moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Utamu wa penzi unanoga zaidi pale unapojua hisia zako na mwenza wako zinaambatana pamoja, nia yenu pia ni moja, matamanio na ndoto yenu ya kujenga familia yenye furaha, amani na afya njema nayo ni moja.

Ni mchana, jua si kali sana mbele yetu wanasimama vijana wawili wa kike na kiume wamekuja wakiwa wameambatana pamoja, hapa katika viwanja vya Kituo cha Afya Kiwangwa.

Kuna tukio linaloendelea, wananchi wamejitokeza kupata elimu na uchunguzi wa awali wa kinasaba cha Siko Seli, lililoandaliwa na Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli Tanzania [SCDPCT].

SCDPCT imeandaa tukio hili kwa ushirikiano na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, halmashauri ya Chalinze na wadau mbalimbali wa masuala ya Siko Seli na maendeleo ya kijamii.

Basi wanapokewa na maafisa utabibu wa SCDPCT waliopo hapa, wanajitambulisha kwa pamoja "Sisi ni wachumba".

Punde sauti inaniita "Dada Vero, sogea karibu hapa," natambua sauti ile ni Afisa Utabibu Julius Joseph. Najongea kwa haraka.

Julius anaongeza "Vijana hawa ni wachumba, wamekuja wanahitaji elimu na kuchunguza hali zao,". Hii ni sentensi aliyoitoa kwa furaha.

JE KWANINI?

Nilielewa wazi furaha hii inatokana na ukweli kwamba katika matukio kadhaa ambayo tumepata kwenda kwa jamii kufanya uchunguzi wa afya, hatujawahi kupata vijana waliokiri wazi mbele yetu wao ni wachumba.

Julius anaishi pia na ugonjwa wa Siko Seli anaelewa kwa kina changamoto mbalimbali ambazo mtu mwenye Siko Seli hukabiliana nazo karibu kila siku.

Ukweli mwingine ni ule wa ushahidi wa kisayansi, ikiwa mtu mume na mke wenye kinasaba cha Siko Seli wakiamua kuishi pamoja na kuanza kutengeneza mtoto/watoto wana uwezekano mkubwa wa kumrithisha.

Kwa hiyo hatua waliyochukua wachumba hawa ni ya muhimu na ya msingi katika kuepusha familia kupata mtoto mwenye uwezekano mkubwa wa kuzaliwa na ugonjwa wa Siko Seli.

Mimi nawapongeza, kisha nasogea kando kidogo kumpisha Julius ili awape elimu na wafanyiwe uchunguzi kama walivyohitaji.

Anawauliza, "Je mnajua Siko Seli ni nini?". Kwa pamoja wanajibu "Hapana".

Uelimishaji unaanzia hapa, wanaeleweshwa kuhusu Siko Seli. Julius anawaeleza "Siko Seli si ugonjwa wa kuambukiza.

"Mtoto huzaliwa nao kwa kurithi vinasaba vya ugonjwa kutoka kwa baba na mama yake ambao wao huwa ni wabebaji wa vile vinasaba ndani ya miili yao,".

Gloria anasisitiza "Mtu mwenye kinasaba kimoja cha Siko Seli yeye si mgonjwa, ila tu ndani ya mwili wake ni mbebaji, kama mimi nimebeba kinasaba lakini siumwi.

"Mtu aliyebeba kinasaba cha Siko Seli haoneshi dalili yoyote, isipokuwa mtu mwenye ugonjwa ndiye ambaye huonesha dalili na kuugua mara kwa mara,".

Somo likawaingia, baada ya muda mfupi nashuhudia, maafisa utabibu wakifungua karatasi, vipimo vya 'Sickle Scan' wakavichukua.

Julius anampima mmoja na Gloria Mubyazi anampima mwingine. Baada ya dakika kadhaa tu, majibu yao yapo tayari wachumba hawa wapo vizuri nashuhudia pia sura zao zikiwa na tabasamu.


HALI HALISI PWANI

Mkoa wa Pwani una jumla ya wagonjwa 5,423 wa Siko Seli, kati yao 1,300 wanaishi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.

Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze inafuatia, yenyewe ina jumla ya wagonjwa 399, takwimu hii ni kwa mujibu wa Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza katika Mkoa wa Pwani Dkt. Eligreater Mzava anasema changamoto ambayo bado inaonekana ni uelewa duni wa jamii kuhusu ugonjwa huo.

"Bado kuna watu hawajijui hali zao, hata wale ambao wana watoto wenye ugonjwa huu baadhi kwa sababu ya uelewa duni hawawaleti hospitalini mapema.

"Wengi wanafikiria ni ugonjwa wa kurogwa na wanachelewa kufika hospitali kupata matibabu, lakini si wa kurogwa unatokana na urithi wa kinasaba,”.

Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa ile yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa Siko Seli nchini Tanzania.

"Kila mwaka kuna watoto wapatao 14,000 wanaozaliwa na Siko Seli Tanzania, idadi hiyo imeiweka katika nafasi ya tatu Barani Afrika na ya nne duniani kwa wingi wa wagonjwa,".

Mratibu wa Siko Seli Wizara ya Afya Dkt. Asteria Mpoto anasema hilo na kuongeza "Kwa sababu hiyo, Tanzania hatutakaa kimya, tunashirikiana na wadau mbalimbali kuifikia jamii.

"Ndiyo maana leo tumekuja hapa Kiwangwa ni juhudi za kuhakikisha elimu inafika na uchunguzi wa mapema unafanyika.

"Tunahimiza vijana kujua hali zao kwa sababu kwa kufanya hivyo inasaidia mno kuvunja mduara wa kupata mtoto au watoto wenye ugonjwa wa Siko Seli,".

"Siko Seli bado ni tatizo kubwa, hatutachoka kuendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali," anasisitiza Dkt. Asteria.

SISI HATUKUJUA

Sasa wachumba waliofika hapa natambua majina yao ni Yusuph Isack na Loveness Elia na katika mahojiano yetu maalum wanasema hapo kabla hawakuwa na uelewa kabisa Siko Seli ni nini?

Vijana hawa wanasema pia hawakujua iwapo kuna umuhimu wa kupima vinasaba vyao kabla ya kuzama kwenye penzi.

"Tunapokaa ni jirani na eneo hili, tuliposikia muziki mkubwa, tukajiuliza kuna nini huko, tukasema lazima nasi tufike eneo hili," anasema Isack.

Loveness anaongeza "Unajua sisi ni wafanyabiashara ndogo ndogo na hatukuwa hapa jana, kwa hiyo leo tuliposikia muziki ndiyo maana tuliamua kusogea.

"Kwa vile tupo jirani hapa na MC alikuwa anatangaza tulihamasika na kuja, tulipoona kuna upimaji basi tukasema ni jambo zuri, kwanini tusipime,".

Kwa pamoja wanasema namna walivyopokewa kwa ukarimu mkubwa na wataalamu wa afya iliwavutia pia na kukubali kupima hali zao.

Yusuph na Loveness wanasema "Sisi tuna miezi miwili sasa tangu tumeanza kuishi pamoja.

"Sasa kwa namna walivyotueleza kama tungekuwa na hicho kinasaba maana yake tungeweza kupata mtoto mwenye ugonjwa huu," anasema Loveness.

Anaongeza "Sisi hatukuwahi kujua wala hatukuwahi kusikia kuhusu Siko Seli".

KIJIJI KWA KIJIJI

Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze sasa inaelekezwa kuchukua hatua zaidi kufikia jamii kijiji kimoja hadi kingine, kupeleka elimu sahihi kuhusu Siko Seli na uchunguzi wa awali wa kinasaba.

Hatua hii itasaidia kuibua mapema walio wagonjwa na kuwahishwa kupata huduma stahiki hospitalini, hivyo kuokoa maisha.

"Serikali imeimarisha huduma za afya, hapa tulipo tu mnaona tumejengewa Kituo cha Afya Kiwangwa hapo kabla ilikuwa zahanati."

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Leon Mgweno anasema hayo akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete.

Leon anamwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo kuandaa utaratibu mzuri utakaowezesha wataalamu wake kwenda kuibua wagonjwa hadi vijijini.

“Takwimu zinaeleza ambao wamegundulika Chalinze yetu ni 399, Mkurugenzi na DMO nakuagiza, hii ubainishaji au vipimo, andaa utaratibu mzuri.

“Halmashauri yetu inajimudu kusema kwamba kila wiki mbili tukatenga siku tatu, tatu kwa kila kata tukawasogezee wananchi huu.

“Wakaenda wakapata uchunguzi na wakapata majibu, sisi Chalinze tunaweza. Andaa utaratibu, wasiliana na timu ya Wizar ana Mkoa,” ameagiza.

Mgweno anasisitiza “Kama kunahitaji uwezeshaji mimi kama Mwenyekiti… tunajimudu, nitafanya hilo kuhakikisha huduma inafika huko [kwa wananchi], ili tuweze kujipanga tutambue ukubwa wa Tatizo.

“Yaweza ikawa watu huko pengine … kwa sababu Siko Seli ni ugonjwa anakuwa na upungufu wa damu, tukaamini mambo ya kishirikina huko vijijini kwamba sasa ita lambalamba [mganga wa jadi].

“.., ita sijui nani kuna kitu kinakula mtoto damu. Kuna kitu sijui kinafanya hivi na mambo mengineyo.

“Kumbe ni suala tu la kupima na kujua basi maisha mengine yanaendelea kama kawaida. Dada yangu pale [Mkurugenzi wa SCDPCT], ukimuona anavyoshine yupo vizuri kabisa.

“Lakini mtu akisikia Siko Seli anaona sijui ni kitu cha aina gani, kumbe ni magonjwa ambayo wewe unaweza ukawa huna Siko Seli una magonjwa mengine, hivyo ni vitu vya kawaida kabisa,” amesema.

Wachumba hao wakizungumza na mwandishi wa makala haya.

HATUA ZAIDI

Diwani wa Kata ya Kiwangwa Malota Kwaga anahimiza uongozi wa Kituo cha Afya Kiwangwa kuhakikisha kinakusanya na kuweka data zake vizuri za wagonjwa wa Siko Seli ili zisaidie katika kuandaa mipango thabiti.

Mkurugenzi Mtendaji wa SCDPCT Arafa Said anasema lengo hasa la taasisi hiyo katika maadhimisho hayo ilikuwa kueneza elimu ya Siko Seli pamoja na watu kujijua hali zao za vinasaba.

“Pia, kuwapa wananchi elimu ya lishe, uchungui wa kisukari, shinikizo la damu, urefu na uzito na kuna waliojitokeza kuchangia damu kwa hiyari.

“Tunakusudia pia kupata Gazelle Machine moja ambayo tutakuja kuileta hapa Kituo cha Afya Kiwangwa ili kuendelea kushirikiana vema na Serikali kusogeza huduma kwa wananchi.

“Hivyo, tunaendelea kuwaomba wadau mbalimbali wa maendeleo waendelee kutuunga mkono katika hili,” anatoa rai.

Mpango huo pia unalenga kuimarisha huduma za outreach ili elimu, uhamasishaji na uchunguzi wa Siko Seli viweze kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya Chalinze.

Hususan jamii ambazo bado hazijafikiwa vya kutosha na huduma na taarifa kuhusu Siko Seli.

Aidha, SCDPCT inaomba Serikali na wadau kuendelea kushirikiana katika kuwezesha watoto wanaoishi na Siko Seli kupata bima ya afya.

".., ili kupunguza changamoto za gharama za huduma na kuwawezesha kupata huduma wanazohitaji kwa wakati,".

Anatoa rai kwa jamii kuacha imani potofu kuhusu Siko Seli na kutafuta taarifa sahihi kutoka kwa wataalamu wa afya.

"Mtu mwenye Siko Seli ana uwezo na haki sawa na wale wasio na ugonjwa, ikiwamo kusoma, kufanya kazi na hata kujenga familia na kuchangia maendeleo ya kijamii na Taifa," anasisitiza.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Theopister Joseph anasema tukio hilo lililoandaliwa na SCDPCT limekuwa la kipekee na lenye manufaa kwa jamii.

"Nikuhakikishie mgeni rasmi, pamoja na watendaji wenzangu tutakwenda kuandaa mpango ulioagiza wa kufika kwa jamii kufanya uchunguzi na uelimishaji wa Siko Seli."

Yusuph na Loveness Kwa pamoja, wachumba hao wanatoa rai kwa vijana wengine nchini.

Ni muhimu kufika mapema vituo vya kutolea huduma za afya kabla ya kuanza mapenzi ili kupata elimu ya Siko Seli na kufanya uchunguzi wa hali zao za vinasaba.”

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement