Na Mwandishi Maalum
Wataalamu wa afya ya akili wamepongeza juhudi za Tanzania Mental Health Journalists Organization (TAMHJO) katika kuwaunganisha waandishi wa habari na wataalamu wa afya ya akili, wakisema jukwaa hilo lina nafasi kubwa ya kuchagiza ajenda ya afya ya akili kupitia sekta ya habari nchini.
Wataalamu hao walitoa kauli hizo katika kikao cha mtandaoni kilichoandaliwa na TAMHJO tarehe 9 Agosti 2026, kilichokuwa na mjadala wenye mada “Je, Vyombo vya Habari Vina Nafasi Ipi katika Kuimarisha Afya ya Akili kwa Jamii?”
Kikao hicho kilifunguliwa na Rais wa TAMHJO, Veronica Mrema, ambaye alisema TAMHJO ni jukwaa la waandishi wa habari za afya ya akili lililoanzishwa kwa lengo la kuondoa pengo lililokuwapo kati ya wataalamu wa afya ya akili na waandishi wa habari.
Mrema alisema hadi sasa TAMHJO imewajengea uelewa zaidi ya waandishi wa habari 100 kupitia mafunzo ya mtandao na ana kwa ana, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha sekta ya habari inashiriki ipasavyo katika kuielimisha jamii kuhusu afya ya akilli.
Alisema TAMHJO ilianzishwa rasmi kufuatia maoni yaliyotolewa na wataalamu wa afya ya akili, kwenye mdahalo wa kwanza wa kitaifa kuhusu afya ya akili ambao ulifanyika JNICC mwaka 2022 ambapo ilionekana wazi kuna haja ya kuhusisha sekta ya habari ipasavyo ili jamii ipate taarifa sahihi zitakazowasaidia kujenga afya bora ya akili.
Alisema dhamira ya TAMHJO ni kuona waandishi wa habari wanapata uelewa na ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wataalamu ili waweze kuandika na kuripoti masuala ya afya ya akili kwa usahihi, huku taarifa hizo zikisaidia kuelimisha jamii.
Katika kikao hicho, Makamu wa Rais wa TAMHJO, Dkt. Raymond N Mgeni, alieleza namna tafiti mbalimbali zinavyoonesha umuhimu wa vyombo vya habari katika masuala ya afya ya akili, akitolea mfano tafiti zilizofanyika nchini Ethiopia (Anbessie et al., 2023). zinazohusisha nafasi ya vyombo vya habari na uelewa wa jamii kuhusu afya ya akili.
Dkt. Mgeni alieleza umuhimu wa kutumia ushahidi wa tafiti katika uandishi wa habari za afya ya akili, akisisitiza haja ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya wataalamu wa afya ya akili na waandishi wa habari ili taarifa zinazowafikia wananchi ziwe sahihi na zenye kusaidia jamii.
Wataalamu hao wamesema bado kuna pengo kubwa la uelewa kuhusu afya ya akili katika jamii, hivyo uwepo wa jukwaa linalowaunganisha wataalamu na waandishi wa habari ni muhimu katika kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi na kusaidia kupunguza hofu, unyanyapaa na mitazamo potofu kuhusu afya ya akili.
Akizungumza katika kikao hicho, Jessie Mbwambo, Dkt. Bingwa Magonjwa ya akili mstaafu alisema bado kuna changamoto ya kutofautisha kati ya afya ya akili, magonjwa ya akili na changamoto za afya ya akili, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwajengea waandishi wa habari uelewa kuhusu masuala hayo.
Naye Leah Natujwa Omari, Dkt wa sosholojia alisema watu wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa ya akili, hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuendelea kutoa nafasi kwa wataalamu ili jamii ipate elimu sahihi.
Dkt. Leah pia alisisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi watu wenye uzoefu wa changamoto za afya ya akili kutoa ushuhuda wao, akisema uzoefu huo unaweza kusaidia kujenga uelewa ndani ya jamii.
“Elimu itolewe na wataalamu wa masuala ya afya ya akili, lakini pia ni muhimu kuwapa nafasi waathirika ili nao watoe zile shuhuda zao, zinasaidia katika kujenga uelewa ndani ya jamii,” alisema.
Kwa upande wake, Mama Lucy Chikongoye kutoka TEWWY (Tap Elderly Women's Wisdom for Youth) alisema TAMHJO ina kazi kubwa ya kufanya katika kubadilisha tafsiri ya jamii kuhusu afya ya akili, kutoka kwenye hofu na unyanyapaa kuelekea uelewa.
Alisema bado watu wengi hawajui afya ya akili ni nini, hivyo jukwaa hilo linapaswa kuendelea na juhudi za kuhakikisha elimu inawafikia wananchi kupitia vyombo vya habari.
Naye Tumaini Mzengi kutoka Arusha alisema TAMHJO inapaswa kuwa endelevu kutokana na uhitaji mkubwa wa elimu ya afya ya akili katika jamii.
Alisema afya ya akili ni ajenda pana inayogusa maisha ya watu kwa namna mbalimbali, hususan vijana ambao wanakabiliwa na changamoto kama msongo wa mawazo, ukosefu wa ajira, changamoto za mahusiano na ndoa.
Aliongeza kuwa shinikizo kutoka kwa makundi rika, muziki na sanaa, pamoja na matarajio ya maisha yanayoonyeshwa katika jamii, yanaweza kuongeza changamoto kwa baadhi ya vijana pale wanaposhindwa kufikia kile wanachokiona au kukitamani.
Aidha, alisema changamoto zinazohusiana na mwonekano wa mwili, ikiwamo kutoridhishwa na unene au unyembamba, pamoja na makovu yanayotokana na ajali, zinaweza pia kuathiri ustawi wa mtu na kusababisha msongo wa mawazo na changamoto nyingine za afya ya akili.
Nankondo Mtaita, Afisa Muuguzi, alisema vipindi vya afya ya akili vinapaswa kuwa endelevu redioni na kwenye runinga, huku magazeti yakiendelea kuandika makala zinazolenga kuelimisha jamii.
Alisema ushirikiano kati ya waandishi wa habari na wataalamu ni muhimu katika kumsaidia mwananchi kufahamu namna ya kulinda afya yake ya akili, kutambua anapohitaji huduma na kujua mahali pa kupata huduma hizo.
Alisema bado kuna watu wanaokwenda kwa waganga wa kienyeji kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu huduma za afya ya akili zinazopatikana.
Kwa upande wa waandishi wa habari, Christina Mwakangale, mwandishi wa Nipashe, alisema bado kuna changamoto ya baadhi ya wataalamu wa saikolojia kutokuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari wanapohitaji mahojiano kwa ajili ya habari au makala.
Alisema ushirikiano wa karibu zaidi kati ya wataalamu na waandishi wa habari unaweza kusaidia kuhakikisha habari za afya ya akili zinaandaliwa kwa usahihi na kwa kuzingatia utaalamu.
Akizungumza katika kikao hicho, Daktari bingwa wa magonjwa ya akili Dkt. Saidi Kuganda aliwashukuru wataalamu na waandishi wa habari walioshiriki, akisema mjadala huo umeonyesha umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo.
Alisema waandishi wa habari wanapaswa kutumia kalamu zao vizuri ili jamii ipate uelewa kuhusu afya ya akili, itambue dalili za awali na ichukue hatua mapema.
“Jambo hili linapaswa kuendelea na waandishi wa habari muendelee kutumia vyema kalamu zenu ili jamii ipate uelewa, ifahamu dalili za awali na kuchukua hatua mapema,” alisema.


Chapisha Maoni