moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Siku walipoingia kambini, walijitambulisha "sisi ni mafundi nguo", ni mtizamo waliokuwa nao tangu huko walikotoka, wakitekeleza shughuli zao za kila siku.

Ushonaji wa mavazi ndiyo fani waliyochagua, wamejiajiri na wanapambana kutafutaa riziki zao, mkate wao wa siku pamoja na familia zao

Lakini mtizamo huo si waliotoka nao baada ya kupitia darasa la mafunzo maalum ndani ya siku 40 tu chini ya mkufunzi wa kimataifa 

Wasichana 30 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani walikuwa kambini katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA.

Ni fursa adhimu chini ya ufadhili wa Sisters in Imaan, Fashion for Empowerment, Demure by Shiba na VETA Chang'ombe hawakutoa hata senti tano, kulipia darasa hilo.

Umri wao ni kati ya miaka 15 hadi 28 ... wasichana 30, usiione [idadi hii kama namba] ndogo ni kubwa sana ukiingalia nyuma.

"Kwa sababu kila msichana mmoja aliyesaidika hapa anafamilia inayomtegemea nyuma.

"Hivyo, unazungumzia wasichana 30, familia 30, ndoto 30. Tumesaidia vijana hawa, tumesaidia jamii" amesema Mwenyekiti wa Sisters in Imani, Khadija Mjatta.

Taasisi hiyo inaamini kumpa kijana elimu na ujuzi ni kumpa nyenzo ya kujenga maisha yake, pamoja na kuwa na mchango chanya katika familia na jamii.

"Program hii haikulenga kuwafundisha vijana kushona pekee, bali kuwapa ujuzi unaoweza kuwawezesha kujiajiri na kupata kipato," amesema Khadija.

Natasha Jese ni miongoni mwa vijana walionufaika na mpango huo, amesema anashukuru mno kwani imempa mwanga mpya katika kipaji chake.

"Nitakachofanya, naenda kuwa mbunifu, na kuingia katika soko kuwa mmoja wa wabunifu chipukizi na inshalah nitakuja kuwa mbunifu mkubwa," amesema Natasha.

Wasichana hao wamefundishwa kwa vitendo utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za mavazi, ikiwamo nguo, pochi na kofia kwa kuongeza thamani na kupata bidhaa bora zaidi ya kibunifu na mtindo unaovutia zaidi.

"Hatua hii ililenga kuwapanua fikra zao na kujitambua kwamba wao si mafundi nguo tu" amesema Shiba na kuongeza,

".., ni wabunifu wa mavazi na unapoweka ubunifu unaongeza thamani ya bidhaa na hivyo unaweza kutengeneza kipato kizuri,".

Naye Salma Yusuph amesema "Nimejifunza vingi, hivyo mkae tayari kwa sababu designer mdogo naingia kazini, na mtegemee nitaitangaza nchi yetu,". 

Akizungumza katika mahafali ya kundi hilo la kwanza [cohot 1], Meneja wa VETA Kanda ya Dar es Salaam, Wilhard Soko, amepongeza juhudi za Sisters in Iman pamoja na wadau wake kwa hatua hiyo.

"Ushirikiano huu ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha vijana wanapata ujuzi wa ufundi unaoweza kutumika moja kwa moja katika maisha," amesema.

Soko amedokeza katika mpango huo Chuo cha VETA Chang’ombe kilichaguliwa kutokana na kuwa na miundombinu ya Textile and Fashion Design.

"VETA tunaendelea kupanua mtandao wa vituo vya mafunzo nchini, kutoka vituo takribani 29 mwaka 2001 hadi kufikia 80 kwa sasa" amesema.

Amesisitiza Serikali pia ina mpango madhubuti wa kuhakikisha idadi ya vyuo vya VETA inaongezeka hadi kufikia vituo 145.

"Kwa hiyo bado tunaalika wadau wengine nao waungane nasi, mimi moyo wangu unapenda sana 'vocational training' [mafunzo ya ufundi stadi].

"Vijana wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne, waje wajiunge na vyuo vyetu wapate elimu ya ufundi stadi, vimetapakaa nchi nzima.

"Kwa sababu kwa ufundi stadi, ujuzi ni fedha. Yaani unabuni bidhaa, unaitengeneza kisha unaiuza, unapata fedha," amesisitiza.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement