moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Jamii imehimizwa kuzingatia mtindo bora wa maisha, kufanya mazoezi na kula mlo wenye uwiano ili kupunguza hatari ya kisukari na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Rai hiyo imetolewa katika matembezi yaliyoandaliwa na Tanzania Non-Communicable Diseases Alliance [TANCDA], Siku ya Kisukari Duniani 14, Nov. 2026.

Lengo ikiwa kuongeza uelewa kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na umuhimu wa uchunguzi wa afya.

Dkt. Recho anasema Serikali imekuwa ikiimarisha elimu na uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza hadi ngazi ya jamii kupitia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii [CHWs].

Anasema wahudumu hao wamepewa mafunzo ya kushughulikia pia magonjwa yasiyoambukiza, ikiwamo kisukari.

“Mtu anapofika kwa huduma anaweza kupimwa ili kujua kama ana kisukari au la,” anasema Dkt. Recho, akisisitiza umuhimu wa mtu kujua hali yake mapema ili kuchukua hatua kabla ugonjwa haujasababisha madhara makubwa.

Kwa upande wa watoto na vijana, Daktari Bingwa wa Watoto Mbobezi wa Magonjwa ya Kisukari na Homoni, Dkt. Monica Appollo, anasema mabadiliko ya maisha yamepunguza shughuli za mwili miongoni mwa kundi hilo.

Anataja kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa, matumizi ya pombe na sigara, ikiwamo shisha, pamoja na unene kupita kiasi kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza hatari ya kisukari aina ya pili kwa vijana.

“Vijana wengi wanakuja na aina ya pili kwa sababu ya mtindo mbovu wa maisha,” anasema.

Hata hivyo, anasema kisukari aina ya kwanza huwapata zaidi watoto na vijana na si matokeo ya mtoto kula pipi au vyakula vyenye sukari nyingi.

Changamoto kubwa ni kuchelewa kutambua dalili kama kiu kali, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito na uchovu.

Dkt. Appollo anasema zaidi ya asilimia 90 ya watoto wanaogundulika kuwa na kisukari Muhimbili hufika wakiwa katika hali mbaya, baadhi wakiwa na diabetic ketoacidosis [DKA].

Tanzania STEPS Survey 2023 inaonyesha pia kuwa zaidi ya asilimia 72 ya watu waliokuwa wamegundulika kuwa na kisukari hawakujua kuwa wanaishi na ugonjwa huo.

Wataalamu wanahimiza jamii kuongeza shughuli za mwili, kula kwa uwiano na kupima afya mapema ili kupunguza madhara ya kisukari.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement