa mkono kwa fahari na 'Brand South Africa', ambao dhamira yao ya kuhamasisha uzalendo, fahari ya taifa, na uwajibikaji wa raia inaendana kikamilifu.
Tuzo za mwaka 2025 zinakaribisha uteuzi katika vipengele mbalimbali, vikiangazia ubora katika nyanja tofauti kuanzia utetezi wa jamii hadi athari za kimataifa.
Vipengele 11 vya mwaka huu ni Tuzo ya Msaada wa Kibinadamu , Tuzo ya Uundaji wa Ajira, Tuzo ya Uvumilivu, Tuzo ya Usawa wa Kijinsia.
Tuzo ya Uwezeshaji wa Wanawake, Tuzo ya Mwanamke wa Ardhi, Tuzo ya Mwanamke Bora wa Mwaka na Tuzo ya Msichana Bora wa Mwaka.
Tuzo ya Mwanamke katika Sekta ya Afya, Tuzo ya Athari za Kimataifa naTuzo ya Kukomesha Ukatili wa Kijinsia.
Kwa kupitia link www.fabulouswomanawards.co.za maombi ya ushiriki kutoka kila kona ya Bara la Afrika yanapokewa hadi Juni 30, 2025 kilele cha tuzo hizo ni hapo Agosti, 2025 huko Sandton, Johannesburg.
Usiku utakaong'arisha hadithi za nguvu, maendeleo na uwezo waliojaliwa wanawake wa Afrika na hasa Afrika Kusini.
Chapisha Maoni