Na Veronica Mrema
Tanzania ya mwaka 2050 itakuwa na zaidi ya watu milioni 118, kwa makadirio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku vijana wakitarajiwa kuwa zaidi ya nusu ya idadi ya watu.
Ni kizazi kinachotarajiwa kuwa nguvu kazi ya Taifa, wabunifu, wataalamu, wazalishaji na viongozi wa Tanzania ya baadaye.
Lakini wakati Taifa likiandaa mipango ya miaka 25 ijayo, kuna swali moja la afya linalohitaji kuulizwa sasa, watoto na vijana ambao tayari wanaishi na Ugonjwa wa Kisukari watafikaje mwaka 2050?
Swali hilo si la mbali kama unavyofikiri! Linaanzia kwa mtoto anayekunywa maji mengi kuliko kawaida, anayekwenda kukojoa mara kwa mara, anayepungua uzito na kuanza kupoteza nguvu mwilini.
Kwa mzazi, dalili hizi zinaweza kuonekana kama uchovu, mtoto kutokula vizuri au mabadiliko ya kawaida ya ukuaji.
Lakini zinaweza pia kuwa dalili za ugonjwa wa kisukari. Na kwa baadhi ya watoto, kuchelewa kuzitambua kunaweza kumfikisha hospitalini akiwa katika hali ya hatari zaidi.
KLINIKI MUHIMBILI
M24 TANZANIA imefanya mahojiano maalum Daktari Bingwa wa Watoto Mbobezi wa Magonjwa ya Kisukari na Homoni, Dkt. Monica Appollo.
Dkt. Monica pia ni Mkuu wa Kitengo cha Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH].
"90% ya watoto wanaogundulika kuwa na kisukari Muhimbili hufikishwa wakiwa katika hali mbaya, wengi wakihitaji kulazwa katika chumba cha uangalizi maalumu," anabainisha.
Baadhi yao hufika wakiwa na hali inayojulikana kitabibu kama DKA [diabetic ketoacidosis], hali hatari inayoweza kutokea mwili unapokosa insulin ya kutosha.
Hapo ndipo tatizo linapoonekana kwa ukubwa mwingine. Sio tu mtoto kuwa na kisukari.
Ni mtoto kufika hospitalini akiwa tayari katika hali ambayo ingeweza kuzuilika kama ugonjwa mwilini mwake, ungetambuliwa mapema.
Katika kliniki ya watoto ya Muhimbili, Dkt. Appollo anasema takriban watoto 300 huonekana ndani ya kipindi cha miezi mitatu, bila kuhesabu wale wanaorudia kliniki.
Takwimu hizi zinaweka watoto katika kiini cha mjadala ambao mara nyingi huangaliwa zaidi kwa upande wa watu wazima.
KISUKARI AINA YA KWANZA
Dkt. Appollo anasema kisukari aina ya kwanza huwapata zaidi watoto na vijana, ingawa kinaweza kutokea katika umri wowote.
Lakini tofauti na dhana iliyozoeleka ndani ya jamii, mtoto kupata kisukari aina ya kwanza si kwa sababu amekula pipi nyingi, kunywa soda au kula sukari nyingi.
“Mara nyingi kwa watoto inatokana na autoimmune, au kuharibika kwa kinga zao wenyewe,” anasema.
Katika hali hiyo, mfumo wa kinga ya mwili hushambulia seli zinazozalisha insulin, na hivyo mwili kushindwa kuzalisha insulin ya kutosha.
Watafiti hadi leo wanasema hakuna njia ya kawaida iliyothibitika kuzuia aina hii ya kisukari.
Kinachoweza kubadilisha maisha ya mtoto ni utambuzi wa mapema, upatikanaji wa insulin, elimu sahihi na ufuatiliaji wa matibabu.
“Ujumbe kwa jamii ni kwamba hakuna mtoto anayepaswa kupoteza maisha kwa kuchelewa kugundulika au kukosa insulin. Insulin kwao ni maisha,” anasisitiza Dkt. Appollo.
Mtoto wa leo ndiye nguvu kazi ya 2050.
Dira hiyo inalenga Tanzania yenye ustawi na kuboresha ubora wa maisha ya watu, ikiwamo kuongeza umri wa kuishi hadi angalau miaka 75 na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.
Katika mpango wa utekelezaji wa muda mrefu wa Dira hiyo, Tanzania imeweka pia utambuzi wa mapema na kinga ya magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo magonjwa ya moyo, kisukari na saratani.
Pamoja na programu za lishe bora na kupunguza magonjwa yanayohusiana na unene. Kwa hiyo, mtoto mwenye kisukari si suala la leo pekee.
Ni sehemu ya swali kuhusu afya ya kizazi kinachotarajiwa kuijenga Tanzania ya 2050. Mtoto anayehitaji insulin leo ndiye kijana atakayekuwa sehemu ya nguvu kazi ya taifa kesho.
Na kama Dira 2050 inahitaji kizazi chenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo, basi afya ya kizazi hicho haiwezi kusubiri mpaka wafikie utu uzima.
Dalili zinapopuuzwa, mtoto analipa gharama
Kwa mzazi, dalili za mwanzo zinaweza kuonekana ndogo. Kiu kali. Kukojoa mara kwa mara. Kupungua uzito. Uchovu na kupungua nguvu.
Lakini dalili hizi zikijitokeza, Dkt. Appollo anasisitiza umuhimu wa mtoto kufanyiwa uchunguzi. Kwa sababu mtoto mwenye kisukari aina ya kwanza anapokosa insulin, hali yake inaweza kubadilika kwa haraka.
Na hapo ndipo baadhi yao huishia Muhimbili wakiwa tayari katika hali mbaya. Changamoto hiyo inaonyesha kwamba elimu ya kisukari haiwezi kuwa ujumbe wa siku moja kwa mwaka.
Inahitaji mzazi, mwalimu, mhudumu wa afya na jamii kwa ujumla kujua kwamba kisukari kinaweza kuanza utotoni.
Vijana nao wanaingia kwenye picha. Lakini hadithi ya kisukari kwa watoto na vijana haishii kwenye aina ya kwanza.
Dkt. Appollo anasema vijana wengi wanaanza pia kuonekana na kisukari aina ya pili, aina ambayo kwa muda mrefu ilihusishwa zaidi na watu wazima.
Tofauti na aina ya kwanza, ambapo mchakato wa kinga ya mwili una nafasi kubwa, kwa kisukari aina ya pili mtindo wa maisha unaweza kuwa miongoni mwa mambo yanayoongeza hatari.
“Vijana wengi wanakuja na aina ya pili kwa sababu ya mtindo mbovu wa maisha,” anasema.
Anataja kutofanya mazoezi, matumizi ya pombe, uvutaji wa sigara na shisha, ulaji usiofaa na kuongezeka kwa unene kupita kiasi.
Hivyo, ndani ya kundi la watoto na vijana kuna hadithi mbili tofauti. Kuna mtoto ambaye mwili wake unashindwa kuzalisha insulin kwa sababu ya mchakato wa kinga ya mwili.
Na kuna kijana ambaye mazingira ya maisha yanaweza kumweka katika hatari ya kisukari aina ya pili.
Kizazi kisichotembea kama zamani
Kwa Dkt. Appollo, mabadiliko ya maisha yanaonekana katika namna watoto na vijana wanavyoshughulisha miili yao.
Kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, kucheza na kufanya shughuli nyingine za kila siku kulikuwa sehemu ya maisha ya kawaida. Leo, shughuli hizo zimepungua.
“Zamani walikuwa wanafanya mazoezi, hata kilomita tano kwenda na kurudi shule tuliona kawaida. Siku hizi kushughulisha mwili kumepungua,” anasema.
Mabadiliko hayo yanaenda sambamba na mabadiliko ya ulaji. Baadhi ya watu wanakula vyakula vyenye wanga mwingi huku mboga zikiwa chache.
Mfano ni mtu anayekula ugali mwingi na mboga kidogo. Kwa Dkt. Appollo, suluhisho si kuacha kundi moja la chakula, bali kuwa na mlo wenye uwiano na kuhakikisha mwili unapata shughuli.
Na mazoezi si lazima yaanze gym. Kutembea, kucheza na kushiriki shughuli zinazoufanya mwili ufanye kazi ni sehemu ya maisha yenye afya.
Tatizo la kisukari ni kubwa kuliko tunavyoliona
Wakati watoto na vijana wakianza kuonekana katika picha ya kisukari, Tanzania pia inakabiliwa na changamoto kubwa ya watu ambao wanaishi na ugonjwa huo bila kujua.
Kwa mujibu wa Tanzania STEPS Survey 2023, zaidi ya asilimia 72 ya watu waliogundulika kuwa na kisukari wakati wa utafiti hawakuwa wanajua kwamba wanaishi na ugonjwa huo.
Dkt. Appollo pia anasema zaidi ya asilimia 30 ya wanawake wana unene uliopitiliza, hali inayoweza kuongeza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza, ikiwamo kisukari.
Hii inaifanya elimu, uchunguzi na kinga kuwa muhimu kabla mtu hajaanza kuishi na madhara ya ugonjwa.
Uchunguzi unapelekwa hadi jamii
Dkt. Recho anasema Serikali imekuwa ikichukua hatua za kuongeza elimu na uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza hadi ngazi ya jamii.
Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs) wamepewa pia nafasi katika elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza.
Hivyo, mtu anapofika kupata huduma anaweza kupimwa ili kujua kama ana kisukari au la.
Lengo ni kutambua ugonjwa mapema na kuanza hatua za matibabu na udhibiti kabla haujaleta madhara makubwa.
2050 INAANZA LEO
Tanzania inaweza kuwa na watu zaidi ya milioni 118 ifikapo 2050, huku vijana wakitarajiwa kuwa zaidi ya nusu ya idadi ya watu.
Tume ya Taifa ya Mipango inawataja vijana kama nguvu kazi muhimu katika kufanikisha Dira hiyo. Lakini nguvu kazi haiishii kwenye idadi. Inahitaji afya.
Mtoto mwenye kisukari anayepata insulin kwa wakati, anayefuatiliwa kliniki na anayepata elimu sahihi ana nafasi ya kukua, kusoma, kufanya kazi na kushiriki kikamilifu katika taifa la 2050.
Kijana anayefundishwa mapema kuhusu ulaji unaofaa, shughuli za mwili na hatari zinazohusishwa na matumizi ya pombe na sigara ana nafasi ya kupunguza baadhi ya vihatarishi vya kisukari aina ya pili.
Kwa hiyo, Dira 2050 haiwezi kuangaliwa kwa majengo, uchumi, teknolojia na ajira pekee. Inaangaliwa pia kwa mtoto anayekunywa maji mengi leo. Kwa kijana anayekosa shughuli za mwili leo.
Na kwa mtoto ambaye maisha yake yanategemea insulin. Kwa sababu Tanzania inayotaka kuwa na kizazi chenye afya mwaka 2050, inapaswa kuanza kukilinda kizazi hicho leo.
Na kwa mtoto mwenye kisukari aina ya kwanza, mwanzo wa ulinzi huo unaweza kuwa rahisi lakini wenye uzito mkubwa:
Kumtambua mapema. Kumsaidia kupata insulin. Na kutomruhusu ugonjwa umnyang'anye utoto wake.


Chapisha Maoni