Dar es Salaam
Upanuzi wa wigo wa uelimishaji jamii kuhusu hifadhi ya jamii, umewaleta pamoja maafisa wa juu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma [PSSSF] na Tanzania Bloggers Network [TBN].
Mapema hii leo, katika ofisi za makao makuu ya TBN yaliyopo Kijitonyama Dar es Salaam maafisa wa PSSSF wamefanya ziara na kujadili na uongozi wa TBN namna bora ya kushirikiana kimkakati.
Mazungumzo hayo yaliyolenga kujenga ushirikiano wa manufaa ya pande zote mbili yakijikita katika kuimarisha uhusiano wa kisekta kwenye masuala ya habari.
Pia, uelimishaji wa umma, na usambazaji wa maarifa sahihi kuhusu mifumo ya pensheni na uwekezaji nchini.
Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, ameeleza utayari wa mtandao huo kusimama kidete kama chombo cha kutoa elimu na kusambaza maarifa sahihi kwa umma na katika nyanja za kidijitali.
Hata hivyo, amesisitiza ili kufikia malengo hayo kwa ufanisi zaidi, ni muhimu wanachama wa TBN, wakapatiwa kwanza mafunzo ya kina na ya kutosha kuhusu shughuli na uendeshaji wa mfuko huo.
Ushirikiano huo unatazamiwa kufungua ukurasa mpya katika matumizi ya vyombo vya habari vya mtandaoni kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wengi zaidi nchini.
Mkuu wa msafara huo kutoka PSSSF, Abdul Njaidi, ameeleza kwamba ziara hiyo inalenga kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya habari pamoja na kutoa elimu kwa jamii.
Amewahakikishia viongozi wa TBN kwamba maombi na hoja zote zilizowasilishwa zitafanyiwa kazi.
"Ushirikiano huu mpya unalenga kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu masuala ya pensheni na uwekezaji unaofanywa na PSSSF.
Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, ambaye ameshiriki katika mkutano huo, ameeleza kwamba mtandao huo wenye historia kubwa unajivunia weledi na ufanisi mkubwa.
Amesema TBN ipo kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inasomeka vyema katika medani za kidijitali ili kuchochea na kutanua zaidi gurudumu la maendeleo ya taifa.
Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, ameongeza "Mtandao huu upo tayari kutoa waandishi wake mahiri na kutumia majukwaa yake mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi.
".., na za kuaminika zitakazowezesha kufanikiwa kwa utekelezaji wa majukumu ya wananchi na wadau wa maendeleo," amesisitiza.
Katika mkutano huo, ujumbe wa PSSSF ulioongozwa na Abdul Njaidi, ulijumuisha maofisa wengine akiwemo Regina Kumba, Grayson Mgunda, na Doreen Lyimo.
Kwa upande wa TBN, viongozi waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, mtaalamu wa mawasiliano, Cathbert Kajuna na Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi.

Chapisha Maoni