moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Kila mzigo unaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege huwa na mwenyewe. Lakini kwa mzigo huu, mambo yalikuwa tofauti.

Ulitokea nchini India ukiwa umepakiwa kwenye ndege pamoja na mizigo mingine ya abiria.

Ukafika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere [JNIA], Dar es Salaam, lakini baada ya ndege kutua, mizigo ikapitishwa kwenye sehemu yake ila hakuna aliyefika eneo hilo, kuuchukua.

Abiria wengine walichukua mizigo yao na kuondoka. Huu ukabaki. Maafisa wa JNIA wakauchukua na kuuweka pembeni.

Muda ukasonga, mwenyewe hajitokezi wakautilia shaka na kuamua kufungua begi moja, kuna dawa na si moja ni nyingi.

Kwa wakaguzi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba [TMDA] ambao wapo hapo pia uwanjani kila siku wakitekeleza majukumu yao, mzigo huo sasa wakautazama kwa jicho la tatu.

Ukaguzi zaidi ukafanywa, mabegi mengine nayo yakakutwa na bidhaa za tiba [dawa pamoja na vifaa tiba], sasa yamefika takribani masanduku 20.

Swali kubwa, wakajiuliza, Kwa nini mtu atume kiasi hiki kikubwa cha dawa nchini, halafu asije kukichukua?

Shaka hiyo ikawasukuma kuendelea kukagua zaidi shehena hiyo, ndipo wakabaini  mzigo huo haukuwa na kibali cha kuingizwa nchini.

Boksi moja baada ya jingine ilikaguliwa, kuna dawa zinazotumika katika matibabu ya saratani, kisukari, shinikizo la damu, malaria, pumu, magonjwa ya damu na kifua kikuu.

Pia kuna antibiotiki, dawa za homoni kwa wanaume na wanawake, dawa za kupunguza uzito, pamoja na vifaa tiba vya hospitalini, ikiwamo vifaa vya upasuaji na vifaa vya meno bandia.

Miongoni mwa bidhaa zilizotajwa ni zile zinazohusishwa na Ozempic/semaglutide na dawa za kundi la GLP-1, ambazo zimepata umaarufu mkubwa katika udhibiti wa kisukari na kupunguza uzito.

Lakini jambo lililowatia wasiwasi zaidi maafisa hao halikuwa wingi wa bidhaa hizo pekee. Hakuna hata moja iliyokuwa imesajiliwa nchini Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Dkt. Adam Fimbo amefafanua "Maana yake ni kwamba bidhaa hizo hazikuwa zimepita katika mchakato wa kawaida wa uthibitishaji unaofanywa na TMDA.

"Ili kuhakikisha dawa au kifaa tiba kinachotumika nchini kinakidhi viwango vinavyotakiwa vya ubora, usalama na ufanisi,". 

Mzigo huu tulioukamata una thamani ya TZS Mil. 310, lakini kinachoshtua zaidi na kuacha swali la msingi kuhusu mzigo huu uliotelekezwa JNIA, je nini kingetokea iwapo ungefika kwa mwananchi.

NI HATARI!

Kwa mgonjwa, jina la dawa, rangi ya boksi au maelezo yaliyoandikwa kwenye kifungashio yanaweza kumfanya aamini kuwa bidhaa hiyo ni salama.

Lakini kwa mamlaka ya udhibiti, hilo pekee halitoshi. Dawa inahitaji kuthibitishwa.

TMDA uhusisha mchakato wa ukaguzi ubora, usalama na ufanisi ikiwamo kuhakikisha ina kiambata kinachotakiwa na kwamba imetengenezwa kwa kufuata viwango vinavyotakiwa.

"Hivyo, dawa isiyosajiliwa ni dawa ambayo haijapitia uthibitishaji huo kwa matumizi katika soko la Tanzania," amesema Dkt. Fimbo na kuongeza,

"Hatari yake inaweza kuwa kubwa zaidi kwa dawa zinazotumika kutibu magonjwa makubwa. Kwa mfano, mgonjwa wa saratani akipewa dawa ambayo haijathibitishwa.

".., na kumbe haina kile kiambata kinachotakiwa, anaweza kuendelea kutumia dawa akiamini anapata matibabu, wakati ugonjwa unaendelea. anaweza hata kupoteza maisha,".

M24 TANZANIA imezungumza na baadhi ya wananchi, "Ni habari inayoshtua, mzigo huo ni mkubwa na kama haujasajiliwa ungefika mtaani wananchi tusingejua, tungenunua na kutumia.

Amesema Asteria Kimaso Mkazi wa Mabibo External na kuongeza "Binadamu hawana huruma tena, wanaangalia fedha badala ya utu, naipongeza Serikali kwa kuzikamata na wafungwe kabisa.

Kauli ambayo inaungwa mkono na Goodluck Benson "Ni suala linalosikitisha, lakini ni hatua nzuri kuona mzigo umezuiliwa na kukamatwa kabla haujafika kwetu.

"Ungeingia mtaani huo tungetumia na ujue sisi wananchi si rahisi kujua kama dawa au sindano uliyonunua ina kibali, imekaguliwa au la, unashangaa unatumia huponi,".

SHEHENA NYINGINE

Uchunguzi wa shehena hiyo iliyonaswa Septemba 7, 2026 ukiendelea TMDA imenasa shehena nyingine Septemba 9, 2026.

Safari hii, ilikuwa ni dawa za sindano na bidhaa nyingine za tiba zenye thamani ya takribani TZS Mil. 50.

Miongoni mwa dawa zilizokamatwa ni lignocaine, bupivacaine, adrenaline na vitamini. Hivyo, ndani ya siku mbili hizi shehena ya TZS Mil. 360 imeingizwa kinyemela na kunaswa na TMDA.

Lakini thamani ya fedha si kipimo pekee cha ukubwa wa tukio hili ambalo Dkt. Fimbo na maafisa wake wa TMDA wameeleza hawajawahi kurekodi kiwango kikubwa cha ukamataji namna hiyo. 

Swali muhimu zaidi ni: Ni wagonjwa wangapi wangeweza kufikiwa na dawa hizi kama zingeingia kwenye soko bila kugunduliwa?

Na zingeishia wapi? Duka la dawa? Hospitali? Kliniki binafsi? Au mikononi mwa mtu anayenunua dawa moja kwa moja bila ushauri wa mtaalamu?

AFYA NA MAISHA YA WATU

Dkt. Fimbo amesema mapambano dhidi ya dawa zisizosajiliwa, bandia na duni yanafanyika kila siku TMDA.

"Mamlaka ina ofisi za kanda nane nchini na inaendesha ukaguzi katika maeneo mbalimbali, huku vituo 32 vilivyotengwa kisheria kwa ajili ya kuingiza bidhaa nchini vikiwa na maafisa wa ukaguzi.

"Dar es Salaam ni lango kubwa kutokana na uwepo wa bandari, uwanja wa ndege na vituo vya ICD. 

"JNIA, maafisa hufanya kazi upande wa mizigo na upande wa abiria, kwa kushirikiana na Polisi na maafisa wa forodha," amesisitiza.

Amesema TMDA pia hutumia taarifa za kiintelijensia, mifumo inayohusishwa na TRA, ukaguzi wa kushtukiza, upimaji wa haraka na operesheni za pamoja na vyombo vingine vya dola.

Kwa baadhi ya matukio, mamlaka hufuatilia hata chanzo cha bidhaa nje ya Tanzania ili kubaini namna bidhaa hizo zilivyofika nchini.

UCHUNGUZI UNAENDELEA

TMDA tayari imenasa watuhumiwa watano katika sakata hilo la shehena ya JNIA, uchunguzi unaendelea pia wanafuatilia katika viwanda husika ambako mizigo hiyo imetoka.

"Maafisa wameweza kupata baadhi ya taarifa kupitia vitambulisho vya mizigo vilivyokuwa kwenye mabegi hayo na wanashirikiana na mamlaka nyingine kumtafuta mhusika," amesema Dkt. Fimbo.

Ameongeza kila mwananchi ana nafasi katika kushirikiana na TMDA katika kulinda afya ya jamii.

"Natoa wito waendelee kutupa taarifa pale wanapobaini viashiria vya dawa au vifaa tiba vinavyotiliwa shaka kupitia ofisi zetu, au namba yake ya bure 0800110084,".

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement