Dar es Salaam
Uandaaji na usambazaji maudhui bora ya uelimishaji jamii pamoja na kuitangaza vema Tanzania kupitia majukwaa ya kidijitali ikishirikiana na taasisi za umma na binafsi ni dhamira ya Mtandao wa Wanablogu Tanzania [TBN].
Mwenyekiti wa TBN ametangaza hilo, alipozungumza katika kikao maalum baina ya viongozi wa TBN na ujumbe kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma [PSSSF].
Kikao hicho kimefanyika Makao Makuu ya TBN, Kijitonyama jijini Dar es Salaam ambapo maafisa hao wa PSSSF wamefanya ziara ya kikazi kwa ajili ya mazungumzo na TBN.
Msimbe amesisitiza wakati umefika kwa taarifa chanya za maendeleo kupewa nafasi kubwa zaidi katika ulimwengu wa kidijitali.
Amesema umuhimu, umeongezeka katika kipindi hiki ambacho teknolojia ya akili unde imewezesha taarifa kutafutwa, kupatikana na kusambazwa kwa kasi kubwa kuliko wakati mwingine wowote.
“Ni jambo la kusikitisha kuona taarifa zinazoongoza katika mifumo ya habari za kidijitali na kusambaa duniani kote kuhusu Tanzania mara nyingi ni zile zinazotokana na matukio ya udaku mitandaoni.
"Badala ya habari muhimu za maendeleo,” amesema Msimbe huku akitolea mfano halisi kwamba wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere.
"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizindua, ni mradi wenye manufaa makubwa kwa Taifa.
"lakini, baadhi ya taarifa zilizovuma zaidi mitandaoni kutoka Tanzania hazikuhusu umuhimu wa mradi huo, bali maisha binafsi ya nyota wa filamu na muziki,".
Msimbe amesema hali hiyo inaonesha umuhimu wa taasisi, vyombo vya habari na wadau wengine kushirikiana kuhakikisha mafanikio ya maendeleo ya Taifa yanapewa uzito unaostahili mitandaoni.
“TBN ipo tayari kushirikiana na taasisi mbalimbali kuongeza wingi wa taarifa chanya katika mifumo ya habari za kidijitali.
"Tunapaswa kuhakikisha Tanzania haitambuliki kwa habari zinazohusu maisha binafsi ya watu pekee, bali pia kwa mafanikio yake makubwa ya kiuchumi na kijamii,” amesema.
Msimbe ameeleza kufurahishwa na dhamira ya PSSSF ya kushirikiana na TBN katika kupanua utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu hifadhi ya jamii, mifumo ya pensheni na uwekezaji waliyonayo.
Ambainisha TBN ina wanachama zaidi ya 200 waliopo nchini na nje ya nchi, wenye uwezo wa kuwafikia wananchi wengi kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali.
“Tupo tayari kutumia uwezo, uzoefu na wigo mpana wa majukwaa ya wanachama wetu kutoa elimu sahihi za shughuli, huduma, uwekezaji na mifumo mbalimbali inayosimamiwa na PSSSF,” amesema.
Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, amesema mtandao huo una historia kubwa katika maendeleo ya habari za kidijitali nchini.
"Na tunajivunia kuwa na wanachama wenye weledi, uzoefu na uwezo mkubwa wa kuwafikia wananchi," amesema na kuongeza,.
"TBN ilianzishwa kwa dhamira ya kuhakikisha Tanzania inajenga taswira nzuri katika medani za kidijitali kwa kusambaza taarifa sahihi, zenye manufaa na zinazochochea maendeleo ya Taifa.
“TBN ipo tayari kushirikiana na PSSSF kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wananchi kwa lugha nyepesi, sahihi na inayoeleweka kupitia majukwaa ya kidijitali,” amesema Michuzi.
Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, amesema mtandao huo upo tayari kutumia waandishi wake mahiri na majukwaa ya wanachama wake kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye kuaminika.
Amesema taarifa hizo zitawawezesha wananchi kuelewa vyema haki na wajibu wao pamoja na fursa zinazopatikana kupitia mifumo ya hifadhi ya jamii.
Pallangyo amesema ushirikiano baina ya TBN na PSSSF unaweza kuwa daraja muhimu la kuiunganisha taasisi hiyo na wananchi.
"Hususan katika kipindi hiki ambacho majukwaa ya kidijitali yamekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya habari, elimu na maarifa," amesema.
Akizungumza kwa niaba ya PSSSF, Mkuu wa Msafara, Abdul Njaidi, amesema ziara hiyo ilikuwa sehemu ya jitihada za mfuko kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya habari na kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii.
Njaidi amewahakikishia viongozi wa TBN kuwa maombi, mapendekezo na hoja zote zilizowasilishwa katika mkutano huo zitafanyiwa kazi.
Amesema dhamira ya PSSSF ni kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu masuala ya pensheni na hifadhi ya jamii.
Pamoja na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo kwa manufaa ya wanachama na Taifa kwa ujumla.
Ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Abdul Njaidi na kuwajumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo.
Kwa upande wa TBN, mkutano huo umehudhuriwa na Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, mtaalamu wa mawasiliano Cathbert Kajuna na Mdhamini Issa Michuzi.

Chapisha Maoni