Na Veronica Mrema,
Kabla ya familia kuamua kuacha kuni au mkaa na kuhamia nishati safi ya kupikia, kuna maswali kadhaa ambayo huhitaji majibu kabla ya uamuzi huo kufanyika.
Jiko litanigharimu kiasi gani? Mtungi au kifaa nitakinunua wapi? Nitakuwa nalipa kiasi gani kila ninapohitaji kuongeza nishati? Je, vifaa hivyo ni salama?
Na kama ninataka kutumia jiko la umeme, gharama ya matumizi itakuwaje na huduma ya umeme itapatikana kwa uhakika?
Maswali hayo yanaweka wazi changamoto kubwa iliyo mbele ya Tanzania katika safari ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Si kuwashawishi wananchi kwamba nishati hiyo ni muhimu pekee, bali kuhakikisha wanaweza kuifikia, kuimudu na kuitumia kwa uaminifu.
Regina Miami, mkazi wa Makabe jijini Dar es Salaam, anasema licha ya kutambua umuhimu wa nishati safi, uwezo wa kifedha wa familia unaweza kuamua aina ya nishati itakayotumika siku hiyo.
“Nishati safi ni wazo zuri, lakini uhalisia wa maisha yetu sisi ni watu wa kutafuta fedha kila siku. Kuna wakati inatokea mtungi umeisha na huna hela, unaishije?” anauliza.
Anasema katika mazingira kama hayo, wakati mwingine hulazimika kutafuta kuni ili kuhakikisha familia yake inaendelea kupata chakula.
“Kwa kweli mimi huwa naingia porini na kusaka kuni mbili, tatu ili nipike familia ile,” anasema. Uzoefu huo unaonyesha kwa nini gharama na upatikanaji haviwezi kutenganishwa na mjadala wa nishati safi.
Mwananchi anaweza kuwa na uelewa wa faida za kuacha kuni au mkaa, lakini pale anapokosa fedha ya kununua au kujaza nishati anayopendelea, anahitaji njia mbadala ya kuendesha maisha yake.
Kwa familia kama ya Regina, swali si tu kama nishati safi ni bora, bali kama inaweza kumudu matumizi yake kwa mwendelezo.
Kuna mitizamo tofauti pia ikiwamo nafasi ya Sera, rasiliamli fedha, teknolojia na sekta ya habari katika kusukuma mbele agenda ya nishati safi, Tanzania.
Suala linalowaleta pamoja wanahabari kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam [DAR-PC] na wadau wa masuala ya sekta ya niashati safi ili kujadili kwa pamoja 13 Nov, 2026.
"Kuna suala la mabadiliko ya tabianchi lakini linapozungumzwa kuna ambao wanaelewa ni ongezeko la joto, jua kali au mvua kupita kiasi, au kupungua kwa mvua.
"Lakini mabadiliko ya tabianchi yanakuja na athari nyingi ikiwamo ukosefu wa chakula, majanga na magonjwa mbalimbali,' anasema Mhariri Mwandamizi Hafidh Kido.
Kwa mtazamo wa Kido, matumizi ya nishati safi ya kupikia ni sehemu ya mjadala mpana wa namna jamii inavyolinda mazingira.
Mtizamo ambao unafanana kwa ukaribu na wa Mwandishi nguli na Mhariri Mwandamizi Joyce Shebe ambaye kwa muda sasa, amejikita katika uchechemuzi wa masuala ya mazingira nchini Tanzania.
Joyce anasema matumizi ya nishati safi yatasaidia kupunguza uhitaji wa matumizi ya kuni na shughuli nyingine zinazochangia uharibifu wa mazingira.
"Bado waandishi wa habari tuna nafasi ya kusaidia jamii ya Tanzania kuachana na ukataji miti, tunaona sasa hivi hali ya hewa imebadilika, imekuwa mbaya.
"Tunahitaji kupanda miti na kutunza mazingira, kutumia nishati safi kwa sababu sisi ni binadamu na bado tutaendelea kutegemea mazingira," anasema Joyce.
NYENZO BIASHARA
Wakati changamoto ya gharama inaweza kumrudisha mwananchi kwenye kuni, kwa wengine nishati safi tayari imekuwa sehemu ya shughuli zao za kila siku za kiuchumi.
Fabian Ismail, anayejishughulisha na uuzaji wa vitafunwa, hasa chapati na keki, anasema anatumia nishati safi kwa sababu inamwezesha kufanya kazi kwa urahisi, usafi na haraka.
“Unakuta wateja wamenijalia hapa, nauza zaidi jioni. Nina majiko mawili, nina vijana watatu, wanasaidiana chap-chap, watu wanapata huduma,” anasema.
Kwa mfanyabiashara kama Fabian, suala la nishati haliishii kwenye namna ya kupika. Linaingia moja kwa moja kwenye uwezo wa kuzalisha, kuhudumia wateja na kuendesha biashara.
Uzoefu wake unaonyesha upande mwingine wa mjadala wa nishati safi: kwamba inapopatikana kwa namna inayokidhi mahitaji ya mtumiaj.
Inaweza kuwa sehemu ya kuongeza ufanisi na kufungua nafasi za kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo.
KUTOKA SERA HADI JIKONI
Katika ngazi ya sera, nishati safi ya kupikia imewekwa kama sehemu ya safari ya Tanzania kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Tanzania imeweka Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034, unaolenga kufikisha matumizi ya nishati hiyo kwa 80% ya Watanzania ifikapo mwaka 2034.
Lakini utekelezaji wa sera hiyo unatokea jikoni mahali ambapo familia hupima gharama, urahisi, usalama na uwezo wa kuendelea kutumia nishati waliyoichagua. Ndiyo maana taarifa za wananchi zinakuwa muhimu.
Hapa ndipo unapoonekana umuhimu wa sekta ya habari na waandishi wa habari katika kuhakikisha anawafikishia taarifa za kina wananchi.
Ni muhimu kuangazia matumizi ya nishati safi kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, familia, wafanyabiashara wadogo, wapishi wa shule na taasisi nyingine ili kuelewa kile kinachotokea baada ya teknolojia kufika kwa mtumiaji.
Kwa kufanya hivyo, habari inaweza kuonyesha tofauti kati ya kile kinachokusudiwa na sera na kile kinachotokea katika maisha ya wananchi. Jukumu hilo linaungwa mkono na wanahabari wenyewe.
Suleiman Jongo ni Mjumbe wa Bodi ya DAR-PC na Mhariri Mwandamizi wa Uhuru Publication anasema wanahabari wanao wajibu wa kusimama pamoja katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi.
"Kwa sababu hili ni suala mtambuka na linagusa maisha ya sehemu kubwa ya jamii.
"Tunapaswa kuendelea kutoa elimu ili wananchi waelewe umuhimu wa nishati safi na athari chanya zinazoweza kutokana na matumizi yake," anasisitiza Jongo.
Changamoto nyingine ipo katika namna jamii inavyoitazama teknolojia yenyewe.
Meneja wa Sera na Mikakati Uendelevu wa CRDB, Rukonge Sospeter Muhongo, amesema baadhi ya vikwazo vya matumizi ya majiko banifu vinahusishwa na mitazamo na tamaduni zilizojengeka katika jamii.
Ametoa mfano wa imani kwamba baadhi ya vyakula, ikiwemo wali wa nazi, haviwezi kuwa na ladha inayotarajiwa vinapopikwa kwa majiko banifu.
Hii inaonyesha kwamba mpito wa nishati hauhusishi kubadilisha kifaa pekee; pia unahusisha kubadilisha namna watu wanavyokiona na kukitumia kifaa hicho.
Kwa hiyo, elimu ya umma haiwezi kutenganishwa na utekelezaji wa ajenda ya nishati safi.
Waandishi wanaweza kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa kueleza aina za majiko yanayopatikana, teknolojia zake, ubora.
Uimara, gharama na namna yanavyotumika katika mazingira halisi badala ya kuandika kuhusu faida zake kwa ujumla.
Fedha zinaingia kwenye mnyororo
Wakati wananchi wakihitaji nishati safi inayoweza kumudu, sekta ya fedha nayo inaanza kuonekana kama sehemu ya suluhisho.
Muhongo amesema CRDB imeweka takribani dola za Marekani milioni 62, sawa na Sh bilioni 157.1, kupitia mpango wake wa Kijani Bond kwa shughuli zinazohusiana na ufadhili na uendeshaji wa sekta hiyo.
Kwa mujibu wa CRDB, bidhaa za nishati safi ya kupikia ni sehemu ya mpango huo, huku benki ikiandaa bidhaa zitakazohusisha biashara ya hewa ukaa na matumizi ya majiko banifu.
CRDB pia inatarajiwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni [NCMC], kilicho chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, katika mkataba unaohusu bidhaa ya biashara ya hewa ukaa.
Hapa ndipo ajenda ya nishati safi inapopanuka kutoka suala la jiko la familia na kuwa sehemu ya mnyororo mpana unaohusisha fedha, biashara, teknolojia na fursa kwa wajasiriamali.
Lakini fursa hizo nazo zinahitaji habari zinazomweleza mwananchi zinavyofanya kazi na nani anayenufaika nazo.
Maswali hayo ndiyo yanaweza kuifanya habari kuwa sehemu ya suluhisho.
Kwa sababu mwisho wa safari, mafanikio ya nishati safi ya kupikia hayatapimwa kwa idadi ya mikakati iliyotangazwa au teknolojia zilizozalishwa pekee.
Yatapimwa pia na familia zinazoweza kupika kwa nishati salama, inayopatikana na inayoweza kumudu na wananchi wanaoweza kufanya uamuzi huo wakiwa na taarifa sahihi.
Hapo ndipo kalamu ya mwandishi wa habari inapopata nafasi yake katika safari ya Tanzania kuelekea 2034 na hatimaye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Chapisha Maoni