moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema - Afrika Kusini

Uvutaji sigara na matumizi ya bidhaa nyinginezo zitokanazo na zao la tumbaku kwa kiasi fulani huchochewa na urithi wa kijamii  au kuiga mtindo wa maisha, kizazi kimoja hadi kingine.

Ni hali inayochochewa pia na ushawishi wa makundi rika, masuala ya kijamii na historia ya kilimo cha tumbaku kwa baadhi ya maeneo.

Mtu anapovuta sigara hutoa moshi, moshi ambao wanasayansi wanatafsiri kwamba ni hatari kubwa.

Si tu kwa mtu anayevuta moja kwa moja, bali pia huathiri hadi wale walioko pembeni yake au karibu yake huyo anayevuta.

Afrika Kusini ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliana na changamoto kubwa ya matumizi ya sigara za moshi ni kama yalivyo mataifa mengine Barani Afrika, ikiwamo Tanzania.

Ndani ya Mji wa Cape Town, ni miongoni mwa madereva wa usafiri wa kukodi, miaka mingi sasa amekuwa akisafirisha abiria kutoka eneo moja hadi jingine.

Godfrey Payo hubeba abiria wa rika zote na wateja wake wakubwa siku za kazi ni wafanyakazi pamoja na wanafunzi wa sekondari na vyuo.

Mara nyingi amekuwa na nyakati ngumu ndani ya gari lake, akishuhudia waziwazi vijana hasa barobaro wakivuta sigara na kupuliza moshi bila wasiwasi wowote ule.

"Vijana wanavuta mno sigara hapa Afrika Kusini, sasa bahati mbaya kidogo, kuna wale ambao hawajali kama ndani ya gari kuna wale wasiovuta sigara, ikiwamo mimi mwenyewe si mvutaji wa sigara,".

Payo anasimulia zaidi, "Unaweza kukuta gari yangu yote inanuka moshi wa sigara humu ndani.

"Ni hatari mno kwa afya yangu najua, lakini nitafanyaje?, sina jinsi nahitaji fedha kwa ajili ya kula na kuendesha maisha yangu na familia yangu.

KASI INAYOTISHA

Kisa cha Payo na abiria wake ni simulizi walizonazo madereva wengine pia hapa Afrika Kusini, mkasa ya namna hii ipo pia kwa jamii nyinginezo Barani Afrika.

Barani Afrika, uvutaji wa sigara unaongezeka kwa kasi, kulingana na Shirika la Afya Duniani [WHO] idadi ya watu wanaovuta sigara imeongezeka kutoka Mil. 52 [mwaka 2000] hadi Mil. 66 [mwaka 2015].

Idadi hiyo huenda itaongezeka hadi kufikia Mil. 84 [mwaka 2025]. Watu wanaovuta sigara za moshi wanazidi kwa kiasi kikubwa kuongezeka Afrika.

Ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa, ongezeko hilo ni karibu 60% katika kipindi cha miaka 25 tu.

Ni janga linaloendelea kuongezeka kwa kasi Afrika, hususan katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, licha ya jitihada kubwa zinazofanyika katika utungaji wa Sheria mbalimbali za udhibiti.

Hii ni kulingana na ripoti za tafiti za kisayansi, inaelezwa licha ya mataifa mengi Afrika kuweka Sheria za kudhibiti matumizi ya bidhaa hizi, bado kuna changamoto kubwa.

Ripoti za hivi karibuni zinaonesha, tatizo hilo la uvutaji sigara bado linaendelea kushamiri sambamba na ongezeko la  visa vya watu wanaopata Magonjwa sugu Yasiyoambukiza (NCDs).

Kwa kiasi kikubwa magonjwa hayo huhusishwa na athari za uvutaji/uvutishwaji moshi utokanao na bidhaa za tumbaku ikiwamo sigara.

HOJA TATU

“Ikiwa haujawahi kuvuta sigara – usianze. Ikiwa unavuta – acha. Lakini ikiwa umeshindwa kuacha, chagua mabadiliko: tumia bidhaa mbadala zisizotoa moshi ili kujilinda na kuwalinda wengine'.

Ni kauli mbiu ya mkutano wa TECHNOVATION smoke-free 2025 ambayo ndani yake kuna hoja tatu za msingi ambazo ndizo hasa ziliwaleta pamoja wanasayansi, wanahabari na watafiti wa PMI kujadili.

Ripoti za wanasayansi zinaeleza Bara la Afrika linaendelea kubeba mzigo mzito wa madhara ya tumbaku, licha ya kuwapo kwa kampeni zilizojikita katika uelimishaji jamii.

Bado kuna jambo la ziada linapaswa kufanyika kupata suluhu /  mbinu itakayosaidia kudhibiti ongezeko la watu wanaoingia katika uvutaji sigara za moshi,

Kwa sababu bado kunaripotiwa ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza [NCDs] yanayochochewa na matumizi ya bidhaa hizo.

Je, namna gani basi Afrika itaweza kujikomboa kutoka ndani ya janga la uvutaji bidhaa za tumbaku za moshi kunusuru mamilioni ya watu wake?

“Ni wakati sasa kwa mataifa ya Afrika kubadili mwelekeo wa mikakati yao ya udhibiti wa tumbaku na kukubali mabadiliko kupitia suluhu mbadala,”.

Kauli yake Themba Mathebula, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa Philip Morris Afrika Kusini [PMSA] katika mahojiano maalum na M24 TANZANIA MEDIA.

Kwa mujibu wa Themba, kampuni hiyo inaamini matumizi ya bidhaa mbadala zisizotoa moshi kama sigara za kielektroniki (vaping).

"Sigara za kupasha joto na pakiti za nikotini, vinaweza kusaidia kupunguza madhara ya ki-afya kwa watu wazima waliokwama kwenye uraibu wa sigara za kawaida," anasema.

Anasisitiza si jambo rahisi mtu ambaye alijiingiza katika matumizi ya tumbaku na bidhaa zake za moshi kuacha mara moja.

Jambo hili linaonesha tishio kubwa la ki-afya linalozidi kuinyemelea Afrika, hali ambayo ndiyo hasa ilitusukuma PMI kuingia kazini kufanya tafiti ya kina namna gani tutasaidia kukabili janga hili.

TEKNOLOJIA

Kwa miongo mingi binadamu amekuwa akibuni nyenzo mbalimbali kumrahisishia maisha na kuyafanya yawe bora zaidi ya hapo awali.

Ubunifu ni ngao yake kuu tangu enzi za kale, kizazi hadi kizazi na teknolojia imekuwa ikikua kwa kasi na kuongezeka maradufu, miaka na miaka.

Ni mbinu inayotazamwa kwa jicho la tatu na PMI kwamba utasaidia kuleta ufumbuzi Barani Afrika.

Makamu wa Rais, Mawasiliano na Ushirikishwaji ndani ya PMI Tommaso Di Giovanni anasema dunia imepata mafanikio mengi makubwa kwa kugeukia teknolojia kwenye sekta mbalimbali.

"Afrika imekuwa ikikumbatia teknolojia pia na kupata mafanikio, leo hii tuna Wi-Fi, simu janja, benki mtandao kupitia simu.

"Tuna nishati ya jua na huduma za afya kwa njia ya masafa ya mtandao [telemedicine]. Umewahi kujiuliza maisha yangekuwa namna gani ikiwa tusingekuwa na teknolojia tulizonazo leo hii?".

Teknolojia za bidhaa zisizo na moshi ni chachu muhimu katika kuleta mabadiliko ya haraka.”

PICHA HALISI

PMI ni moja ya makampuni yanayoongoza katika kuwekeza kwenye uvumbuzi wa bidhaa zisizo na moshi, ikiwa ni pamoja na mfumo wa IQOS. 

Bidhaa hizo za kiteknolojia zisizotoa moshi sasa inaipatia zaidi ya 40% ya mapato yake kimataifa.

Ni jambo linaloonesha mwenendo wa dunia kuelekea kupunguza uvutaji sigara za kawaida zinazotoa moshi na kuathiri afya ya jamii kubwa zaidi.

Tomasso anasisitiza "Katika juhudi za kupunguza madhara ya tumbaku, Sweden imefanikiwa kushusha kiwango cha uvutaji sigara hadi chini ya 5%.

"Sasa inatambulika kama taifa la kwanza barani Ulaya kuwa 'Smoke-Free'. Uingereza inahimiza matumizi ya e-cigarettes kama suluhisho kwa watu waliokwama kuacha sigara.

"Marekani, kupitia FDA, imeidhinisha baadhi ya bidhaa mbadala kama njia salama zaidi kwa wavutaji watu wazima," anasema.

AFRIKA IPO WAPI?

Licha ya mafanikio hayo, mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Tanzania bado hayajatoa ruhusa ikiwamo  kutunga sera mahsusi kuhusu bidhaa mbadala zisizo na moshi.

Afrika bado haijaweka wazi tofauti kati ya sigara za moshi na bidhaa zisizo na moshi. Nchi nyingi bado hazijatoa mwongozo rasmi wa matumizi ya bidhaa mbadala.

Ni changamoto inayosababisha wavutaji kukosa chaguo salama la kupunguza madhara [Tobacco Harm Reduction].

“Tunahitaji sera nzuri zinazolinda vijana lakini pia kuwasaidia watu wazima walio katika uraibu wa sigara kupata taarifa sahihi na chaguo mbadala,” anasisitiza Themba.

Kwa sababu ni hali ambayo imekuwa ikiongeza tishio la athari za ki-afya kwa mamilioni ya watu kwa siku zijazo Barani Afrika.

NCDs kama vile saratani ya mapafu, magonjwa ya moyo, na matatizo ya kupumua bado ni mzigo mkubwa.

Licha ya juhudi za mataifa mengi katika ukanda huo kutunga sheria za udhibiti wa tumbaku, changamoto hii bado inazidi kuenea, huku idadi ya wavutaji sigara ikiendelea kuongezeka kwa kiwango kinachotia wasiwasi.

SAYANSI INASEMAJE?

Kampuni ya Philip Morris International (PMI) imewekeza zaidi ya dola bilioni 14 katika utafiti na maendeleo ya bidhaa zisizo na moshi. 

Dkt. Buhle Binta Mkuu wa Masuala ya Utafiti, Kusini mwa Jangwa la Sahara -PMI anasema “Bidhaa hizi si kwa ajili ya vijana au watoto, bali kwa watu wazima waliokwama kwenye uraibu wa sigara za kawaida.”

Anasema PMI imeamua kupunguza kiwango cha nikotini hadi chini ya miligramu 12 kwa kila bidhaa yake [sigara] moja.

"Ni sehemu ya uwajibikaji wa kijamii, wakati kiwango cha juu kilichopendekezwa na BfR cha Ujerumani ni miligramu 16.6," anabainisha.

Anaongeza "Ni muhimu Serikali zetu ziache kutumia sera za zamani na zianze kufuata ushahidi wa kisayansi. Tunapambana kuokoa maisha ya mamilioni ya Waafrika.

Tommaso anasisitiza sasa ni wakati wa Afrika kuchukua hatua kama hiyo katika vita dhidi ya sigara. 

"Tunahitaji sera zinazotofautisha kati ya sigara za kawaida na bidhaa mbadala. Sera bora, kodi rafiki, na elimu ya kisayansi vinaweza kuleta mabadiliko makubwa,”.

PMI imeshawekeza zaidi ya dola bilioni 14 katika tafiti, uzalishaji, na usambazaji wa bidhaa zisizo na moshi, huku zaidi ya 40% ya mapato yake yakitokana na bidhaa hizo.

Ingawa mjadala kuhusu matumizi ya bidhaa hizi bado unaendelea miongoni mwa wataalamu wa afya, juhudi za kutafuta suluhisho mbadala zinazidi kuungwa mkono sehemu kubwa duniani.

Themba anasisitiza "Tunahimiza matumizi ya bidhaa mbadala zisizo na moshi kama njia ya kupunguza madhara ya ki-afya.

"Tunataka kila sigara ya kawaida ibadilishwe na bidhaa bora mbadala kama vile sigara za ki-elektroniki (vaping) na vifaa vya kupasha joto tumbaku.

Themba anatolea mfano halisi, "Katika kipindi cha janga la COVID-19, Afrika Kusini ilipiga marufuku ya bidhaa za tumbaku.

"Hali ile ilisababisha kuongezeka kwa biashara haramu ya tumbaku na bidhaa zake kutoka 30% hadi 60%. Hali iliyoweka afya za watu wengi hatarini zaidi.

Hali hiyo ilionesha kwamba, marufuku pekee hazitoshi kuwasaidia watu kuacha kuvuta sigara, bali zinachochea matumizi ya bidhaa haramu zisizodhibitiwa.

Themba anabainisha "Afrika Kusini iliamua kuwa miongoni mwa mataifa machache yaliyoanza kuchukua hatua za wazi, za mapema.

"Kwa kushirikiana na sekta binafsi iliamua kuweka sera zinazozingatia afya ya umma, ikiwamo pia kuruhusu bidhaa za tumbaku zisizo na moshi," anasema.

'SERA ZITASAIDIA'

Payo anasema ni kweli Afrika Kusini imeruhusu bidhaa hizo lakini yeye kama mzazi pia anashauri ni muhimu kuongeza udhibiti wa bidhaa hizo mpya za kiteknolojia hasa kwa kundi la vijana wadogo.

"Hivi karibuni, mambo yamebadilika, ni kweli vijana hawavuti hadharani sigara zinazotoa moshi, ila hizo bidhaa mpya za kiteknolojia," anasema.

Anaongeza "Lakini naona pia kuna watoto nao wanaanza kuvuta, sasa hapa nitoe angalizo kama mzazi, tusiache watoto wakaingia huku.

"Unajua, hii ya vape ni kitu kipya, nia ni njema kuokoa mamilioni ya watu ila tusijikute tunatengeneza uraibu mpya, ziwekwe sera bora za kudhibiti ili kulinda kizazi kijacho pia," anasema.

Anasisitiza "Juhudi ambazo mashirika ya afya wamefanya kuhusu sigara, angalia ni muda gani imechukua kuweza kuzuia uvutaji wa sigara hadharani. 

"Ilichukua miaka mingi sana, miaka mingi mno. Sasa hivi, mtu anaweza kutoka na kuanza kuvuta vape hadharani bila wasiwasi. Lakini kwa vape, ingawa ni madhubuti na vina uraibu.

Payo anabainisha "Bado hakuna matangazo ya kutosha yanayofanywa kuelezea umma kuwa vape pia vina uraibu. 

Bulhe anasema kwamba PMI inalitambua hilo na ndiyo maana imekuwa ikiweka msisitizo zaidi kwa Serikali kushirikiana na watafiti ili kuweka mbiu bora zaidi ya udhibiti.

"Kama tunataka kusaidia watu wazima kubadilika, tunahitaji ‘smart regulation’ kanuni bora zinazolinda vijana huku zikiruhusu taarifa sahihi kufikia watu wazima," anasisitiza Bulhe. 

Anafafanua ".., katika harakati za kuweka viwango vya usalama, taasisi ya BfR nchini Ujerumani imependekeza kiwango cha juu cha nikotini kisizidi miligramu 16.6 kwa kopo moja. PMI.

"Kwa upande wake, imeamua kupunguza hadi chini ya miligramu 12 kama hatua ya uwajibikaji.

KIGINGI KILIPO

Licha ya uwepo wa teknolojia hizi, kumekuwa na uvumi mwingi dhidi ya bidhaa hizo mpya hasa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari.

"Watu wazima wanaovuta sigara hawapati taarifa sahihi kuhusu bidhaa hizi mbadala, hali ambayo inawanyima uwezo wa kufanya maamuzi ya kiafya yanayofaa,” anasema Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Haki ya Mteja - PMI Yahel Ossowski.

Anasisistiza taarifa za upotoshaji ni kikwazo kikubwa kwa mapambano ya kupunguza uvutaji.

"Bidhaa hizi si kwa ajili ya watoto wala vijana, bali kwa watu wazima waliokwama katika uraibu wa sigara za kawaida," anasisitiza Yahel. 

Yahel anasema wameona upo umuhimu wa kutumia Akili Mnemba [AI] kusaidia wananchi kuchambua tofauti kati ya propaganda na ushahidi wa kisayansi. 

“AI inaweza kusaidia jamii kupata taarifa zilizochujwa na kuthibitishwa kitaalamu badala ya kutegemea uvumi,” anasema. 

“Kwa Tanzania, huu ni wakati sahihi wa kuanza mjadala wa wazi juu ya uwezekano wa kupunguza madhara ya tumbaku kupitia bidhaa mbadala,” anashauri.

Anasema ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wanahabari na wataalamu wa afya unaweza kusaidia katika kuunda sera zinazozingatia ushahidi badala ya hofu.

“Vyombo vya habari pia vina wajibu mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu tofauti ya bidhaa zenye moshi na zisizo na moshi. 

“Kwa lengo la kulinda afya ya umma bila kuendeleza matumizi haramu au yasiyo sahihi, katika ulimwengu unaozidi kuelekea kwenye mabadiliko chanya kwa afya ya jamii. 

Anaongeza “Afrika haiwezi kubaki nyuma, kama tulivyojadili mapema asubuhi, sasa ni wakati wa kuchukua hatua. 

“Wavutaji sigara watu wazima wanahitaji chaguo. Na chaguo bora ni kile kinachopunguza madhara yao ya kiafya,”.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement