moja

Responsive Advertisement

Na Mwandishi Maalum

Kila siku, Rahma Abdallah hulazimika kufikiria jambo moja muhimu kabla ya mambo mengine ‘dawa yake’.

Anaishi Chanika, Dar es Salaam, Rahma ni mmoja wa watu wanaoishi na Ugonjwa wa Siko Seli ambao hutegemea dawa ya hydroxyurea kusaidia kudhibiti athari za ugonjwa huo.

Kwa siku, yeye anatumia vidonge viwili vya dawa hiyo, ambapo kila kidonge hununua kwa Sh2,000.

“Ni changamoto sana, hasa unapokuwa huna kazi na unategemea ndugu,” anasema.

Kwa wagonjwa wengi wa Siko Seli, hydroxyurea si dawa ya kawaida tu.

Inaweza kuwa sehemu muhimu ya maisha yao, hususan katika kusaidia kupunguza baadhi ya madhara na vipindi vya maumivu makali vinavyoweza kujirudia.

Ndiyo maana taarifa za Senegal kuanza uzalishaji wa dawa hiyo zimepokelewa kwa matumaini mapya miongoni mwa baadhi ya watu wanaoishi na ugonjwa wa Siko Seli na wadau wa afya Barani Afrika.

Rahma anaona hatua hiyo kama jambo la kujivunia kwa Bara la Afrika.

“Senegal kuanza utengenezaji ni hatua nzuri, kwa sababu bei ya dawa inaweza ikazidi kupungua ili tuzipate kwa wingi,” anasema.

Hatua ya matumaini kwa Afrika

Daktari Collin Kanza kutoka Sickle Cell Center - Muhimbili anaelezea hatua ya Senegal kama mafanikio makubwa kwa mapambano dhidi ya Siko Seli Barani Afrika.

“Ni hatua kubwa sana. Senegal ina wagonjwa wachache wa Siko Seli ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine za Afrika lakini imeweza kufanya jambo hili kubwa.

“Sisi tuna uhitaji mkubwa zaidi wa dawa hizi. Ni wazi tunalo la kujifunza na kuiga mfano kutoka kwao,” anasema.

Tanzania inashika nafasi ya nne duniani na ya tatu Barani Afrika kwa nchi zenye idadi kubwa ya wagonjwa wa Siko Seli, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Takwimu za Wizara ya Afya zinaeleza kila mwaka kuna Watoto 11,000 hadi 14,000 wanaozaliwa na ugonjwa huo kila mwaka nchini Tanzania.

Matibabu dhidi ya ugonjwa huu wa kurithi ni ya muda mrefu, uwezo wa dawa muhimu kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu unaweza kuleta tofauti kubwa katika maisha ya wagonjwa na familia zao.

Hatua ya Senegal pia inafungua mjadala mpana kuhusu uwezo wa Afrika kuwekeza katika uzalishaji wa dawa muhimu zinazohitajika na watu wake.

Kwa sasa, baadhi ya dawa zinazotumiwa na wagonjwa wa Siko Seli Tanzania zinaendelea kupatikana kupitia uzalishaji na mifumo ya usambazaji kutoka nje ya Bara la Afrika, ikiwamo hii ya hydroxyurea.

Iwapo uzalishaji wa hydroxyurea utaongezeka Barani Afrika na dawa hiyo kusambazwa katika nchi nyingine, matumaini ya wagonjwa wengi ni kwamba gharama inaweza kushuka na upatikanaji wake kuongezeka.

Bima ya afya inapunguza mzigo

Wizara ya Afya Tanzania iliingiza dawa hii katika orodha ya dawa zinazopatikana ndani ya bima ya afya.

Kwa Felister John, mzazi wa shujaa wa Siko Seli anayeishi Kigoma, kuwa na bima ya afya kwa mtoto wake kumeleta mabadiliko makubwa.

Anasema kabla ya kuweza kumkatia mtoto wake bima ya afya, familia yake ilipitia changamoto kubwa kwa sababu alilazimika kutoa fedha kutoka mfukoni kununua dawa na kugharamia huduma za matibabu.

“Lakini baada ya kupata bima, hali imeanza kubadilika. Kwa sasa, anaweza kumudu baadhi ya gharama za matibabu ya mtoto wake kupitia bima ya afya,” anasema.

Hata hivyo, kwa familia ambazo hazina uwezo wa kugharamia bima, mzigo wa Siko Seli unaweza kuwa mkubwa zaidi.

Julieth Mombuli ni miongoni mwa wale wanaopambana kila siku kuhakikisha mtoto wake anapata dawa.

“Nashindwa. Mimi ndiye baba na mimi ndiye mama, baba yake alikataa kwamba huyu sim toto wake, nimempata na mwanaume mwingine nje ya ndoa, jambo ambalo si kweli.

“Hivyo, sina jinsi ya kufanya. Naumia, lakini ni mwanangu siwezi kumuacha akiteseka peke yake, ninafanya biashara ndogondogo, kuna wakati nalazimika kujinyima ili angalau mwanangu apate dawa,”.

Anasema mwanawe anapotumia dawa yahydroxyurea huwa na nafuu kubwa, humsaidia kupunguza vipindi vya maumivu makali vinavyojirudia mara kwa mara.

Kwa Julieth, kutafuta fedha za dawa ni sehemu ya mapambano ya kila siku ya kumlea mtoto anayeishi na Siko Seli.

Mahitaji ni makubwa

Veronica Mrema, Afisa Habari wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli Tanzania (SCDPCT), anasema jumuiya hiyo imekuwa ikisaidia baadhi ya watoto wanaoishi na ugonjwa huo kupata bima ya afya.

“Lakini mahitaji bado ni makubwa.  Kwa mfano tangu Januari mwaka huu hadi sasa, tumeweza kuwakatia bima ya afya watoto 36 tu kwa kushirikiana na mdau mmoja aliyetuunga mkono.

“Orodha tuliyonayo bado tuna wengine wengi ambao hatujaweza kuwafikia kwa sababu uhitaji ni mkubwa,” anasema.

Veronica anasema juhudi hizo hutegemea kwa kiasi kikubwa msaada kutoka kwa wadau mbalimbali.

“Tunaweza kuwasaidia pale tunapopata wadau wanaotuchangia na kutuwezesha kuwakati bima za afya. Kuna wadau pia hutusaidia kununua dawa hizi na sisi huzigawa bila malipo kwa baadhi ya mashujaa wenye uhitaji.”

Anasema, kwa muktadha huo, hatua ya Senegal kuanza uzalishaji wa hydroxyurea ni hatua inayostahili pongezi kubwa na ina maana kubwa katika mapambano dhidi ya Siko Seli.

“Kwa hatua ambayo Senegal imeweza kufikia, imetuletea faraja kubwa. Ni hatua kubwa, na mashujaa, wazazi na walezi wameipokea kwa furaha kubwa,” anasema.

Je, bei itashuka?

Kwa wagonjwa wanaonunua dawa kila siku, swali kubwa sasa ni iwapo uzalishaji wa hydroxyurea ndani ya Afrika utaweza hatimaye kushusha gharama zake.

Watu wanaoishi na Siko Seli Tanzania wana matumaini kwamba iwapo Senegal itafikia uwezo wa kuzalisha dawa kwa kiwango cha kutosheleza na kuisambaza katika nchi nyingine za Afrika, ikiwamo Tanzania, gharama za ununuzi zinaweza kupungua kwa kiasi kikubwa.

Kwa Rahma, ambaye kwa sasa hununua vidonge viwili kwa siku, matumaini hayo yana maana kubwa.

Uzalishaji wa dawa ndani ya Afrika unaweza kuwa mwanzo wa safari ndefu kuelekea upatikanaji wa dawa kwa gharama nafuu zaidi kwa wagonjwa wengi.

Hatua ya Senegal, kwa hiyo, si habari ya kiwanda pekee. Kwa wagonjwa wa Siko Seli kama Rahma, wazazi kama Felister na Julieth, na mashirika yanayopambana kusaidia wagonjwa nchini Tanzania.

“Ni ishara ya matumaini kwamba siku moja dawa muhimu kwa maisha yao zinaweza kupatikana kwa urahisi zaidi na kwa gharama ambayo familia nyingi zinaweza kuimudu,” anasema Veronica.

Kwa Afrika, huenda huu ukawa ni mwanzo wa kujenga uwezo wa kuzalisha zaidi dawa zinazohitajika na watu wake badala ya kuendelea kutegemea matumaini yanayotoka mbali.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement