moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Unapotazama usanifu wa jengo ni mvuto wa aina yake, nakshi na mapambo unaona wazi akili ilitumika vema, ikiwamo pia mandhari yake ya ndani. 

Mpangilio wa taratibu na utekelezaji wa mambo ni wa kipekee. Lakini Bunge ni zaidi ya jengo ulionalo, ndani yake kuna maisha ya kila mwananchi.

Afya ya umma haiishii hospitalini, kwenye dawa au kwa madaktari wanaowahudumia wagonjwa. 

Nyuma ya huduma hizo kuna sera, sheria, bajeti na maamuzi yanayofanyika katika ngazi ya Taifa, ikiwamo ndani ya Bunge.

Suala hili ndilo lilikuwa hasa msingi wa safari ya wajumbe 53 kutoka Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Pwani na Singida waliopata fursa ya kutembelea Bunge la Tanzania kupitia AIDF.

AIDF [Africa Initiative Development Foundation] ni shirika lisilo la kiserikali ambalo limejikita katika kuhudumia jamii kwenye masuala mbalimbali yanayogusa afya ya umma.

Kuna uhamasishaji na uchangiaji damu salama, afya ya mama na mtoto, matumizi ya nishati safi ya kupikia, usafi na utunzaji wa mazingira, nakadhalika.

Oktoba 28, 2026 wajumbe hao wakiwa katika ziara hiyo, walipata nafasi ya kujifunza kuhusu historia ya Bunge, namna linavyofanya kazi na nafasi ya wananchi katika mfumo wa kidemokrasia.

Safari hiyo ilifungua ukurasa mwingine wa uelewa kwamba hoja zinazohusu afya ya wananchi zinapofika katika Bunge, zinahitaji uwakilishi, maswali, takwimu na sera zinazoweza kubadilisha maisha ya watu.

Miongoni mwa masuala yaliyoelezwa katika ziara hiyo ni namna wabunge wanavyotumia nafasi yao kuihoji Serikali kuhusu utekelezaji wa mambo mbalimbali yanayowahusu wananchi, ikiwamo huduma za afya.

Afisa Mwandamizi wa Bunge anayeshughulikia Habari, Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Patson Sobha anasema wabunge wana utaratibu wa kuwasilisha maswali yao kabla ya Bunge kuanza.

Hatua hiyo husaidia Serikali kujiandaa kwa majibu sahihi. Kwa mujibu wa Sobha, maswali hayo huwasilishwa siku 21 kabla ya Bunge kuanza.

Jambo linalowapa wataalamu wa sekta husika muda wa kutafuta nyaraka na taarifa zinazohitajika, hasa takwimu, ili kuwawezesha mawaziri na manaibu mawaziri kutoa majibu yenye ufasaha.

Utaratibu huo unaifanya takwimu kuwa sehemu muhimu ya majadiliano ya kitaifa, kwani swali la mbunge linapohitaji majibu kuhusu hali ya huduma au utekelezaji wa sera, majibu huhitaji taarifa sahihi.

Mbunge anayepata jibu pia anaweza kuuliza swali la nyongeza, lakini Sobha anasema swali hilo linapaswa kubaki ndani ya muktadha wa swali la msingi na si kugeukia jambo jingine lisilohusiana.

Washiriki pia walielezwa kuhusu maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu na namna utaratibu huo unavyofanyika ndani ya Bunge.

Kwa upande wa afya, uelewa huu una umuhimu kwa sababu masuala mengi yanayowagusa wananchi kuanzia upatikanaji wa dawa, huduma za mama na mtoto.

Magonjwa yasiyoambukiza, damu salama na huduma za dharura yanahusisha utekelezaji wa sera na maamuzi ya Serikali ambayo yanaweza kuibuliwa na wawakilishi wa wananchi.

BUNGE MIAKA 100

Ni ziara inayofanyika wakati Tanzania ikielekea katika maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Bunge.

Jambo lililowapa washiriki fursa ya kupata historia ya chombo hicho na kuelewa namna kilivyokua hadi kufikia mfumo wa sasa.

Mafunzo hayo pia yalihusu mgawanyo wa mamlaka kati ya mihimili mikuu ya Dola ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama na namna kila mhimili unavyotekeleza majukumu yake.

Kwa wajumbe wengi, ilikuwa ni zaidi ya kutembelea jengo la Bunge. Ilikuwa ni nafasi ya kuelewa mahali ambapo sheria zinajadiliwa na kutungwa.

Wawakilishi wa wananchi wanapowasilisha hoja na Serikali inapowajibishwa kuhusu utekelezaji wa mambo mbalimbali na siku hiyo walikuwapo Bungeni wakishuhudia kila kinachoendelea.

Sobha anawahimiza vijana na wanawake kutokuwa na hofu ya kujitokeza kugombea ubunge ili kupata nafasi ya kuwawakilisha wananchi.

Ujumbe huo ulienda sambamba na ushauri kwa vijana wanaotafuta ajira kutokuwa na hofu ya kuomba nafasi wanapokuwa na sifa zinazohitajika.

Sobha anasema waombaji wanapaswa kujiamini na kutumia sifa zao za kitaaluma, akieleza kuwa mchakato wa mahojiano huzingatia uwezo wa mtu kitaaluma na si kuwa na “connection” au kufahamiana na mtu.

AIDF BUNGENI

Mkurugenzi wa AIDF, Joel Temba, anasema ziara hiyo imefanyika kufuatilia mwaliko wa Katibu Mkuu wa Bunge kwa Watanzania akitoa maelekezo namna wanavyoweza kuwasilisha maombi.

"Tunamshukuru mno, tuliona tangazo lake na tukaandika barua nasi tupate fursa ya kujifunza, kuhusu Bunge na namna linavyotekeleza shughuli mbalimbali kwa ajili ya Taifa," anasema.

Temba anasema AIDF na washirika wake wamekuwa wakitekeleza shughuli zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi, huku moja ya maeneo wanayoyapa uzito ikiwa ni uhamasishaji wa uchangiaji damu salama.

“Damu haipatikani kiwandani, bali inatoka kwenye mwili wa binadamu,” anasema Temba, akisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kuchangia damu.

Katika msafara huo, AIDF pia iliambatana na mashujaa wa damu salama, wakiwemo watu wawili ambao wamevunja rekodi kwa kuchangia damu zaidi ya mara 100.

Kwa mujibu wa Temba, uchangiaji damu ni tendo la kizalendo kwa sababu unit moja ya damu inaweza kusaidia kuokoa maisha ya watu wazima hadi wanne.

Kwa upande wa kundi la watoto unit moja inaweza kusaidia watoto wapatao sita, kutegemea mahitaji yao ya matibabu.

Anasema juhudi hizo zinaunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuokoa maisha ya mama na mtoto pamoja na wagonjwa wengine wanaohitaji damu.

Miongoni mwao ni watu wanaoishi na Siko Seli, wagonjwa wa saratani, majeruhi wa ajali na wagonjwa wengine wanaohitaji huduma hiyo.

Temba anasema AIDF hivi karibuni ilizindua mpango wa kuwafikia viongozi wa taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha uchangiaji damu, huku ikiwa na mpango wa kuwafikia pia wabunge.

“Tumeanza mpango wa kuwafikia viongozi wa taasisi mbalimbali. Tunataka pia kuwafikia wabunge,” alnaema.

Anasema taasisi hiyo imekuwa ikifanya uhamasishaji katika shule, vyuo, jamii na kupitia vyombo vya habari.

Katika msafara huo pia alikuwepo mwandishi wa makala haya Veronica Mrema, ambaye hutumia jukwaa lake la M24 TANZANIA kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya.

Veronica pia ni miongoni mwa wanawake wachache wanaochangia damu kwa hiyari Tanzania, akitambuliwa na Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Mashariki [EZBTS] kama balozi mzuri wa Damu Salama.

"Veronica amekuwa akitumia vema taaluma yake katika kuelimisha jamii kuhusu magonjwa mbalimbali jinsi ya kuepuka na matibabu yake ikiwamo Siko Seli pamoja na magonjwa mengine.

Temba anadokeza nia ya AIDF kufanya uhamasishaji uchangiaji damu salama pamoja na elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kwa wabunge.

BUNGE NI LENU

Sobha anasisitiza mpango wa AIDF kufikisha wajumbe wake Bungeni ni mzuri na unafaa kuendelezwa.

Uongozi wa AIDF anauelekeza kuwasilisha mapema barua ya kuomba nafasi hiyo ya kuwafikia wabunge ili iweze kuhudumiwa kwa utaratibu unaostahili.

Vijana waliokuwa katika msafara huo, fursa hiyo imekuwa njia ya kuondoa baadhi ya dhana walizokuwa nazo kuhusu Bunge na nafasi yao katika masuala ya Taifa.

Clara Joseph kutoka AIDF Dar es Salaam anasema mafunzo hayo yamempa mwanga zaidi kuhusu historia ya Bunge na kumuongezea morali ya kuwa mzalendo kwa Taifa lake.

“Vijana tuna mengi hatuyajui, ukipita mitandaoni tunalaumu, lakini leo nimejifunza kitu kikubwa. Nashauri na wengine waombe kulitembelea Bunge,” anasema Joseph.

Kwa washiriki, somo kubwa lililobaki ni kwamba uelewa wa wananchi kuhusu taasisi za Taifa ni sehemu ya kujenga ushiriki wao katika maendeleo.

Kwa upande wa afya ya umma, uelewa huo una maana zaidi kwa sababu maamuzi kuhusu afya hayafanywi hospitalini pekee. Sheria, sera, bajeti na uwajibikaji wa Serikali vina nafasi kubwa katika kuamua.

Kuanzia huduma ambazo mwananchi atazipata, dawa atakazopata, mfumo wa dharura utavyofanya kazi na namna watu wenye mahitaji maalumu ya kiafya watakavyohudumiwa.

Kwa muktadha huo, ziara hiyo kwa wajumbe wa AIDF haikuwa tu safari ya kujifunza historia ya Bunge kuelekea miaka 100.

Bali pia ilikuwa safari ya kuelewa mahali ambapo sauti ya jamii inaweza kufika na namna ambavyo wananchi wanaweza kushiriki katika maamuzi yanayogusa maisha yao.

Kwa upande wa afya, ujumbe unabaki kuwa mmoja: Afya ni sera, na sera ni maisha.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement