moja

Responsive Advertisement


Na Mwandishi Wetu

Orodha ya waandishi wa habari sita ambao wamechaguliwa kuendelea na mchakato wa tuzo za ISU Elihle kwa mwaka 2026 Barani Afrika imetajwa hadharani, miongoni mwao ni Mtanzania Veronica Mrema.

Veronica ametajwa katika orodha hiyo baada ya wazo lake la habari kuhusu watoto wanaoishi na ugonjwa wa Siko Seli kupitiwa, na kuonekana ni bora.

Jopo la majaji wa tuzo hizo limesema kulikuwa na mawazo 155 ambayo walipokea kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Kupitia wazo lake lililochaguliwa Veronica atafanya uchunguzi na kuibua simulizi kuhusu mzigo unaoongezeka wa ugonjwa wa Siko Seli miongoni mwa watoto nchini Tanzania.

Ataangazia kwa kina namna ugonjwa huo unavyoathiri maisha ya watoto, kuanzia afya zao, lishe, elimu, ukuaji wa kimwili, pamoja na ustawi wao wa kihisia na kisaikolojia. 

Makala zitaeleza kwa kina changamoto zinazowakabili watoto hao na familia zao katika kupata huduma bora za afya, uchunguzi wa mapema, matibabu na lishe stahiki.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, idadi ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa Siko Seli nchini imeongezeka kutoka takribani watoto 8,000 hadi 14,000 kila mwaka, hali inayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huo Afrika na duniani. 

Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi tatu zenye idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo Barani Afrika kila mwaka huku ikishika nafasi ya nne duniani.

Pamoja na ukubwa wa tatizo hilo, bado kuna watoto bado hukumbana na changamoto za kuchelewa kugundulika, ukosefu wa huduma maalum za matibabu na uelewa mdogo wa jamii kuhusu ugonjwa huo.

Veronica atakusanya simulizi za watoto wanaoishi na Siko Seli, wazazi na walezi wao, wataalamu wa afya, wataalamu wa lishe pamoja na watunga sera, kwa lengo la kuonesha hali halisi ya maisha yao na kuibua suluhisho zinazoweza kuboresha afya na ustawi wa watoto hao.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mmoja wa washindi, Veronica amesema amepokea kwa heshima kubwa kutajwa katika orodha hiyo ya ISU Elihle.

"Ni fursa ya kuendelea kutumia uandishi wa habari kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

"Kuchaguliwa miongoni mwa waandishi sita kutoka kazi 155 zilizowasilishwa ni heshima kubwa kwangu na kwa Tanzania. Lakini zaidi ya yote, ni nafasi ya kuhakikisha sauti za watoto wanaoishi na Siko Seli zinasikika.

"Ninaamini simulizi hizi zitasaidia kuongeza uelewa wa jamii na kuhimiza uwekezaji zaidi katika uchunguzi wa mapema, huduma za afya na lishe kwa watoto hawa," amesema.

Ameongeza atatumia uandishi wa habari unaozingatia ushahidi, takwimu na simulizi za wahusika ili kuonesha changamoto halisi zinazowakabili watoto wenye Siko Seli na kuibua mijadala itakayochochea maboresho ya sera na huduma za afya.

Makala zake zitaandikwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza ili kuwafikia wasomaji wa ndani na wa kimataifa na zitachapishwa kupitia Jamhuri Media katika toleo la gazeti na majukwaa yake ya mtandaoni.

Pia zitachapwa M24 TANZANIA MEDIA, jukwaa la kidijitali analoliendesha akiwa amejikita katika uandishi wa habari za afya, maendeleo na masuala ya jamii.

Kwa majukwaa hayo, simulizi za watoto wanaoishi na Siko Seli zinatarajiwa kuwafikia wasomaji wengi zaidi ndani na nje ya Tanzania, kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ugonjwa huo na kuchochea mijadala itakayosaidia kuboresha huduma za afya na ustawi wa watoto.

ISU Elihle Award inalenga kuhamasisha uandishi wa habari unaoweka watoto katikati ya simulizi na unaochochea mijadala yenye kuleta mabadiliko ya sera, uwajibikaji na hatua za kuboresha ustawi wa watoto barani Afrika.

Pamoja na Veronica Mrema wa Tanzania, washindi wengine wa ISU Elihle Award 2026 ni David Arome wa The Development Report [Nigeria] na Hind Fawzi wa Medina FM [Morocco].

Rakiya Mohamed wa Blueprint [Nigeria], Wezzie Joy Gausi wa Times Group [Malawi] na Kelvin Tambo wa Capital Radio [Malawi].

Kupitia tuzo hiyo, washindi watapata fursa ya kutekeleza miradi yao ya uandishi kwa msaada wa wahariri na wataalamu wa uandishi wa habari, pamoja na ushauri wa kitaalamu [mentorship] ili kuhakikisha simulizi hizo zinafikia viwango vya juu vya ubora na kuleta athari chanya kwa jamii.

Katika hatua hii, pia watapewa kiasi cha R.10,000 ili kwenda kutekeleza miradi ya uandishi wa makala kulingana na mawazo yao ya habari ambayo waliyawasilisha katika mchakato huo wa kwanza.

Baadae kazi zao zitapitia mchakato wa awamu ya pili ambapo zitashindwa ili kupata washindi watatu bora, miongoni mwao.

Hatua ya Veronica kutajwa kwenye tuzo hiyo inaongeza rekodi nzuri katika uandishi wa habari za afya na maendeleo na kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuendelea kutoa waandishi wa habari wanaotumia kalamu zao kuibua changamoto za watoto na kuchochea mabadiliko yenye manufaa kwa jamii.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement