Na Veronica Mrema
Kwa wanawake, kufikia ukomo wa hedhi si mwisho wa hedhi pekee. Ni mwanzo wa kipindi cha mabadiliko ya mwili yanayoweza kuathiri utendaji kazi wa mwili mzima.
Suala la uratibu wa usingizi, hisia, uwezo wa kuzingatia mambo, mahusiano na mengineyo kwa siku nzima, huweza kuathirika.
Johari Kibena alianza kuona mabadiliko kadhaa, alipofikia umri wa miaka 40, alipata vipindi vya joto kali ghafla, alikosa usingizi na kuhisi hasira.
Kitu kingine kilichomsumbua zaidi kilikuwa hali ya akili yake. Muda mwingi alikuwa anahisi ni kama vile mawazo yake yamekwama.
Kazi ambayo hapo awali aliifanya vizuri na kuikamilisha ndani ya muda mfupi, sasa alijikuta akitumia muda mwingi pasipo kuikamilisha.
Changamoto, anashindwa kuzingatia mambo kama zamani na wakati mwingine alihisi kuna kitu kisicho cha kawaida kinachomtokea.
Awali hakujua dalili hizo zinaweza kuhusishwa na mabadiliko ya homoni yanayoambatana na kuelekea ukomo wa hedhi, alianza kutafuta maelezo mengine.
“Nilifikiri labda nimechezewa michezo ya nguvu za giza,” anasema Johari, akieleza namna alivyokuwa akijaribu kuelewa mabadiliko aliyokuwa akipitia.
"Nimetumia dawa nyingi mbalimbali, watu wamekuwa wakisema tumia hii na ile, si unajua tena sisi huwa tunaenda madukani na kununua tu, nimefanya hivyo lakini sijapata matokeo chanya!,".
Siku moja alipokwenda katika kikundi chao cha vikoba ndipo alipoanza kubaini mambo ni tofauti na vile alivyofikiri kwanza.
"Kuna mama mmoja alikuwa anatusimulia kuhusu mambo aliyopitia katika ukomo wa hedhi, ndipo nikalinganisha na yangu, nikaona kumbe nilikuwa nakabiliana na hali hiyo pia.
"Nilichukua hatua na kwenda hospitalini, sasa nipo kwenye matibabu" anasema Johari.Simulizi yake inaamsha swali kuu, linalojenga msingi wa makala haya...
Tanzania inajua kwa kiasi gani kuhusu wanawake wanaofikia 'menopause' na changamoto wanazopitia na ufumbuzi wake upo kwa kiwango gani?
UHALISIA WA MAMBO
Tanzania ina takwimu za kitaifa zinazoonyesha ukubwa wa wanawake wanaofikia menopause, lakini bado kuna pengo la taarifa kuhusu wanachopitia wanawake hao katika maisha yao ya kila siku.
Kwa mujibu wa Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey 2022 [TDHS-MIS 2022], 0.6% ya wanawake wenye umri wa miaka 30 hadi 49 walitambuliwa kuwa 'menopausal' kwa mujibu wa vigezo vilivyotumika katika utafiti huo.
Takwimu hizo zinaonesha ongezeko kadiri umri unavyoongezeka. Kwa wanawake wenye miaka 30 hadi 34, kiwango kilikuwa 3.1%, huku kwa wenye miaka 35 hadi 39 kikiwa 4.5%.
Kwa kundi la miaka 40 hadi 41 kilikuwa 8.2%, miaka 42 hadi 43 11% na miaka 44 hadi 45 12.1%.
Kwa wanawake wenye miaka 46 hadi 47, kiwango kilifikia 26.6%, na kwa wenye miaka 48 hadi 49 kilikuwa 46.1%.
Hata hivyo, takwimu hizi zinaonyesha zaidi ni wanawake wangapi walikuwa wamefikia menopause wakati wa utafiti, si kwa kina namna hatua hiyo inavyoathiri maisha yao.
Hazielezi, kwa mfano, ni wanawake wangapi wanapata joto kali mwilini, kukosa usingizi, mabadiliko ya hisia.
Kushindwa kuzingatia au hali ya “brain fog”, wala ni kwa kiwango gani dalili hizo zinaathiri kazi, familia na mahusiano.
Hapo ndipo pengo la taarifa linapoonekana.
M24 TANZANIA imefanya mahojiano maalum na Profesa Muzdalifat, Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi na Medical Director wa Aga Khan Hospital,
Anasema kuna haja ya tafiti zaidi zitakazosaidia kuelewa kwa kina hali na mahitaji ya wanawake wanaopitia menopause.
Kwa hiyo, si kwamba Tanzania haina kabisa takwimu za menopause. Badala yake, swali linalobaki ni: wanawake hao wanapitia nini, kwa kiwango gani na wanahitaji huduma gani?
'MENOPAUSE' NI HATUA YA MAISHA
Profesa Muzdalifat anasema 'menopause ni hatua ya kawaida katika maisha ya mwanamke.
Hatua hiyo, inaweza kutokea katika umri wa kati ya miaka 45 na 55, wakati ovari zinapopunguza uzalishaji wa homoni ya 'estrogen'.
Kabla ya kufikia 'menopause' yenyewe, mwanamke hupitia kipindi cha perimenopause, ambacho huambatana na mabadiliko ya homoni na dalili mbalimbali.
Dalili hizo zinaweza kujumuisha joto kali mwilini, kukosa usingizi, maumivu ya kichwa, mabadiliko ya hisia, hasira, kizunguzungu.
Kusahau, kushindwa kuzingatia, hali ya “brain fog”, pamoja na maumivu ya misuli na viungo.
Kwa baadhi ya wanawake, dalili hizi zinaweza kuonekana kama matatizo mengine kabisa. Hilo ndilo lililomtokea Johari.
Bila taarifa sahihi, mwanamke anaweza kuanza kutafuta maelezo ya mabadiliko anayopitia katika maeneo mengine kabla ya kufahamu kuwa yanaweza kuhusishwa na kipindi cha perimenopause au menopause.
Menopause kazini: Kwa Dkt. Zuhura Majapa, changamoto ya menopause haishii hospitalini. Inaweza kuingia kazini.
Dkt. Zuhura, ambaye pia amewahi kuwa Mganga Mkuu katika hospitali, anasema amekutana na hali ambazo wanawake waliokuwa katika kipindi cha 'perimenopause' au 'menopause'.
Anasema walionekana kupoteza ufanisi kazini, huku sababu ya mabadiliko hayo ikiwa haikueleweka.
"Mwanamke anaweza kupata usingizi hafifu usiku, kuamka akiwa amechoka, kushindwa kuzingatia au kupata mabadiliko ya hisia.
"Akiwa kazini, anaweza kuchelewa kukamilisha ripoti au kushindwa kufanya kazi kwa kasi ile aliyozoea.
"Tatizo linakuja pale ambapo mabadiliko hayo yanatafsiriwa moja kwa moja kama uzembe," anataja yale ambayo amewahi kuyashuhudia.
Dkt. Zuhura anatoa mfano wa mfanyakazi anayeshindwa kuwasilisha ripoti kwa wakati na kuishia kukosolewa na mkuu wake bila mtu kujiuliza kama kuna changamoto nyingine inayomkabili.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa si kila kushuka kwa utendaji kazini kunapaswa kuhusishwa na menopause. Kuna wakati uzembe unaweza kuwa uzembe.
Kinachohitajika, kwa maoni yake, ni uelewa. Badala ya mazingira ya kazi kuishia kwenye lawama na barua za onyo.
Dkt. Zuhura anasema elimu na mazungumzo yanaweza kusaidia waajiri na wafanyakazi kuelewa mabadiliko yanayoweza kutokea katika hatua hii ya maisha.
Kwa mwanamke, pia kuna maisha nje ya ofisi. Dkt. Zuhura anaeleza kuwa menopause inaweza kuathiri mahusiano ya kifamilia na ndoa.
Baadhi ya wanawake wanaweza kupoteza hamu ya tendo la ndoa au kupata hali inayofanya tendo hilo kuwa na usumbufu.
Katika mazingira ambayo mwenza hajui kinachoendelea, mabadiliko hayo yanaweza kutafsiriwa vibaya.
Ndiyo maana, kwa mtazamo wake, elimu kuhusu menopause haipaswi kuwafikia wanawake pekee. Familia na wenza nao wanahitaji kuelewa.
HRT: Suluhisho si kujitibu Kadiri uelewa kuhusu dalili za menopause unavyoongezeka, baadhi ya wanawake wanaweza kutafuta njia za kupunguza changamoto wanazopitia.
Ikiwemo kutumia dawa za Hormone Replacement Therapy, maarufu kama HRT. Lakini matumizi ya dawa hizi yanahitaji tathmini ya kitabibu.
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania [TMDA] inaeleza kuwa HRT ni miongoni mwa dawa zinazotakiwa kutolewa kwa cheti cha daktari.
M24 TANZANIA imefanya mahojiano maalum na Dkt. Yonah Mwalwisi, mtaalamu wa famasi na Mkurugenzi wa Udhibiti wa Dawa za Binadamu na Wanyama katika TMDA,
Anasema matumizi ya HRT yanapaswa kufanyika baada ya ushauri na usimamizi wa mtaalamu wa afya.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMDA, jumla ya dawa nane za HRT zimesajiliwa nchini katika mfumo wa vidonge, kapsuli na pessaries.
Hata hivyo, uwepo wa dawa hizo sokoni hauimaanishi kila mwanamke mwenye dalili za menopause anapaswa kuzitumia.
Profesa Muzdalifat anaeleza "Mwanamke anayehitaji HRT anapaswa kwanza kufanyiwa tathmini ya kitabibu ili kubaini kama anafaa kutumia dawa hizo na kama ana sababu zinazoweza kuongeza hatari ya madhara.
“Unahitaji kwanza umuelimishe yule mtu, umfanyie evaluation kama yupo kwenye risk ya kupata hatari,” anasema.
Aina ya dawa, dozi, njia ya matumizi na muda wa kutumia vinaweza kutegemea hali ya mwanamke, umri, historia ya afya na sababu nyingine za hatari.
TMDA inaeleza kuwa matumizi yasiyofaa yanaweza kuhusishwa na hatari kama kuganda kwa damu kwenye mishipa na kiharusi.
Kwa baadhi ya wanawake wanaotumia mchanganyiko wa estrogen na progestogen kwa muda mrefu, kunaweza pia kuwa na ongezeko la hatari ya saratani ya matiti.
Kwa mwanamke mwenye kizazi, matumizi ya estrogen pekee bila progestogen inayofaa yanaweza kuongeza hatari ya saratani ya ukuta wa kizazi.
Madhara mengine yanaweza kujumuisha kutokwa damu ukeni isivyo kawaida, maumivu ya matiti, maumivu ya kichwa, kuhifadhi maji mwilini na mwingiliano na dawa nyingine.
TAKWIMU ZA TMDA
Takwimu za TMDA zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025, jumla ya taarifa 2,624 za matukio yaliyoshukiwa kuwa madhara au athari za dawa zilihusishwa na dawa za homoni zinazotumiwa na wanawake.
Mwaka 2021 kulikuwa na taarifa 14, mwaka 2022 zilikuwa 28, mwaka 2023 zilipanda hadi 1,052, mwaka 2024 zilikuwa 726 na mwaka 2025 zilikuwa 804.
Hata hivyo, takwimu hizi zinahitaji kutafsiriwa kwa uangalifu. Hazimaanishi kuwa taarifa zote 2,624 zilitokana na HRT pekee.
Dkt Mwalwisi anasema hadi sasa hakuna taarifa katika kipindi hicho iliyohusisha madhara makubwa yaliyosababisha ulemavu wa kudumu au kifo.
Pia, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hakuna bidhaa ya HRT iliyoripotiwa au kubainika kuwa haijasajiliwa, bandia au yenye ubora duni.
"Wanawake wanaotumia HRT wanapaswa kutumia dawa zilizosajiliwa, kununua kupitia maeneo halali kama hospitali.
"Vituo vya afya na maduka ya dawa, na kufuata maelekezo kuhusu dozi, njia na muda wa matumizi," anatoa rai.
KLINIKI MAALUM
Profesa Muzdalifat anadokeza zaidi, suala la 'menopause' linahitaji zaidi ya dawa. Tanzania inahitaji miongozo ya kitaifa kuhusu 'menopause'.
Huduma maalumu na wataalamu waliopewa mafunzo ya kutosha katika eneo hilo, sasa hivi bado kuna pengo katika utaalamu maalumu wa 'menopause' nchini.
Jambo ambalo limemsukuma yeye mwenyewe kuendelea na mafunzo yanayohusiana na eneo hilo kupitia programu ya nchini Uingereza.
Pia changamoto nyingine ni gharama za matibabu kwa baadhi ya wanawake wanaohitaji matibabu.
"Kwa mwezi mwanamke mmoja anaweza kuhitaji wstani wa TZS 300,000 hadi 400,000 kwa ajili ya baadhi ya dawa na huduma zinazohusiana na matibabu hayo.
Hivyo, suala la kama huduma hizi zinagharamiwa kwa kiwango gani na bima pia linahitaji mjadala zaidi, hasa ikiwa Tanzania inalenga kujenga huduma jumuishi kwa wanawake wanaopitia 'menopause'.


Chapisha Maoni