moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Kuna kundi dogo mno la wanawake ambao hufika moja kwa moja hospitalini kutibiwa, kwa sababu ya changamoto ambazo wanapitia kuelekea kipindi cha ukomo wa hedhi 'menopause' Tanzania.

'Menopause" ni tendo la kibaiolojia kwa walio wengi hutokea kati ya umri wa miaka 45 mpaka 55 na kabla ya kukoma kabisa kwa hedhi na huambatana na mabadiliko mbalimbali wanayopitia ambayo husababishwa na kupungua kwa homoni ya 'eostrejen'.

Homoni hii ndiyo Ile ambayo hutolewa kwenye vifuko vya mayai kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke katika maisha yake.

Kipindi cha 'menopause' homoni hiyo huanza kupungua taratibu, taratibu, mwili nao hupata taarifa kwa hisia mbalimbali, baadae mtu husika hupata mabadiliko ya mwili mzima.

Kuna wanaopata mabadiliko kwenye ubongo [yaani ule] ufahamu unaanza kupungua, anakuwa anaanza kusahau sahau, au anahisi kizunguzungu, anakosa usingizi au kichwa kinamuuma.

Kuna wanaopata mabadiliko ya 'mood', mara ana hasira, zile dalili zinashuka mwili mzima, kwa hiyo pia ngozi inaweza kuwa inabadilika. viungo vyake vyake vyote vya mwili vinaanza kumuuma.

Maumivu ya misuli, kupungua ama kuongezeka uzito, wakati mwingine hata kushindwa kutembea vema anapoamka asubuhi mpka achangamke changamke pamoja na changamoto nyinginezo. 

Tanzania ina takwimu za kitaifa ambazo zinazoonesha idadi ya wanawake wanaofikia 'menopause'. 

Lakini bado kuna pengo la taarifa kuhusu wanachopitia wanawake hao aina na ukubwa wa dalili, athari zake katika kazi na mahusiano, uelewa wao kuhusu 'menopause', pamoja na huduma wanazohitaji.

Kwa mujibu wa 'Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey 2022', 10.6% ya wanawake wenye umri wa miaka 30 hadi 49 walikuwa wamefikia 'menopause'.

Kwa wanawake wenye umri wa miaka 48 hadi 49, kiwango hicho kilikuwa 46.1%.

Hata hivyo, takwimu hizo hazitoi picha kamili ya changamoto zinazowakabili wanawake wakati wa kuelekea na baada ya 'menopause'.

Profesa Muzdalifat Salim Abeid, Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, ni Medical director Hospitali ya Agakhan katika mahojiano maalum na M24 TANZANIA amesema kuna haja ya kufuatilia kwa ukaribu wanawake hawa.

"Sisi [Agakhan] tuliona vema kuanzisha kliniki maalum kabisa kwa wanawake hawa, nimekuwa napata baadhi yao wakitaka niwaanzishie dawa za homoni, lakini utaratibu haupo hivyo.

"Lazima ukae na kuzungumza na mtu husika, ufanye tathmini maana si kila umri mtu anapewa dawa hizi, sasa unamuuliza mtu unajua si kila mtu anastahili kutumia?, je unajua athari zake?.

"Hajui, isipokuwa anadai amepewa ushauri na rafiki yake aliyekutana naye kwenye kikundi au kazini, hata hawa ambao tunapata kliniki yetu, unakuta mara nyingi kwa sababu ya uelewa mdogo, mwanzo wanakuwa wamekaa nyumbani wanaona ni kawaida.

Ameongeza "Au wanashauriana na wale waliopita nao wanaambiwa ni uzee tu watakuwa sawa, hata wakienda hospitali wanakuwa wametibiwa vitu vingi na haikuwasaidia, wanakuwa wameshindwa kugundua mapema, ni kwa sababu uelewa mdogo.

Lakini si kila mwanamke anayepitia changamoto za kipindi cha ukomo wa hedhi anastahili kuanza kutumia dawa za homoni [Hormone Replacement Therapy - HRT] ili kusaidia miili yao kuratibu vema hali hiyo.

"Kwanza kumfanyia mwanamke tathmini ili kubaini kama anafaa kutumia dawa hizo na kama ana sababu zinazoweza kuongeza hatari ya kupata madhara.

“Unahitaji kwanza umuelimishe yule mtu, umfanyie evaluation kama yupo kwenye risk ya kupata hatari,” amesisitiza Profesa Muzdalifat.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania [TMDA] imesisitiza dawa hizo hazipaswi kutumiwa kiholela bila ushauri na usimamizi wa mtaalamu wa afya.

Mtaalamu wa famasi na Mkurugenzi wa Udhibiti wa Dawa za Binadamu na Wanyama TMDA, Dkt. Yonah Mwalwisi  katika mahojiano haya maalum amesema HRT ni miongoni mwa dawa zinazotakiwa kutolewa kwa cheti cha daktari.

TMDA mpaka sasa imesajili jumla ya dawa nane za HRT katika mfumo wa vidonge, kapsuli na pessaries ndani ya soko la Tanzania.

HRT inaweza kuwa na manufaa kwa baadhi ya wanawake wenye dalili za menopause, lakini matumizi yake yanapaswa kufanyika baada ya tathmini ya kitabibu na chini ya usimamizi wa mtaalamu wa afya.

Baadhi ya hatari zinazoweza kuhusishwa na matumizi ya HRT, kwa mujibu wa TMDA, ni kuganda kwa damu kwenye mishipa, kiharusi na ongezeko la hatari ya saratani ya matiti kwa baadhi ya wanawake na hata saratani katika ukuta wa uzazi.

Madhara mengine yanaweza kujumuisha kutokwa damu ukeni isivyo kawaida, maumivu ya matiti, maumivu ya kichwa, kuhifadhi maji mwilini na mwingiliano na dawa nyingine.

Takwimu za TMDA zinaonesha, kati ya mwaka 2021 na 2025, jumla ya taarifa 2,624 za matukio yaliyoshukiwa kuwa madhara au athari za dawa zilihusishwa na dawa za homoni zinazotumiwa na wanawake.

Kwa kina zaidi usikose kufuatilia makala maalum, uchambuzi wa kina kuhusu suala hili, ambayo tutaichapa ndani ya ukurasa huu Septemba 25, 2026. Karibu sana.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement