Na Veronica Mrema
Upo mkutano mkubwa wa kwanza wa kihistoria katika sekta ya
afya unaokwenda kufanyika kwa siku mbili [Oktoba 29 na 30, 2024] ndani ya Jiji la Dar
es Salaam.
Ni mkutano wa 11 wa Merck Foundation ambapo hii ni taasisi
kubwa duniani waanzilishi wake ni wa huko Ujerumani, makao yake makuu yakiwa
Dubai.
Taasisi hiyo imejikita kwa miaka mingi kuangazia afya ya
mwanamke, kupiga vita vitendo vya ukatili na unyanyapaa kwa waliokosa watoto
pamoja na kuhimiza elimu kwa mtoto wa kike.
Hivi sasa ikizidi kutanua mbawa zake kuangazia pia masuala
ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo Kisukari na Shinikizo la damu.
Ni magonjwa yanayoathiri idadi kubwa ya watu hivi sasa
ulimwenguni, Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu na hii
ni hatua kubwa katika sekta ya afya.
Wageni kutoka nchi za Bara la Afrika na Asia wapatao 600
wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wakiwamo wenza wa Marais kutoka nchi 15 za
Afrika.
Kundi jingine ni la wataalamu wa afya hususan madaktari
wakiwamo wale wa upandikizaji mimba.
Ujio huo unahusisha pia kundi la waandishi wa habari
waliojikita sekta ya afya ambao ni mabalozi wa Taasisi hiyo kutoka nchi
mbalimbali nao watashiriki.
KWANINI
TANZANIA?
Hili ni swali ambalo bila shaka unajiuliza, kwamba kwanini
Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa wa kimataifa kwa
sekta ya afya. Makala haya yanakujuza kwa kina.
“Huu mkutano [ili ufanyike nchini husika, Merck Foundation] huwa mara nyingi wanangalia vingi,”.
Yanaelezwa hayo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga.
Anaongeza “Kubwa [ni] jinsi nchi yako inavyokabiliana na
changamoto mbalimbali aambazo zinaikumba jamii katika masuala ya afya na je
umepiga hatua gani kuzitatua,”.
“Kwa hiyo tunakuja, kwa sababu ni kama kikao kazi [washiriki]
wanaangalia zaidi wawekeze zaidi kwenye masuala yapi [kuboresha zaidi jitihada
na huduma za afya kwa mataifa husika].
MFANO
WA KUIGWA
Mtendaji Mkuu wa Merck Foundation Seneta Dkt. Rasha Kelej
katika mkutano wake wa awali na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam hivi
karibuni,
Anasema wameichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mwaka huu
kwani ni mfano mzuri wa kuigwa kutokana na namna ilivyofanya uwekezaji mkubwa
katika sekta ya afya.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
na ndiye ‘atakayebariki’ mkutano huo.
Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Mama Maria Mwinyi yeye atawakilisha upande wa Tanzania katika
mkutano huo.
“Washiriki wengine ni
wataalamu na watafiti nguli katika sekta ya afya, wenza wa marais, watunga sera
na waandishi wa habari,” anasema na kuongeza,
"Tumeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu kwani
tumevutiwa mno na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya
afya," anasema.
Dkt. Rasha anasisitiza “Uongozi wa Dkt. Samia ni mfano wa kuigwa,
ndiyo maana hatujasita kuja Tanzania,”.
Ndani ya mkutano huo kutakuwa na makongamano
yatakayoendelea ambapo wataalamu wote watajadiliana kwa pamoja na kupeana ujuzi
na maarifa mapya.
Balozi Mindi anasisitiza “[Makongamano hayo] yanalenga kutoa
elimu kwa madaktari, kwa hiyo kuna madaktari wa Tanzania wamejiandikisha tayari
watashiriki.
“Wenza wa marais ndiyo wanaubeba huu mkutano, tayari
wamewasili wengi nchini, walimuomba [Rais Samia mkutano huo uwe Tanzania] kwa
sababu ya jitihada ambazo tumepiga.
“.., katika suala zima la afya na magonjwa ambayo yanaikabili
jamii kwenye upande wa afya mama na mtoto,” anasisitiza na kuongeza.
“Kwa ile jihitada waliomba kwamba nchi yako ni mfano kwa
hiyo tukifika tunaweza kupata nyenzo za kuwapa wenza wengine nini cha kufanya
kwenye nchi zao.
“Rais
alilidhia kwa sababu ni katika harakati za kujifunza na kuwafundisha wengine,
wakija madaktari wako wakifundihwa inasaidia kutatu changamoto nyingine ambazo
pengine siye hatujafikia.
Anaongeza
“[Mada zilizochaguliwa kujadiliwa ni kuhusu] afya ya mama, ugonjwa wa saratani,
ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu na mipango ya maendeleo ya kujengewa
uwezo.
“.., wanaangalia Tanzania mmefikia wapi na tuweke nguvu
katika maeneo gani. Tunatazamia watu 600 kutoka nje wanakuja Tanzania kwa ajili
ya kushiriki mkutano huo,”.
Anasema pia kuna Watanzania waliojiandikisha hivyo idadi
hiyo itaongezeka na kwamba kuna watu kati ya 400 na 500 ambao watadhuhuria kwa
njia ya mtandao.
USHIRIKIANO
MADHUBUTI
Kwa miaka miaka mingi Merck Foundation imekuwa ikishirikiana bega
kwa bega na Tanzania hasa katika kufadhili masomo kwa wataalamu wa sekta ya
afya.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
Dkt. Dorothy Gwajima anasema,
“Mawaziri wa afya, jinsia, mawasiliano, elimu, ustawi wa jamii
kutoka nchi zilizoalikwa watashiriki mkutano huu,”.
Anasema mkutano huo utafungua njia ya utekelezaji wa ahadi mpya
zitakazotolewa na wenza wa marais, mawaziri na timu ya Merck Foundation.
"Ni katika kuhakikisha upatikanaji wa suluhu bora na usawa wa
huduma za afya na watu wa Afrika hasa kutoka nchi zitakazokuwepo katika mkutano
huu, ikiwamo Tanzania.
Anasema utatumika kama jukwaa la kuchukua hatua mahususi katika
kushughulikia unyanyapaa na mtazamo wa kijamii wa utasa.
"Kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi salama
iliyodhibitiwa na yenye ufanisi kwa wanawake na wasichana," anabainisha
Waziri Gwajima.
Anasema washiriki watanufaika na maarifa na uzoefu unaotolewa na
wataalamu mbalimbali na watafiti ambao watazungumza kwa kina mada
zitakazowasilishwa.
“Nchi zingine ambazo mkutano wa namna hiyo umefanyika kwa awamu
zilizopita ni pamoja na Ujerumani, Kenya, Cote d'Ivoire, Misri na Mauritius.
“Mkutano huo pia umekwisha fanyika katika nchi za Senegal, Ghana,
Zambia, Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na India,” anabainisha.
SEKTA
YA UCHUMI
Balozi Mindi anabainisha mikutano mikubwa kama huo husaidia
kuchochea uchumi na kuongeza fedha za kigeni ikiwamo Dola.
“Kwa mfano [ikiwa mtu mmoja atatumia kiasi cha] Dola 1000 [ukipiga
hesabu kwa washiriki] 600 [maana yake ni wastani wa] Dola 600,000 [watatumia].
“[Hii ni sawa na kiasi cha] Tsh. Bil. 1au 2 na hiyo ni
makisio ya [matumizi kwa] ‘minmum’ [lakini ikiwa mtu] ataamua ku-spend zaidi ya
hapo,
Anaongeza “…, nadhani kwa wakati mmoja itachechemua uchumi
wetu na watu wadogo wadogo eneo la Dar es Salaam ambako [mkutano] utafanyika.
SEKTA
YA HABARI
Siku ya pili ya mkutano huo ni mahususi pia kwa kundi la
waandishi wa habari ambapo watakuwa na semina maalum ya kuwajengea uwezo wa
umahiri katika habari za afya.
“Wametoa kipaumbele kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa
habari ambao wamejikita kwenye kuandika habari za afya,” anasisitiza Balozi
Minde.
Anaongeza “[Merck Foundation] wanasema kama mwandishi wa habari hajajua vizuri
jinsi ya kuandika, kwa mfano magonjwa sugu, uzazi.
“Mwandishi
ajue jinsi ya kuiandikia, Tanzania wametoa fursa waandishi kujiunga
[kushiriki],”.
Anasema hii ni tofauti kabisa na mikutano na makongamano
mengine ambapo kundi hili hufika tu kuripoti habari na kuondoka.
Anasema hatua ya kuwapo kwa semina hiyo kwa waandishi itawajengea uwezo zaidi kuboresha maudhui ya afya popote watakapokwenda kukusanya taarifa zao ili kusaidia jamii na Taifa.
KISWAHILI/TEKNOLOJIA Ai
Ai hii ni miongoni mwa mada ambazo kwa mwaka huu pia itawasilishwa katika semina hiyo kwa waandishi wa habari.
"Ni eneo mojawapo ambalo tumeliangalia na kuona linafaa kwa waandishi kupatiwa mafunzo maalum," anasema Seneta Rasha.
Anabainisha Merck Foundation pia kuanzia sasa itaanza kujumuisha lugha adhimu ya kiswahili katika nyenzo zake za kupeleka ujumbe wa afya kwa jamii ya Watanzania.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Taasisi hiyo kutumia lugha ya kiswahili ambapo awali imekuwa ikitumia lugha nyinginezo ikiwamo kingereza na kifaransa.
"Mimi mwenyewe pia nimeanza kujifunza maneno ya kiswahili, kwa mfano najua kutamka neno saratani hii inamaanisha cancer kwa lugha ya kingereza," anasema.
UTALII TIBA/MIKUTANO
Hili ni eneo jingine ambalo Tanzania itanufaika nalo,
utalii wa matibabu na utalii wa mikutano ambapo haya ni mazao mapya ya utalii.
“Tuendelee kuvutia, kwa sababu wanapokuja madaktari wakiona
kwamba tuna uwezo tumeendelea basi mkutano mwingine wa madaktari wa taasisi
nyingine wanaweza pia wakachagua.
Anasisitiza hayo Balozi Mindi na kuongeza, “.., Tanzania [Dar es Salaam] kwa sababu ya ukaribu wake na Zanzibar.
"Lakini pia wataona tuna maeneo mengine mbalimbali ya
kuwawezesha kufanya malazi ya hawa washiriki wa mkutano.
“Ambapo kwa nchi nyingine wanakuwa wanakwama kwenye maeneo
hayo,” anabainisha.
Anatoa rai kwa balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali
kuendelea kuvutia taasisi na mashirika ili zije nchini kufanya mikutano kama
hiyo kama ulivyofanya Balozi wa Falme za Kiarabu.
“Balozi [wa Tanzania katika Falme za Kiarabu] ameshiriki
kwa kiasi kikubwa [kuhimiza ujio wa mkutano huo] kwa sababu ni mojawapo ya
maeneo ambayo tunayapigia chapuo katika balozi zetu.
Anaongeza “Ukienda huko nchi tunaangalia jinsi ya kuvutia
mikutano hii ya kimataifa,
“Tuendelee kushirikiana kuvutia uwekezaji, utalii wa mikutano
pia kama sekta binafsi tuendelee kushirikiana bega kwa bega kuhimiza waandaaji
waweze kuja Tanzania,” anatoa rai.
JAMII
KWA UJUMLA
Balozi Mindi anasema mkutano huo ni wenye tija kwa Taifa
kwani madaktari watapata ujuzi na maarifa mapya ambapo watakaporejea kwenye
vituo vyao vya kazi watayatumia kuboresha huduma.
“Elimu watakayopata watakwenda kuongeza jitihada kwenye
eneo la kazi,” anasisitiza.
Anasema tayari Wenza wa Marais 15 wameshawasili na kila mmoja
amefika na wajumbe wake.
“Waziri wake wa afya au maendeleo ya jamii, elimu au
mawasiliano inategemea [jinsi] wizara zao zimejipangaje,” anabainisha.
Anasema pamoja na hayo, baada ya muda fulani Tanzania
itafanya tathmini ya kina kuangalia namna ilivyonufaika kwa ujumla kwa mkutano
huo utakaofanyika kwa siku hizo mbili.
Baadhi ya nchi ambazo wenza wa marais wake wanashiriki ni
pamoja na Botwasana Burundi, Zambia, Zimbabwe, Ghana Kenya, Sao Tome, Cape
Verde, Afrika ya Kati na Mwenyeji Tanzania.


Chapisha Maoni